2018 Mwaka wa Masahihisho

8:44:00 PM Unknown 0 Comments

2018
MWAKA WA MASAHIHISHO
Kama wanadamu tunakosea na kila mwaka unatupa fursa ya kufanya mambo mawili mosi, unatupa fursa ya kufanya mambo mazuri na sahihi; pili, unatupa fursa ya kukosea. Amesema mzaburi, “BWANA kama wewe ungehesabu maovu yetu nani angesimama?” Kwa siku zaidi ya mia tatu za mwaka 2017 yako mengi yasiofaa ambayo tumeyatenda na hayapaswi kuendelea kufanyika; yako pia ya kufaa ambayo yanatakiwa kuendelezwa katika mwaka 2018. Yako pia mazuri ambayo tulitakiwa kufanya na hatukuyafanya!
Kwa kuwa katika mwaka 2017 kulikuwa na makosa na mapungufu ambayo kwa hekima ya kawaida huwa tunayachukua kama shule kwa ajili ya mwaka 2018 basi mapungufu hayo yasituumize. Hatutegemei katika mwaka 2018 kuendelea na makosa ya 2017 ambayo tumesha hitimu shule yake.
Tunaweza kutaka mabadiliko katika mwaka 2018 na tusiweze, pengine nguvu zetu ni kidogo na hutuwezi kugeuka, lakini uko msalaba na iko damu ya Yesu! Nguvu ile iliyohuisha mwili wake kaburini naye akafufuka mzima, yaweza kutuhuisha roho zetu na dhambi na kutufanya kuwa watu bora kabisa katika mwaka 2018. Najua nguvu zetu ni kidogo lakini panapo msalaba pana nguvu kubwa ya mageuzi.
Mamilioni ya watu wamekuwa wakipinduliwa kwa nguvu ya msalaba toka utumwa wa dhambi mpaka utakatifu. Nguvu hii ni kwa ajili yetu katika mwaka 2018. Kama tulikosea 2017 imetosha sasa, sasa tumejifunza, sasa ni wakati wa kugeuka. Moja na malengo yako katika mwaka 2018 ni muhimu kuwa kufanya yale uliyotakiwa kuyafanya katika mwaka 2017 na hukufanya. Hii pia ni lengo la kizazi cha sasa yaani, kufanya yale ambayo vizazi vilivyopita vilitakiwa kufanya na havikufanya. Mwalimu Jim Rohn amesema jambo la kufanana na somo hili, “Don’t let learning from your own experiences take too long. If you have been doing it wrong for the last ten years, I would suggest that’s long enough
Masahihisho ni jambo jema kabla ya hukumu, masahihisho yanatupa nafasi ya kujitathmini, kujikosoa na kuanza upya, kamwe yasitazamwe kama hukumu. Katika kitabu nikipendacho cha, “The Virgin Way” kilichoandikwa na Richard Branson imesisitizwa kama unafanya makosa na uyafanye haraka. Kipindi chako cha kukosea na kujifunza kutokana na makosa kisiwe kipindi kirefu mno. Hii imepelekea kukusihi, mwaka 2018 iwe muda wako wa kuanza upya. If you’re doing a mistake do it very quickly in these few days before 2018.
Tufikapo 2018 tuwe wapya tayari kwa ushindi.
Barikiwa!

0 comments :

Inachukua Muda....

5:32:00 PM Unknown 0 Comments

 
Inachukua Muda...

Tunaishi katika ulimwengu ambao karibu kila eneo watu hutaka huduma kwa haraka; usafiri wa haraka (mwendokasi), chakula cha haraka (fast food), mikopo ya haraka, huduma za kifedha na afya kwa haraka (fast track) n.k ! Hakuna anayetaka kukaa muda mrefu kwenye foleni kusubiria huduma. Maendeleo ya sayansi na tekinolojia yamerahisisha upatikana wa huduma nyingi katika jamii na kwa haraka zaidi wakati huu, kuliko miaka kumi iliyopita.
Pamoja na mchango mkubwa wa sayansi na tekinolojia katika upatikanaji wa huduma, watu wengi wamesahau baadhi ya kanuni muhimu za mafanikio ya kweli; katika ulimwengu huu wa haraka haraka, jamii imesahau kuwa mafanikio ya kudumu huchukua muda kuyajenga. Kanuni hii ni rahisi sana kusahaulika katika ulimwengu wa haraka.  Ya kwamba mahusiano mazuri yanachukua muda kuyajenga, familia nzuri inachukua muda kuijenga, mafanikio ya kifedha, huduma, taaluma pamoja na 'career' haya yote huchukua muda kuyajenga.
Ni mwanafunzi anayeamini katika ulimwengu wa haraka kwenye taalumu hufanya bidii aweze kuiba au kuibia kwenye mtihani, ni kijana anayeamini tu katika ulimwengu wa haraka hushinda kijiweni "akibeti" ili kufikia mafanikio ya kifedha. Ndio maana ni rahisi kwa mtu kwenda kucheza "desi" ili apokee mara asilimia mia tatu (300%) kuliko kuwekeza kwenye ufugaji wa kuku, kwa sababu anaona hatapata hiyo asilimia mia tatu haraka. Hutaka kupata kwa haraka bila kufanyia kazi. Nitajie tajiri aliyeko kwenye orodha ya matajiri kwa sababu alishida bahati nasibu au desi; go back to Work!!
Watu ambao hawajui kuwa mahusiano bora na imara huchukua muda kuyajenga wakitofautiana kidogo huvunja uhusiano huo na kama ni wana ndoa hutishia kutengana kabisa. Mzazi ambaye anayeamini katika ulimwengu wa haraka katika malezi, hana muda wa kukaa  na watoto kuwafundisha na kufuatilia malezi yao kwa karibu; wakishapotea na kuharibika kimwenendo hukimbilia kwa watumishi wamuombee ili wapone na kurudi kwenye njia sahihi kwa haraka, amesahau alikuwa na nafasi katika kujenga mwenendo bora kabla.
Anayejenga nyumba juu ya mwamba hutumia muda kuijenga, na kwa sababu hiyo nyumba hiyo itakuwa imara kuliko anayejenga juu ya mchanga.  Kuna baadhi ya maeneo ulimwengu wa haraka hauleti matokeo bora, bali kanuni ya muda!  Mwenyehekima mmoja amewahi kusema "usikimbie mahali panapokutaka kutembea; na usitembee mahali panapokutaka kukimbia "
Mali iliyopatikana kwa haraka itapunguka; Bali yeye achumaye kidogo kidogo atazidishiwa-Mithali 13 :11
There's a place for you at the top

0 comments :

Mtu Jasiri

1:31:00 PM Unknown 0 Comments

MTU JASIRI
Katika ulimwengu wa sasa majasiri wengi hawajulikani. Dunia ya leo imewatukuza wasemaji ikaacha wakimya, imemdharau mtu mpole ikampa heshima mtu mkali. Katika vikao wasikilizaji wazuri hawatambuliwi kama majasiri wa kusema. Kusikiliza si jambo jepesi, hakuna mtu mgumu kumsikiliza kama mtu mkorofi na mtu asiyejua.
Si wengi wanauzoefu na uwezo wa kusikiliza kwa makini, wengi hupenda kusikilizwa si kusikiliza. Huwezi kusikiliza na huku unatazama televisheni au unasikiliza redio. Ni rahisi kuukusanya mwili lakini si akili ya usikivu. Huwezi kusikiliza ikiwa unataka kusema, unaweza kusikiliza ikiwa unataka kusikiliza. Alisema Winston Churchil, “Courage is not only what it takes to stand up and talk but courage is also what it takes to sit down and listen” kwa tafsiri “Inamhitaji mtu jasiri kusimama na kuzungumza, lakini inamhitaji mtu jasiri pia kukaa kimya na kusikiliza”.
Amenukuliwa mzee Kinana Katibu Mkuu CCM akisema, “kiongozi lazima asikilize wananchi”.  Kiongozi si lazima awe kwenye kampuni, kwenye taasisi ya umma au kwenye siasa, badala yake anaweza akawa kwenye familia baba wa familia, mama wa familia, kaka wa familia au dada wa familia.  Siku chache katika nafasi ya uongozi jambo kubwa nililojifunza ni kwamba, uongozi ni kusikiliza, It’s all about listening!
Ni raha kusikiliza, msikivu anaraha kwa kuwa anauelewa mpana. Je, ungependa kuitwa mwongeaji sana au msikivu sana. Je, ungependa mtu akitoka nyumbani kwako aseme hajawahi ona msemaji kama wewe au aseme hajawahi kukutana na mtu msikivu kama wewe.  Si vema mtu akushangae kwa kusema, “What a talker
Ni mtu jasiri peke yake anaweza kuwasikiliza waliotengwa, waliosetwa na wasio stahili katika jamii. Si rahisi kuwasikiliza wahalifu, mtu jasiri pekee anaweza kufanya hivyo.
Kwa kiongozi mpya wa nafasi na ngazi yoyote nasisitiza neno moja, sikiliza, sikiliza, sikiliza.
Tukutane kileleni wasikivu wanapopatikana.

