Ili kufikia malengo yako
Kila mwaka mpya
unapoanza watu wengi huwa na kawaida ya kujiwekea malengo katika mwaka husika.
Karibu kila mtu au mahali huzungumia mipango au malengo anayotamani na
kujipangia; Lengo ni kupata taswira ya mahali ambapo mtu anataka kwenda au
kufanikisha katika mwaka huo. Hili ni jambo zuri kwa kuwa linaleta hamasa,
nguvu na matumaini ya kusonga mbele katika maisha ya kila siku; kwa kuwa kama
mtu hajui anapotaka kwenda (hana malengo au mipango) njia yoyote itamfikisha.
Changamoto moja
ambayo hutokea ni kwamba watu wengi huwa na hamasa kubwa juu ya kuweka na
kutamani kutimiza malengo yao mwanzoni mwa mwaka; lakini kadiri muda unavyozidi
kwenda hamasa na nguvu ya kuyaendea malengo waliojiwekea hupungua au hutoweka
kabisa. Na hivyo wanapofika mwisho wa mwaka wanagundua kuwa hawana kitu cha
kuonesha au wanakitu kidogo tu ukilinganisha na malengo waliokuwa nayo wakati
wanaanza mwaka.
Jambo hili
tunaweza kuliona hata kwa wanaisraeli walipokuwa wanatolewa katika utumwa na
kupelekwa katika nchi yao ya ahadi. Wakati wanatoka walikuwa na hamasa kubwa na
nguvu na matumaini ya kufikia nchi ya ahadi; lakini kwa kadiri walivyokuwa
wanaendelea na safari hamasa, matumaini na nguvu ya kufikia ahadi iliyokuwa
mbele yao ilikuwa ikipungua kwa baadhi yao. Ukitizama safari yao utagundua kuwa
kilichofanya hamasa na matumaini yao
kupungua kadiri walivyosonga mbele, ni kitendo cha wao kuacha kuangalia (Paying
attention) Ahadi na kuanza kuangalia changamoto walizokuwa wanakutana nazo
njiani.
Je unapokutana
changamoto katika mipango uliojiwekea katika mwaka huu, unachagua kuangalia
nini? Unaangalia changamoto au unaangalia malengo yako? Ukitumia muda mwingi
kutafakari changamoto uwe na uhakika hamasa na nguvu hupungua na hatimaye
huweza kutoweka kabisa. Lakini ukitumia muda wako kutafakari malengo yako na kutafuta
namna ya kufanikisha (Mfano; Kutafuta maarifa zaidi kwa kusoma vitabu au kurudi
shule tena, kutenga muda mwingi zaidi wa kufanyia kazi jambo hilo, kutafuta
ushauri, kujifunza kwa waliokutangulia/ waliofanikiwa, kurudia tena
uliposhindwa mara ya kwanza n.k) uwe na uhakika mwisho wa mwaka au muda uliojiwekea utakuwa na kitu cha kuonesha na sio maneno
matupu ya kwanini ulishindwa.
Katika kufikia
malengo au mipango uliojiwekea mwanzoni mwa mwaka au mwezi au kipindi chochote
kile changamoto hutokea au naweza kusema haziepukiki kwa namna moja au
nyingine. Changamoto ndizo zinatufanya tushangilie na kuwa na moyo wa shukrani
pale ambapo tumefikia malengo hayo. Kumbuka jambo hili: Kama ni rahisi
(hakuna changamoto) kila mtu angefanya. Changamoto haziji ili kufisha ahadi
yako, bali zinakupa fursa ya kuona Ukuu na Utukufu wa Mungu kwa namna ambayo
hujawahi kuona. Ni changamoto ya wanaisraeli ndio iliyofanya tutambue Mungu
anaweza kufanya njia mahali pasipo na njia. Mtu hapewi tuzo kwa kusimulia namna
changamoto zilivyomkwamisha; hupewa tuzo kwa kuonesha namna gani ameweza
kufikia malengo yake katikati ya changamoto.
There’s a place
for you at the top!
0 comments :