0 comments :

Umeitwa kuongoza

10:03:00 AM Unknown 0 Comments

UMEITWA KUONGOZA
Mtu hafanyiki kiongozi kwa cheo au nafasi aliyonayo katika Nyanja za siasa, taasisi, kanisa n.k; bali ni kusudi (purpose) linalozaa maono (vision) ndani yake. Sifa kuu ya kiongozi ni kuwa na maono chanya kwa mustakabali wa anachokiongoza. Mahali ambapo hakuna maono hakuwezi kuwa na uongozi, kunaweza kuwa na cheo lakini hakuna uongozi!.
Maono ndio hufanya kiongozi awe kiongozi. Siku zote watu hawafuati mtu, wanafuata maono yake. Mahali ambapo nguvu hutumika ili kufanya watu wafuate (follow) ni kwa sababu hakuna maono yanayoshawishi watu kufuata kwa utashi na hiari yao.
Ikiwa kila mtu ameumbwa kwa kusudi maalumu, basi ni ukweli uliowazi kuwa kila mtu ameitwa kuongoza katika eneo la kusudi lake; kumbuka maono ndio yanayotengeneza kiongozi na sio kinyume chake, na maono ni picha ya kusudi ndani ya mtu. Maono ndio yaliyotengeneza mtu anaitwa mama Theresa, Nelson Mandela, J. K. Nyerere, Martin Luther King Jr n.k. Maono ndio yanayotengeneza makampuni, mashirika, taasisi, ajira kwa watu, biashara, miradi (projects) na sio kinyume chake. 
Ninaposema kila mtu ameitwa kuongoza sina maana kila mtu ameitwa kuwa mwanasiasa (wapo waliokusudiwa hapa pia); na wala si swala la kuwa na cheo au kutokuwa nacho! Bali kwa kuwa umeumbwa kwa kusudi fulani, inatosha kujua mahali uongozi wako unahitajika. Uongozi wako unaweza hitajika kwenye eneo la biashara, eneo la tekinolojia, eneo la sanaa na michezo, eneo la siasa, jamii (social leader), afya, uchumi au madhabahu! (Your area of gifting and passions)
Kwanini nasema umeitwa kuongoza? Kwa sababu maono hutolewa kwa mtu mmoja kwanza kabla hayajapata wafuasi wengi; Na pia kila mtu ana eneo au nafasi yake kwa kadri ya kusudi la kuumbwa kwako sawasawa na maono aliyonayo; Ni kwa sababu ulichopewa si kwa ajili yako, ni kwa ajili ya wengine (japo na wewe utanufaika), mfano. Mwalimu hawi mwalimu kwa ajili yake, japo hupokea malipo ya kazi hio!  Kumbuka, hakuna mti unakula matunda yake wenyewe!!
There's a place for you at the top

0 comments :

Mtu mgumu kutawalika

2:17:00 PM Unknown 0 Comments

 
MTU MGUMU KUTAWALIKA
Ni rahisi sana kutazama wengine na sisi wenyewe tukasahau kujitazama na kujitathmini. Tunaweza tukayajua sana mapungufu ya wengine na tukasahau wapi tunapungua. Imenenwa, “Unakiona kibanzi kwenye jicho la nduguyo na unaacha kutazama boriti ndani ya jicho lako”.
Profesa na Mhadhiri wa chuo kikuu cha Havard cha Nchini Marekani bwana Bill George anaandika hivi katika moja ya vitabu vyake, “The hardest person you will ever have to lead is yourself”.
Wewe ndio mtu usiye tawalika, wewe ndio mtu mgumu kwa viongozi wako. Mara nyingi tumezoea kusema ni fulani na kujisahau kwamba, tunayo mapungufu makubwa. Kwangu mimi mtu mgumu kumtawala ni mimi, na wewe ni vema ujijue vema.
Miili yetu inaasili ya kutokutawalika. Ukipanga mpango wa kuacha michepuko unaweza kushuhudia vita dhahiri ambayo mwili unainua, hali kadhalika unapopanga kufunga. Biblia inasema, “Ifungeni dhabihu kwa kamba kando ya madhabahu”. Imenenwa pia, “Itoeni miili yenu kama dhabihu”. Kwa nini sadaka ifungwe kwa kamba? Isipofungwa itagoma au itakimbia. Isipofungwa haitawaliki.  Warumu 12:1-3
Kufungwa ni kulazimisha, kutia adabu, kufanya tena na tena mpaka maadili mema na utii uwe sehemu ya maisha yetu. Ni ngumu ni lazima ukaze. Wachichanji wanajua, ili uchinje nguruwe unahitaji kufanya kazi, ili utoe fungu la kumi unahitaji kujua kuacha matamanio binafsi na kuwa mtii kwa Bwana.
Tukutane juu.

0 comments :

Chagua kuendelea mbele

12:52:00 PM Unknown 0 Comments

 
Chagua Kuendelea Mbele
Mara nyingi tunapokutana na changamoto katika kufikia yale tuliyopanga au kutazamia; tunaweza kuchagua mambo mawili tu, kusonga mbele au kukata tamaa na kutafuta sababu ya kulaumu na kughairi kuendelea mbele! Kile utakacho kiamua baada ya kukutana na changamoto ndicho utakachokipata baada ya changamoto hiyo kupita.
"Ukifikiri kama unaweza au hauwezi, upo sahihi "
Yaani ukifikiri na kuona kama jambo fulani unaliweza au utaweza basi ujue upo sahihi; na ukiona au kufikiri jambo fulani hauliwezi au hautaliweza basi ujue upo sahihi pia!  Na hii ndio sababu inayofanya wengine waendelee mbele na wengine kuishia kulalamika na kughairi kuendelea 'utukufu' ulio mbele yao
" Bwana akamwambia Musa, Mbona unanililia mimi? Waambie wana wa Israeli waendelee mbele" Kutoka 14 :15
Siri ya kufanikiwa wakati wa changamoto sio kurudi nyuma au kukata tamaa, siri ya mafanikio ya kweli ipo katika kuendelea mbele. Thomas Edison, mwanasayasi na mgunduzi amewahi kusema "Our greatest weakness lies in giving up. The most certain way to succeed is always to try his one more time " (Udhaifu wetu mkubwa upo katika kukata tamaa; njia ya uhakika kufikia mafanikio ni kujaribu mara nyingine: Tafsiri isiyo rasmi)
Kumbuka jambo hili, Haukuanza ili uishie njiani! Ndio, narudia tena haukuanza ili uishie njiani hivyo chagua kuendelea mbele. Mwenye hekima mmoja amewahi kusema, unapochoka usiache (usikate tama); jifunze kupumzika (ili upate nguvu ya kuendelea). Don't stop because you're tired, stop when it's done!
There's a place for you at the top

0 comments :

Mheshimu Rais Wako

2:20:00 PM Unknown 0 Comments

MHESHIMU RAIS WAKO
(Ni kwa Heshima ya aliyemweka katika kiti hicho)
Ukiwa mtawala au mmiliki wa biashara unaweza kumweka yeyote asimamie biashara hiyo kwa niaba yako, asimame kama mwakilishi wako. Mwakilishi huyu bila shaka atakuwa na amri (authority and power) kwa wale utakao waweka chini yake ili awaongoze na kuwasimamia vema. Mwakilishi huyu akidharauliwa bila shaka wewe uliyemweka umedharauliwa pia. Serikali  haziwekwi na wapiga kura, zinawekwa na Mungu. Maeneo mengi tumeshuhudia wenye kura nyingi wakikosa Urais. Wanademokrasia wenye imani wanaelewa hili.
Tunapaswa kuwaheshimu viongozi si kwa sababu ni wema au ni wabaya bali, ni kwa heshima ya yule aliyewaweka watuongoze yaani, Mungu Baba. Ameandika Mchungaji Kenneth Copeland, “Hakukuwa na Serikali korofi kama ile ya wakati wa Yesu Kristo, lakini bado Yesu alitaka iheshimiwe na akasema, ‘yaliyo ya Kaisari apewe Kaisari.’” Kwa maneno mengine Kristo aliwataka watu walipe kodi kwenye Serikali ambayo kimsingi ilikuwa inawakandamiza, hata wao hawakuamini kama Yesu amesema waheshimiwe kama Serikali. Serikali yaweza kuwa dhalimu lakini Mungu aliyeiweka kwa majira husika si dhalimu, na anamakusudi nayo.
Muda mzuri wa kuiheshimu Serikali ni pale inapofanya vibaya, maana ikifanya vema hata wapagani huiheshimu (Luka 6:28). Muda mzuri wa kubariki ni pale watu watakapo kulaani. Katika agano la kale Serikali ya Farao yule wa wakati wa Musa ilikuwa korofi na yenye kiburi hata mbele za Mungu, lakini Mungu alisema ni yeye aliyeiweka kwa makusudi yake. Kuna kusudi kwa serikali yako. Serikali haijiweki madarakani inawekwa. Katika Warumi 9:17 neno nimekusimamisha linaweza kuwa na maana, nimekuweka. Kwa maana maandiko yasema juu ya Farao, ya kwamba, Nilikusimamisha kwa kusudi hili, ili nionyeshe nguvu zangu kwako, jina langu likatangazwe katika nchi yote.Warumi 9:17
Tunamuheshimu mkuu wa nchi  kwa sababu tunayo hofu ya Mungu aliyemweka. Si kila Mtawala (Boss) anastahili heshima kutokana na tabia yake, wengine wanatabia mbaya. Pamoja na hayo kila Mkristo anapaswa kutoa heshima kwa kila mtawala bila kujali tabia yake.
Angalizo:
Katika kumtii kiongozi lazima tuhakikishe hatumkosei Mungu, kiongozi asigeuke sanamu moyoni mwetu. Sauti ya kiongozi ikiwa kinyume na injili ya Kristo na ipuuzwe. Mijadala mambo ya mapenzi ya jinsia moja, mauji ya holela, utoaji wa mimba unaohalalishwa kisheria, ndoa za mitala ni mambo ambayo ni kinyume na injili. Yapuuzwe hata kama msemaji atakuwa ni mkuu wa Nchi.
Mungu anaweza kubadilisha moyo wa kiongozi ikiwa watu watasimama kuomba. Maombi kwa Mungu mwenye nguvu yanaweza kuelekeza nchi wapi ielekee ikiwa mwombaji ataomba kwa bidii. Mungu anaendesha mioyo ya watawala kupitia maombi ya watakatifu.
Endelea kuombea nchi yako….., Shallom Israel, Shallom Tanzania….


0 comments :

Uzuri unadanganya

10:08:00 AM Unknown 0 Comments

UZURI  UNADANGANYA.
(Beauty is fleeting)
Nimewahi kupewa ushauri kutoka kwa watu mbalimbali kuhusu masuala ya mahusiano na ndoa. Nimejitahidi pia kusoma walau vitabu kadhaa. Yote kwa yote kuhusu ndoa na mahusiano sitasahau ushauri huu, “uzuri/urembo unadanganya.” Kwa nini unadanganya? Kwa sababu si wa kudumu, na si kitu utakachokihitaji kila siku.
Si vema kumpuuza mtu mwenye hekima anapofumbua kinywa chake kusema kitu. Solomon mtu mwenye hekima sana ndiye aliyesema katika Mithali 31:30, “uzuri si wa kudumu” Yaani sura, mpangilio wa meno, rangi na umbo zuri havisemi kweli maana baada ya muda mtu huzeeka na ngozi hukunjamana, na mara urembo wote hutoweka. Maana yake uonavyo leo sivyo itakavyokuwa milele. Kwa lugha nyingi si mambo utakayoyahitaji baadaye. Baada ya muda kupita utagundua haukuhitaji sura bali ulihitaji, upendo, ushirika, amani na uaminifu. Kwa nyakati tofauti wachungaji na wenye hekima wameonya kwamba,kufanya uamuzi kwa kujali mwonekano wa nje ni hatari.
Amesema mwenye hekima huyu, “Mwanamke aliye na umbo zuri na sura nzuri pasina maarifa kichwani afaa kwa usiku mmoja, lakini yule mwenye ufahamu na maarifa afaa kwa maisha yote.” Ndoa ni agano la maisha si la usiku mmoja. Mwonekano wa nje hautoshi kutoa taswira ya ndani ya utu, uchapakazi, uaminifu na upendo.
Urembo ukisimama peke yake hautoshi, utanashati peke yake hausaidii. Haipasi kuwa urembo na utanashati, badala yake inafaa kuwa urembo na akili, urembo na uchapakazi, urembo na ibada, urembo na upendo, urembo na uaminifu.
Ili urembo usikudanganye basi ni lazima uwe umeujua ukweli. Tafuta watu wanaoheshimika utagundua si kwa rangi zao wali si kwa urembo na utanishati wao bali ni kwa kujitoa sadaka, kuishi maisha ya heshima, uaminifu na utu wema.
Wewe si Mr. Tanzania unaanzaje kuoa Miss Tanzania? Urembo unadanganya. 
Tukutane kileleni………

0 comments :

Nyuma ya mafanikio ya kila mtu

2:45:00 PM Unknown 0 Comments

NYUMA YA MAFANIKIO YA KILA MTU
(THE SPIRIT BEHIND YOUR SUCCESS)
Ulimwengu usioonekana umekuwa ukitegemeza ulimwengu unao onekana. Ulimwengu wa roho unategemeza ulimwengu wa mwili, Ulimwengu wa roho unaamuru ‘dictate’ ulimwengu wa nyama. Tumezoea kusema nyuma ya mafanikio ya kila mwanaume  kuna mwanamke, hii si sahihi saana.
Ukweli ni kwamba nyuma ya kila mwanaume kuna roho, na si mwanaume tu bali ni nyuma ya kila mwanadamu kuna roho. Nyuma ya mafanikio ya Yusufu kulikuwa na Roho bora, Nyuma ya ustadi wa Daudi kulikuwa na Roho Mtakatifu.
Kila mwanadamu unayemwona, ni ama anapelekwa na Roho wa Bwana au roho wa shetani. Nyuma ya kazi yako kuna roho, nyuma ya Uhasibu wangu kuna roho pia. Kama alivyowahi kusema Mtumishi wa Mungu Nabii Makandiwa, “Hakuna dakika wala sekunde ambapo mwanadamu anaweza kwenda sehemu yoyote bila uongozi wa Roho wa Mungu au roho wa shetani”. Ni ama uko chini ya uongozi wa Roho wa Mungu au roho wa shetani. Warumi 8:14
Umewaona watu sokoni, kanisani, shuleni, au safarini? Ni ama wanaongozwa na Roho wa Mungu au roho ya shetani. Kila siku na kila saa chini ya uongozi wa Roho Mtakatifu, kinyume na hali hii ni uongozi wa Roho wa shetani.
Nyuma ya kila kiongozi kuna roho, matendo ya viongozi hudhihirisha roho wanazozitumikia, Namna pekee ya kujua roho/Roho unayemtumikia ni kwa kuchunguza matunda unayozaa. Matunda ya chuki, uasi, wizi, mgawanyiko, majanga, ukame, njaa, na vita hudhihirisha utawala fulani kiroho. Zamani Mungu alisema na watu wake kwa mvua, njaa, ukame na magonjwa, hata sasa mambo haya huzungumza kitu kutoka ulimwengu wa Roho.
Zingatia haya;
  1. Nyuma ya mafaniko ya kila mwanadamu kuna roho.
  2. Ulimwengu wa roho unatawala ulimwengu tunaoishi na kutembea ndani yake.
  3. Mwanadamu hawezi kuishi bila nguvu ya rohoni.
Tukutane ijumaa, shalom.

0 comments :

USHINDI UPO NDANI YAKO, SIO NJE

9:30:00 AM Unknown 0 Comments


 

USHINDI UPO NDANI YAKO, SIO NJE!

Nimewahi kumsikia mtu akisema kwamba, Ikiwa watu elfu watasema unaweza lakini wewe ukajiambia nafsini mwako na kuamini kuwa hauwezi, kufanikisha jambo fulani au kufanikiwa katika eneo fulani la kimaisha; uwezekano wa wewe kuja kufanikiwa katika eneo hilo ni mdogo sana sawa na hakuna. Na ikiwa watu elfu watasema hauwezi lakini wewe ukasema nafsini mwako na kuamini kuwa utafanikiwa, basi mafanikio huwa dhahiri baada ya muda tu.
Ni ukweli usiopingika kwamba, ikiwa mtu ataona ushindi ndani yake ni rahisi kuona ushindi katika maisha ya kila siku; na ikiwa mtu hataona ushindi ndani yake basi uwezekano wa kuona ushindi nje ni nadra sana sawa na hakuna. Na hapa ndipo panapo tofautisha kati ya mshindi na mshindwa, aliyefanikiwa na aliyeshindwa, anayesonga mbele na anayekwama.
“Maana aonavyo nafsini mwake, ndivyo alivyo” Mithali 23:7
Jambo kuu tunalotaka upate hapa ni kwamba, kama kuna mahali au eneo unataka kuona ushindi katika maisha yako basi utambue kuwa ushindi upo ndani yako sio nje, yaani ushindi huanzia ndani yako. Hauwezi kushinda nje kama haujaweza kushinda ndani yako kwanza. Kumbe hatuwezi kuona badiliko lolote la kudumu kiuchumi au kifedha au kihuduma endapo ndani yetu hatuoni wala kuamini kama tunaweza kufanikiwa na kupata badiliko hilo. You must feel and see it before you realize it.
Njia kuu moja wapo ya kukuwezesha kuona ushindi ndani yako katika eneo fulani la kimaisha ili kuupata ushindi huo nje ni kusikia, kile unacho ruhusu [kusikika] ndani yako ndicho hupata nafasi katika maisha yako. Sauti [maneno] unayoisikiliza au uliyoipa ruhusa ndani yako ndio huamua hatima yako. Hauwezi kujidhihirisha kama samba endapo ndani unajiona kama swala. Ukiona ushindi utaongea kama mshindi, utatembea kama mshindi; ukiona kushindwa hauwezi kuwa na ujasiri na kuongea kama mshindi.
Unapoona ushindi ndani yako, na ukakutana na changamoto akili hupata nguvu ya ziada na kuanza kutafuta namna ya kuondoa au kutumia changamoto hiyo ili kufikia ushindi, lakini kama ndani huoni ushindi, umekata tama akili ‘inaparararizi’ na inakosa nguvu ya kufikiri namna ya kuondoa au kutumia changamoto, hata changamoto ndogo akili huona mlima mkubwa. Na hapa ndipo panapo tofautisha katika ya mshindi na mshindwa, aliyefanikiwa na aliyeshindwa, anayesonga mbele na anayekwama. Ndani ya moyo wako unaona nini? Unachoona ni muhimu sana, kwa sababu kinaweza kukukwamisha au kukufanikisha.
There’s a place for you at the top

0 comments :

Ubongo hauna rangi

7:37:00 PM Unknown 0 Comments

  
UBONGO HAUNA RANGI
(Brain has no colour)
Hakuna utofauti wa akili kati ya bara moja na lingine, hakuna utofauti katika kuumbwa kwa Mzungu na Mwafrika, sote tu sura na mfano wa Mungu. Hakuna tofauti kati ya watu wa magharibi na watu wa kusini. Kila mtu anaweza kuwa atakavyo, na anaweza mambo yote. Kila mwasisi wa Taifa ana nafasi ya kulifanya taifa lake kuwa nambari moja kwa maendeleo.
Ulipopewa rangi nyeusi ya mwili si kwamba umepewa ubongo mweusi. Ubongo hauna rangi, mtu mweusi hana ubongo mweusi, wala mtu mweupe hana ubongo mweupe, ubongo ni ubongo tu. Ukikuta ubongo mweusi basi ni wewe mwenyewe umeupaka rangi nyeusi. Wakati Wright Brothers wanavumbua urushaji wa ndege wengine wanarogana. Wakati mmoja anaun’garisha ubongo wake kwa kusoma kitabu kizuri mwingine anatazama picha za ngono na hivyo anauchafua zaidi. Sote tumefanya hayo lakini leo makala hii ni simu ya kukuamsha, Brain has no colour!
Ben Carson, Usain Bolt, Hayati Dr Myles Munroe ni miongoni mwa wachache walioihakikishia dunia kwamba, wana ngozi nyeusi lakini hawana ubongo mweusi. Hofu, mashaka, kutokujiamini, uchoyo, ubinafsi, uchafu, uchawi, ulevi, ulafi, uasherati na vingine vingi huchafua ubongo na kufanya uwe na rangi nyeusi. Ili uhakikishe hili, chunguza na utagundua jamii nyingi zenye mambo ya kishirikina ziko nyuma kielimu, na familia za kuhusudu ulevi huwa hazisongi mbele.
Kwa asili mwanadamu anazaliwa akiwa na ubongo wenye kumpa akili ya kutenda mambo yote, kuweza kila kitu kwa wakati. Yale yasiyofaa ambayo mwanadamu huona na kusikia huendelea kumharibu na kufanya awe na hofu, kujidharau, kujiwekea mipaka ya kiutendaji. Wafilipi 4:13
Usimfundishe mwanao kuwatukuza wazungu, bali mwambie ana ubongo sawa na wao na anaweza kufanya zaidi ya wao. Darasa moja, mwalimu mmoja na shule moja lakini matokeo ya watoto huwa tofauti kwa sababu ya vizuizi tunavyowawekea. Mwingine anaambiwa anga ndio kuzuizi chake mwingine anaambiwa ajira, ukiajiriwa tu inatosha mwanangu! Huna wa kuajiriwa hawezi jihusisha na tafiti za kurusha vyombo kwenda mwezini au kupasua vichwa vya watu, hii ni kwa sababu upatikanaji wa ajira ni rahisi na hivyo kufikiri kwenda mwezini au kuwa daktari bingwa ni kama kupoteza muda.
Tatizo lolote ikiwamo la ajira, kabla halijawa la Serikali ni la wazazi wa mtoto, baadaye ni la mtoto mwenyewe, na mwisho ni la nchi. Ubongo wetu unapakwa matope na mafuta machafu ya mawazo mgando ndio maana tunashindwa kufikiri kimkakati.
 Tunashindwa kupenya katika majadiliano yenye maslahi makubwa. Mawazo mabaya si kuzini na kuua watu tu, bali ni uoga. Tunaogopa kuanza, tunaogopa kugombea, tunaogopa kuamka mapema, tunaogopa kusafiri, tunaogopa kukopa, tunaogopa kuacha kazi, tunaogopa kusimamia mawazo yetu, tunaogopa kweda nchi za mbali. Ukienda uwanja wa Ndege utaona wanaoingia kwetu ni wengi kuliko wanaotoka, sisi tunaogopa wao wanakuja. Hawajui lugha yetu, wala hawajui asili yetu ila wanakuja kisha wanafanikiwa na wanaondoka. Jifunze kwa wachina waliojazana Kariakoo Dar es salaam.
Ubongo hauchakai kwa sababu unautumia sana, bali unachakaa kwa sababu hautumii akili. Ni kweli hukupata muda wa kwenda shule sawa, Je, hujapata hata muda wa kufikiri? Tofauti kati ya msomi na mtu ambaye hakusoma ipo kwenye kufikiri. Ukiweza kufikiri vizuri na kupanga kimkakati basi wewe ni msomi. Ni vijana wachache ambao hufikiri kimkakati yaani akapanda au akawekeza katika mradi utakao mlipa baada ya miaka hamsini.
Azimio la Arusha lilikuwa tunda la akili ya mwalimu Nyerere, Tuzo ya Nobel ni mtoto wa akili ya Mzee Alfered Nobel aliyesikia sifa zake mbaya na kubadilika. Afrika kusini huru ni mtoto wa akili wa Hayati Nelson Mandela, Microsoft Cooperation ni mtoto wa Bill Gate, TANU si ni mtoto wa Mwalimu Nyerere.
Je, akili yako imetuzalia nini cha maana? What is your brain child?
Wanaotumia akili zao vizuri hubuni, huanzisha na huvumbua. Huasisi mataifa, huanzisha viwanda na makampuni, huanzisha taasisi zao. Hawafi wakiwa wamelala kitandani, hufa wakiwa katika mapambano ya kukamilisha azma na wito wao.

0 comments :

UNATAKA KUFANIKIWA KATIKA NINI?- IV

10:10:00 PM Unknown 0 Comments

UNATAKA KUFANIKIWA KATIKA NINI?-IV
(Amua kuthubutu)
Mtu mmoja amewahi kusema, “Maisha hayatupi tunachokitaka, bali hutupa kile ambacho tupo tayari kukifanyia kazi”. Kile ambacho unatamani kitokee katika maisha yako au katika eneo lolote la maisha yako ni lazima uwe tayari kufanyia kazi ili kiwe halisi. Nioneshe mtu mwenye udhubutu katika yale anayoyatamani, nikuoneshe mtu mwenye matokeo katika maisha yake.
Kuhamasika (motivated) pekee katika jambo fulani hakutaleta matokeo katika maisha kama hakuna udhubutu wa kufanyia kazi jambo hilo. Wako wengi waliopita semina au kusikia mafanikio ya watu wengine, na wakahamasika kweli kufikia malengo waliyojiwekea lakini baada ya muda hakuna wanachoweza kuonesha kama matokeo ya kuhamasika kwao. Na hii ni kwa sababu walihamasika lakini hawakuchukua hatua ya kufanyia kazi matamanio yao.
Mwenyehekima mmoja amewahi kusema, baada ya mwaka kupita au mwezi au muda fulani, tutabaki tukijilaumu na kutamani kama tungedhubutu kuyafanya yale tuliyoyahairisha. Do it today or regret tomorrow. Kumbuka: hakuna jambo lolote lenye thamani ambalo huja kirahisi, ni matokeo ya kazi (nothing worth comes easy, it takes work).
Mtu mvivu husema,Simba yuko nje; nitauawa katika njia kuu” Mithali 22: 13
Adui mkubwa katika eneo la udhubutu ni visingizio; unaweza kuwa katika kundi la watu wanaoeleza kwa nini hawakuweza kufikia malengo yao, au ukawa katika kundi la wachache wanaoleza namna gani wameweza kufikia mafanikio yao katikati ya changamoto nyingi. Kumbuka, ulimwengu hautoi heshima kwa wanaoeleza kwanini haiwezekani, au kwanini hawakuweza au wanaoeleza namna ambavyo watu waliwakatisha tama walipotaka kuanza. Usijipe majibu ya kushindwa au kwamba haiwezekani kabla haujadhubutu. “Maisha hayatupi tunachokitaka, bali hutupa kile ambacho tupo tayari kukifanyia kazi”.

There’s a place for you at the top

0 comments :

Changamoto kwa viongozi vijana

2:09:00 PM Unknown 0 Comments

 
CHANGAMOTO KWA VIONGOZI VIJANA
(Usimzuie mtu kufanya mabaya, ana uhuru)
Changamoto kubwa inayowasonga viongozi vijana ni kumilikiwa. Kuna hatari ya viongozi vijana kumilikiwa au kuongoza kwa akili za walioko nje ya ulingo. Kuna umuhimu wa viongozi vijana kuonesha umakini mkubwa na kipekee.
Ili kummiliki kiongozi kijana watu hutumia vitisho nini kitampata au nini hakitampata. Mara nyingi wenye roho hii (spirit of manipulation) husema, fanya hivi ili upendwe na watu au usifanye hivi watu watachukia. Watu wenye roho hii hutoa hakikisho feki, humwakikishia mtu usalama ambao kimsingi ni Mungu peke yake atupaye kukaa salama katika kazi, biashara na vyeo. Katika amani nitajilaza na kupata usingizi mara, Maana Wewe, Bwana, peke yako, Ndiwe unijaliaye kukaa salama.” Zaburi 4:8
Yesu alijua Petro anaroho hii ambayo hutoka kwa shetani. Petro alimwita Yesu Kristo pembeni akimwonya kwamba, mateso hayatampata. Mara nyingi wenye roho hii hupenda kumbana mtu pembeni, humwita kipekee bila ya watu, hutoa onyo hilo kwa siri.
Ingawa Yesu Kristo alikuwa kiongozi kijana hakusita kumkemea Petro kwamba, “rudi nyuma yangu shetani”. Nakusihi kijana usiruhusu kumilikiwa kinyume na kusudi la kuumbwa kwako, usizuiwe kutekeleza yale ambayo Mungu amekuitia kutekeleza. Mathayo 16:23
Nakumbuka nikiwa kiongozi kijana mtu mmoja aliniita akinikemea na kunieleza fanya hivi au vile, na mara moja nikawa mkali nikamwambia, “Mimi ni mtu wa kanuni, sipangiwi nifanye lipi na lipi nisifanye bali napanga mwenyewe.”
Yes, I am a man of Principle! Nilijibu hivyo waziwazi kwa sababu nilijua ubaya wa roho hii ya kumiliki watu, nilikuwa nimeitafakari usiku wa kabla ya tukio. Mtu anaruhusa ya kuchagua hata mabaya, uhuru wa kuchagua (freedom of choice) ni muhimu kwa kila jamii ya kistaarabu. “Because to take away a man’s freedom of choice, even his freedom to make the wrong choice, is to manipulate him as though he were a puppet and not a person” Madeleine L’Engle
Imani hufanya watu wamilikiwe lakini maarifa huwaweka huru. Hakuna anayeruhusiwa kumiliki utashi na dhamira ya mwanadamu. Hata viongozi wa dini hawaruhusiwi. Mwanadamu ni kiumbe huru, na anapaswa kuamua apendacho.
Endelea kutembea katika uhuru wako, Mungu alimtuma mwenaye kukuokoa na shetani ili uwe huru wala si ili uwe milki ya viongozi wa dini, siasa au serikali.  Kumiliki watu ndio uchawi wa kisasa ambapo mtu hafanyi kitu bila ya kupiga simu au kuomba kibali kwa wanadamu.
Amesema Joyce Meyer, Ukiwa na shida nenda kwenye kiti cha enzi cha Mungu, usikimbilie kupiga simu. (Go to throne not to the telephone) Mtegemee Mungu na yeye atakuwa ngome yako, ngao yako, na kigao wala hautaondoshwa. 
Barikiwa.

0 comments :

Rafiki Mpya, Mambo Mapya

11:29:00 AM Unknown 0 Comments

  
RAFIKI MPYA, MAMBO MAPYA
(Angalia ingizo la rafiki mpya)
Imenenwa katika Mithali 28:24: “Aibaye mali ya babaye au mamaye, na kusema, Si kosa; Mwana huyo ni rafiki wa mtu mharibifu.”  Ziko tabia au mambo ambayo yanapotokea kwako au kwa rafiki yako yanataka kukuonesha kwamba umejiunga na rafiki mwovu au kikundi kibaya.

Mtoto akipata rafiki wabaya atamwibia babaye, kadhalika mtumishi akipata marafiki wabaya ataiba mali ya ofisi (mali ya BOSS). Kuchukua kitu cha nyumbani kwenu bila ridhaa ya wazazi ni wizi, kuchukua mali ya ofisi bila utaratibu si haki. Ukiona mtu anamkono mrefu, anaiba mali za kwao au ya kampuni inayomlipa mshahara ujue amepata marafiki wabaya.
Ukiona mtazamo wako juu ya amri za Mungu unabadilika (huoni yaliyokatazwa) basi jiulize ni nani ameingia katika maisha yako. Ukiona mtazamo wako juu ya mume/mke wa mtu unabadilika basi jiulize ni nani unashinda naye kila siku.  Rafiki mpya huleta tabia mpya, nzuri au mbaya.
Kuna watu wanasema kuiibia serikali si dhambi, hawa ni rafiki ya watu waovu, kuna wanaosema mume/mke ni wa kwako akiwa ndani tu, hawa nao ni rafiki ya waasherati. Biblia inakataa kitendo cha kuiba na kusema ni kosa, yuko mwizi anayejua wizi ni kosa na yuko mwizi aliyehalalisha wizi na haumii tena kwa sababu kitendo hicho kwake si dhambi.
Marafiki wabaya hufanya hata dhambi ionekane kama si kosa, humbadilisha mtu akili ili autazame uovu kama wema. Biblia inasema, “aibaye na kusema, si kosa, ni rafiki ya mtu mharibifu.” Mharibifu wa nini? Mharibifu wa akili. Mithali 28:24
Yuko pia aziniye na kusema si kosa, yuko atoaye rushwa na kusema si kosa, yuko atorokaye shuleni na kusema si kosa, yuko pia adanganyaye na kusema si kosa!
Wazazi wengi wamekataa watoto wao wasihusiane na vijana waharibifu. Wanaharibu akili, wanageuza moyo, na hivyo mtu huangamia bila kujua. Katika kuwapima marafiki tujifunze kwa Yesu: Hawa ni wanafunzi watatu marafiki wa Yesu; Petro mtu wa imani ndiyo yule Kefa, mwanafunzi msemaje aliyesema kuwa, Yesu ni Kristo, Yohana alikuwa mtu wa upendo sana ndiyo yule aliyelala kifuani pa Yesu, na Yokobo mtu mwenye tumaini saana ndiye yule alitufundisha dini njema ya kuona wagonjwa na kulisha masikini. Kwa kuzungukwa na hawa watatu Yesu alichagua kuwa salama ki akili. Alizungukwa na mwenye upendo, imani na tumaini.
Wewe pia ni wastani wa watu wako watano wa karibu, Angalia tabia zako mpya, ujue mchango na uwekezaji wa kitabia ulifanywa na rafiki zako katika maisha yako. Ikiwa haiwezekani kuwashauri kubadilika achana nao, Cut off the link! Usitoe muda wako kwa marafiki wabaya, Mungu akupe neema ya kuachana nao na kujitenga.
Tukutane juu pamoja na watu wako watano wa karibu sana.

0 comments :

Unatatua changamoto gani?

9:19:00 PM Unknown 0 Comments

 
UNATATUA CHANGAMOTO GANI?
Ili kuishi maisha yenye hamasa, swali muhimu unalotakiwa kujiuliza sio unataka kufanya nini katika maisha yako ya kuwa hapa duniani bali unatakiwa kujiuliza ni changamoto gani au tatizo gani unataka kulitatua katika kuishi kwako? Moja ya sifa kuu ya kufanana kwa watu wote waliofanikiwa ni utatuzi wa changamoto; nioneshe mtu aliyefanikiwa nikuoneshe changamoto anayotatua au aliyotatua katika kuishi kwake. Katika ulimwengu huu, usitafute jambo la kufanya; tafuta changamoto ya kutatua.
Kila aliyezaliwa na mwanadamu amebeba jawabu la changamoto fulani; kwa sababu mafanikio ya kweli yamebebwa katika kuleta majibu juu ya changamoto au upungufu uliopo mahali fulani. Watu hawatakufuata wala kukulipa kwa sababu una kipawa au ujuzi au uwezo fulani ndani yako, watu watakufuata na kuwa tayari kukulipa kwa sababu kipawa chako, ujuzi wako na uwezo wako unatatua changamoto walionayo. Thamani yako mbele ya watu inategemea kiwango chako cha utatuzi wa changamoto walizonazo watu hao.
Boresha uwezo wako wa kutatua changamoto.
Kila mara ni muhimu kuboresha uwezo wako wa kutatua changamoto, ndio maana hata watengenezaji wa simu kila mara huboresha simu wanazotengeneza kwa kuziongezea uwezo wa kutatua changamoto mbali mbali. Ndio maana utasikia iPhone 5 mara iPhone 6 mara “iPhone 6 plus”. Wanachofanya hapa si kutengeneza simu nyingine bali ni kuboresha simu iliyotengezwa hapo awali. Na kwa sababu hiyo thamani ya iPhone 6 plus ni kubwa kuliko thamani ya iPhone 6 ya kawaida. Na watu wako tayari kulipa zaidi kwa iPhone 6 plus kuliko iPhone 6 ya kawaida kwa sababu “iPhone 6 plus” imeboreshwa uwezo wake wa kutatua changamoto ya mawasiliano. 
Kuna namna nyingi za kuboresha uwezo wako wa kutatua changamoto katika eneo lako la huduma, biashara, tekinolojia, uongozi, elimu ulipata, uandishi, ofisini, kipawa, michezo (athletes); baadhi ni kwa kutafuta ujuzi zaidi, ‘kupractice’ zaidi, kujifunza kwa waliokutangulia, kujifunza kwa waliofanikiwa, kusoma vitabu vinavyohusiana na eneo umalotaka kulifanyia kazi n.k. Wazo kuu hapa ni kujitahidi kuwa bora zaidi ya jana, tafuta kuwa bora (excellent) katika kila ulichoweka nia ya kukifanya.
There’s a place for you at the top

0 comments :

Ndio maana haukuweza

11:45:00 AM Unknown 0 Comments

 
NDIO MAANA HAUKUWEZA
Zingatia Uhalisia Gal 6:7
Imewatokea wengi kushindwa kufikia malengo, ni jambo la kawaida kwa wengi kushindwa kupungua uzito, si ajabu kwa wanafunzi kufeli mtihani. Kila unaposhindwa jitahidi kurudi kwenye misingi. Wakristo wengi wameanguka katika dhambi na kwao ni muhimu kurejea katika misingi.
Mambo hayatokei yenyewe tu, na kama wakristo tunahitaji miujiza na si maajabu. We need miracles not magic! Maajabu yako hata kwa waganga wa kienyeji, maajabu ni kupata pesa bila kufanya kazi, kufaulu bila kusoma, kahaba kuolewa au asiyehaki kuinuliwa. Ni ajabu kwa anayekula kupita kiasi kupungua uzito.
Miujiza ni tofauti na maajabu. Miujiza inakutaka ushirikiane na Mungu, miujiza inatualika tuungane na Mungu. Miujiza ni mchanganyiko wa sala na kazi, pia miujiza ni mchanganyiko wa imani na matendo. Miujiza hutokea pale watu wanapoamua itokee. Amesema Joel Osteen “Ni imani yetu ndiyo huamsha nguvu ya Mungu”.
Ili muujiza utokee lazima pawepo na imani, sala, mafungo, bidii ya kazi upendo na amani. Upendo unachagiza sana uwepo wa muujiza. Ofisi ambayo upendo umetawala watu watamaliza kazi kwa wakati (finishing before deadline). Maajabu hutokea tu bila sababu, lakini miujiza inahitaji muda, uwekezaji, bidii na upendo. Mungu wetu ni mtenda miujiza (miracles) si maajabu (magic). Kama hauna muda na mpenzi wako usitarajie muujiza wa amani na upendo bali tarajia maajabu ya amani na upendo. Galatia 6:7
Maajabu yanafanya muuzaji mwenye lugha mbaya apate wateja, muujiza hutokea pale muuzaji mwenye busara na kauli nzuri anapopata wateja wengi na kuuza sana sana. Waganga wa kienyeji (chief magic promiser) hawakufundishi huduma nzuri kwa wateja bali wanawahadaa wateja na kufanya upate usichostahili. Usiende kwao, wala kwa wasoma nyota. Wagalatia 6:7
Hata biblia imekataa, kuvuna usipopanda, kupewa usichoomba, kupata usichostahili. Wengi tunao ujuzi wa kutufikisha kileleni, lakini hatuna maarifa ya kutufanya tudumu hapo. Haifai kupenda kuona maajabu. Maajabu hayawezi kudumu maana hata hatujui kwa nini hutokea. Lakini muujiza wa Yesu ukitokea na sisi tunajua tukitimiza yanayotakiwa utatokea tena. Siku moja mpwa wangu alimuona Pastor Chris akiwapuliza watu wanaanguka baadaye na yeye akafanya na akapata matokeo yale yale. Siku za mbeleni nami pia katika kuombea watu nikafanya nikapata matokeo yale yale.
Ushindi ni tabia, mafanikio ni tabia pia. Soma biblia na tazama tabia za waliotendewa miujiza utakuta zinafanana. Si rahisi kuushinda ulimwengu kama bado haujajishinda mwenyewe, si rahisi kuaminiwa na watu ikiwa bado haujimini wewe mwenyewe. Madhara ya kutokujiamini ni sawa sawa na kutokumwamini Mungu.
Batromayo kipofu alihakikisha anapaza sauti na Yesu akamsikia licha ya kelele za umati mkubwa, Zakayo alipanda juu ya mti ili amwone Yesu, mama aliyetokwa na damu alipenya katika ya kundi la watu maana haikuwa rahisi kumgusa Yesu. Muujiza unataka ujipange, uwe juu ya viwango vya watu, muujiza utataka upige kelele mpaka Yesu asikie, muujiza unataka upenye katikati ya watu katika usaili.
Mara ya kwanza ulipoimba vizuri Mungu alitaka ujue kipaji chako, pale ulipohubiri vizuri Mungu alitaka ujue wito wako, pale ulipotengeneza bidhaa nzuri Mungu alitaka ujue kazi yako lakini utambulisho huo haukusaidii kama hautendi hivyo mara kwa mara. Kwa mshindi kushinda ni mazoea, kipaji chako kikiwa tabia yako hapo utadumu. 
Wiki hii ikawe mwanzo wa miujiza katika maisha yako katika jina la Yesu Kristo. Amen

0 comments :

Mungu ni mwakilishi wetu

11:58:00 AM Unknown 0 Comments

 
MUNGU NI MWAKILISHI WETU.
(Anajua kupigana vizuri kuliko sisi)
Tunaishi kwenye ulimwengu wenye changamoto nyingi, watu wanafukuzwa kazi, yatima wanadhulumiwa; wanafunzi wanafeli, wazazi wanagombana, wapenzi wanaachana na vikao vya kazi havimaliziki kwa usalama.
Yote haya yanamfanya mwanadamu ajitahidi kuyakabili bila ya Mungu. Kuna kitu kinamwambia mwanadamu apigane mwenyewe, kuna msukumo usiotaka kumruhusu Mungu apigane.
Kwa nini tunashindwa kumruhusu Mungu aingilie kati? Ni kwa sababu tunadhani tunajua kupigana kuliko Yeye au ni kwa sababu tunafikiri atasahau. Ukweli ni kwamba Mungu anajibu kwa wakati, yuko makini kuliko wahudumu wa chumba cha watu mahututi.
Siku moja usiku baada ya kuona nyumba yangu imezingirwa na mambo yasiyofaa niliamua kumwita BWANA YESU na dakika ile ile shwari ilirejea. Namshangaa Mungu kwa maana amewapa mamlaka kuu wale wanaompigania. Hudson Taylor akijua fika atakwenda nchi ya mbali kwa uinjilishaji, alijifunza kumtegemea Mungu kwa kila jambo. Hata alipotaka pesa hakumwambia mkuu wake wa kazi bali alimwambia Mungu katika maombi. Ananukuliwa, “ni vema nijifunze kumwomba Mungu kwa kila jambo, maana huko China niendeko hakuna mtu wa kumwomba wala kumtegemea”.
Katika biblia tunaona Mungu amekuwa sauti ya wasio na sauti, amewakumbuka matabaka ya walioonewa. Yeye ni Mungu wa vita, anajua kupigana tena ameshinda vita zote. Kuomba ni kumchagua Mungu awe mwakilishi wako katika vita. Ndio maana biblia imeyaita maombi silaha. Waefeso 6:11
Uwezo wa mwanadamu unakikomo, hata akijitahidi hawezi kutuliza yote yanayomsonga. Taarifa ya habari si taarifa yenye habari za kutia tumaini bali ni taarifa yenye habari mbaya; mafuriko, njaa, migomo, ugomvi, kupunguzwa kazini, vifo na magonjwa.
Nakumbuka siku moja nilipopokea taarifa ya kutisha kwamba mpendwa wangu yuko mbioni kufa. Niliogopa sana! Moyo wangu ulizimia kwa hofu. Siku yangu ilikwenda mrama kabisa. Mara ghafla jioni rafiki yangu akanishauri na kutumia Zaburi 46:1-3. Na hapo nikapata nguvu, na hapo nikapata upenyo na hapo nikasimama tena. Na hapa nikajua kama ni vita si mimi nitakaye kufa, bali ni wenzangu ndio watafia nchi zao na falme zao.
“Mungu kwetu sisi ni kimbilio na nguvu, Msaada utakaoonekana tele wakati wa mateso.
Kwa hiyo hatutaogopa ijapobadilika nchi, Ijapotetemeka milima moyoni mwa bahari.
Maji yake yajapovuma na kuumuka, Ijapopepesuka milima kwa kiburi chake.” Zaburi 46:1-3
Nikamkimbilia Mungu kwa sala, tukashinda vita na mpendwa wangu akawa salama! Tishio la kifo, ajali, hukumu ya Mahakama, Waganga, Wachawi halina uwezo wowote kwa yule ajuaye kuliitia jina la BWANA, yule aliyepaka damu ya Yesu ya Pasaka.
Kujiambatanisha na Mungu ni kujiambatanisha na ushindi. Kama wakristo sisi ni washindi, maana tu uzao wa ushindi.
Mkimbilie Mungu ukiwa na cheti cha daktari, mwambie utaishi kwa neno lake wala si kwa chakula, wala si kwa neno la daktari. Ingawa tunaheshimu mchango wa kila taaluma lakini Bwana ndiye atakaya maneno yote, kwa kuwa Yeye ni mwanzo tena mwisho. Hata kama umetenda dhambi usisite kumwendea Mungu wakati wa changamoto yako. Yeye ni kimbilio wakati wa shida, shida zinaturejesha kwake.

0 comments :

Ili kufikia malengo yako

2:10:00 PM Unknown 0 Comments

 
ILI KUFIKIA MALENGO YAKO
Kila mwaka mpya unapoanza watu wengi huwa na kawaida ya kujiwekea malengo katika mwaka husika. Karibu kila mtu au mahali huzungumia mipango au malengo anayotamani na kujipangia; Lengo ni kupata taswira ya mahali ambapo mtu anataka kwenda au kufanikisha katika mwaka huo. Hili ni jambo zuri kwa kuwa linaleta hamasa, nguvu na matumaini ya kusonga mbele katika maisha ya kila siku; kwa kuwa kama mtu hajui anapotaka kwenda (hana malengo au mipango) njia yoyote itamfikisha.
Changamoto moja ambayo hutokea ni kwamba watu wengi huwa na hamasa kubwa juu ya kuweka na kutamani kutimiza malengo yao mwanzoni mwa mwaka; lakini kadiri muda unavyozidi kwenda hamasa na nguvu ya kuyaendea malengo waliojiwekea hupungua au hutoweka kabisa. Na hivyo wanapofika mwisho wa mwaka wanagundua kuwa hawana kitu cha kuonesha au wanakitu kidogo tu ukilinganisha na malengo waliokuwa nayo wakati wanaanza mwaka.
Jambo hili tunaweza kuliona hata kwa wanaisraeli walipokuwa wanatolewa katika utumwa na kupelekwa katika nchi yao ya ahadi. Wakati wanatoka walikuwa na hamasa kubwa na nguvu na matumaini ya kufikia nchi ya ahadi; lakini kwa kadiri walivyokuwa wanaendelea na safari hamasa, matumaini na nguvu ya kufikia ahadi iliyokuwa mbele yao ilikuwa ikipungua kwa baadhi yao. Ukitizama safari yao utagundua kuwa kilichofanya hamasa na matumaini yao kupungua kadiri walivyosonga mbele, ni kitendo cha wao kuacha kuangalia (Paying attention) Ahadi na kuanza kuangalia changamoto walizokuwa wanakutana nazo njiani.
Je unapokutana changamoto katika mipango uliojiwekea katika mwaka huu, unachagua kuangalia nini? Unaangalia changamoto au unaangalia malengo yako? Ukitumia muda mwingi kutafakari changamoto uwe na uhakika hamasa na nguvu hupungua na hatimaye huweza kutoweka kabisa. Lakini ukitumia muda wako kutafakari malengo yako na kutafuta namna ya kufanikisha (Mfano; Kutafuta maarifa zaidi kwa kusoma vitabu au kurudi shule tena, kutenga muda mwingi zaidi wa kufanyia kazi jambo hilo, kutafuta ushauri, kujifunza kwa waliokutangulia/ waliofanikiwa, kurudia tena uliposhindwa mara ya kwanza n.k) uwe na uhakika mwisho wa mwaka au muda uliojiwekea  utakuwa na kitu cha kuonesha na sio maneno matupu ya kwanini ulishindwa.
Katika kufikia malengo au mipango uliojiwekea mwanzoni mwa mwaka au mwezi au kipindi chochote kile changamoto hutokea au naweza kusema haziepukiki kwa namna moja au nyingine. Changamoto ndizo zinatufanya tushangilie na kuwa na moyo wa shukrani pale ambapo tumefikia malengo hayo. Kumbuka jambo hili: Kama ni rahisi (hakuna changamoto) kila mtu angefanya. Changamoto haziji ili kufisha ahadi yako, bali zinakupa fursa ya kuona Ukuu na Utukufu wa Mungu kwa namna ambayo hujawahi kuona. Ni changamoto ya wanaisraeli ndio iliyofanya tutambue Mungu anaweza kufanya njia mahali pasipo na njia. Mtu hapewi tuzo kwa kusimulia namna changamoto zilivyomkwamisha; hupewa tuzo kwa kuonesha namna gani ameweza kufikia malengo yake katikati ya changamoto.
There’s a place for you at the top!

0 comments :

Kipaji chako ni hiki hapa

1:34:00 PM Unknown 0 Comments

 
KIPAJI CHAKO NI HIKI HAPA
(Katika taabu ni rahisi kujua kipaji chako halisi)
Nani ni nani Tanzania, Kuna watu wanafuatana na utambulisho wao, Mchango wao na karama zao zimewatambulisha. Who is who in Tanzania? Sheikh Shaaban Robert amejulikana kwa mashairi, Askofu Moses Kulola amejulikana kwa injili, Rose Mhando amejulikana kwa nyimbo za injili. Wewe unautambulisho gani?
What is your Identity? Tunaposhindwa kujua utambulisho wetu kupitia karama na makusudi ya kuumbwa kwetu tunapoteza maana ya kuishi. Na hapa siku tukiimba vizuri tutafikiri sisi ni waimbaji na siku tukifundisha vizuri tutafikiri sisi ni walimu. Tatizo hili limewasumbua wengi na limekuwa likijulikana kama, The Crisis of Identity, ni hali ya kutokujua utambulisho wetu na mchango wetu kwa jamii.
Ukitaka kukosa mshindi katika mchezo wa mpira wa miguu usimpige refa bali ondoa magoli na hivyo kutakuwa hakuna sehemu ya kufunga na tayari mpira utapoteza ladha. Kingine unachoweza kufanya ni kuweka nguzo nyingi za magoli (yaani badala ya mbili weka nne). Malengo mengi maishani ni usumbufu. Kuwa na malengo mengi hakukupi nafasi ya kuwa mshindi ndio maana kila timu hufunga katika goli moja tu. Maisha bila ya kuwa na lengo kuu la kufanikisha hayana ladha. Ndio maana ni muhimu kujua kusudi lako na kipaji chako. 
Kipaji halisi hujidhihirisha wakati wa taabu, wakati ambao uko peke yako bila ya ulio wazoea. Unachopenda kufanya gizani bila ya kuhimizwa na mtu kinaweza kuwa kipaji chako nuruni. Kipaji cha ubondia hugunduliwa nje ya ulingo na ulingoni ni sehemu ya udhihirisho tu.
Yusufu alitabiri Gerezani, Paulo na Sila waliimba na kumsifu Bwana wakiwa gerezani mpaka milango ya Gereza ikafunguka. Je! kipaji chako kinadhihirika wakati wa shida? Kipaji halisi hakinyamazishwi na mazingira magumu.
Kipaji au karama ya Mungu huonekana hata katika taabu, Yesu aliendelea kuhubiri, kuponya na kuokoa hata akiwa msalabani. Don’t be silenced by problems
Nimeona Mungu akiponya kwa uponyaji mkuu katika mazingira ambayo sikuwa hata na utayari. Siku chache zilizopita tumeshuhudia Boss mkubwa aliyeachishwa kazi TANESCO akiendelea na kuhubiri injili. Kawaida ya kipaji halisi ni nyenzo inayotumika hata katika taabu, kamwe hainyamazi. Umri haunyamazishi kipaji chako, ana miaka 82 ya kuzaliwa bado Jimmy Swaggart anaimba, kupiga kinanda vizuri na kufundisha.
Wako wakimbizi waliotumia vipaji vyao ugenini, wako watumwa waliotawala utumwani. Wako wafanyakazi wa ndani walioishia kuwa wafalme. Ni baada ya kugundua vipaji vyao na kuvitumia hata katika mazingira magumu. Endelea kutumia kipaji chako usikate tamaa.
Mazingira magumu yanapaswa kukuhamasisha kutumia kipaji chako na si kukitelekeza kipaji chako. Kwa tafsiri yangu Paulo alimaanisha hivi, “…chochea kipaji ulichopewa na Mungu kilicho ndani yako.” 2 Tim1:6
Kileleni ndipo tunapopatikana

0 comments :