Ninapotoa dhabihu ya shukurani

2:29:00 PM Unknown 0 Comments

NINAPOTOA DHABIHU YA SHUKRANI “
“Atoaye dhabihu za kunishukuru, ndiye anayenitukuza (anayeniheshimu); anaanda njia ya Mimi kumuonesha wokovu wa Mungu” Zab 50:23 (NIV)
Ili uweza kutafakari mstari tajwa hapo juu ni vema uweke jina lako au ujitazame katika mstari huo. Ni wewe unayemtukuza? Je, ni wewe unayejiandalia njia ya wokovu wa Mungu? Mara nyingi watu hufanya jambo baada ya kutambua uzito au umuhimu wa jambo hilo. Si watu wengi sana wanaelewa umuhimu wa kuwa na moyo wa shukrani mbele za Mungu; hivyo ni rahisi sana kwa mtu kuomba akiwa na hitaji, lakini ni watu wachache sana wanaokumbuka kushukuru baada ya kujibiwa mahitaji yao.  Lakini pia, Mbali na kumshukuru Mungu baada ya kujibu maombi yako, unaweza kujizoeza au kujifunza kuwa na moyo wa shukrani mbele za Mungu kama tabia au mtindo wa maisha yako (A grateful heart).
Kuna tofauti kubwa kati ya kushukuru baada ya Mungu kujibu ombi la mahitaji yako na kuwa na moyo wa shukrani. Moyo wa shukrani ni zaidi ya kushukuru, ni mfumo au utaratibu wa maisha ya mtu. Kushukuru kunaweza kutokea mara moja au kwa msimu, lakini moyo wa shukrani ni tabia au mfumo wa kimaisha endelevu.
Ni mtu mwenye moyo wa shukrani pekee ndiye anayeweza kumshukuru Mungu katika kila jambo. Kumbuka kuna tofauti ya kumshukuru Mungu kwa kila jambo na kumshukuru Mungu katika kila jambo. Tafasiri ya kiingereza ya 1 Wathesalonike 5:17 inasema “toeni shukrani kwa Mungu katika kila hali/jambo kwa kuwa hayo ni mapenzi ya Mungu kwenu” (tafasiri isiyo rasmi). Kinachowafanya baadhi ya watu washindwe kumshukuru Mungu ni hali ya kutokuamini kwamba hayo ni mapenzi ya Mungu. Tukijua kwamba yatupatayo ni mapenzi yake, tutapenda kumshukuru hata kama mambo hayo yameleta simanzi.
Moyo wa shukrani unamfanya mtu ahesabu Baraka za Mungu katika maisha yake kuliko changamoto zake. Ni moyo wa shukrani pekee ndio unaoweza kumfanya mtu aone Mungu ni mkubwa kuliko hali yake. Moyo wa shurani humfanya mtu kuacha kulalamika juu ya kile ambacho Mungu hajajibu na kuanza kumshukuru Mungu juu ya kile ambacho amewahi kujibu.  Moyo wa shukrani hutafuta sababu ya kumshukuru Mungu katika kila jambo na kila hali. (Zab77:2, 6-10,11-19)
Mtume Paulo alipopelekwa gerezani naweza kusema bila shaka hakumshukuru Mungu kwa kutupwa gerezani lakini nina uhakika kuwepo kwake gerezani hakukumzuia kumshukuru na kumsifu Mungu. Hii inatupa kuona kuwa inawezekana kumshukuru Mungu katika kila jambo, na huu ndio moyo wa shukrani yaani mfumo wa Maisha.  (Matendo ya Mitume 16:25-26)
Moyo wa shukrani unatoa fursa kwa Mungu kudhihirisha wokovu wake. Kwa lugha rahisi, moyo wa shukrani hutoa fursa kwa nguvu za Mungu kuwa tayari muda wote (standby) ili kukusaidia utakapohitaji; ndio maana mstari wetu wa kutufungulia hapo juu unasema, “anaandaa njia ya Mimi kumuonesha wokovu wangu”. Moyo wa shukrani huvuta upendeleo (kibali) wa Ki-Mungu katika maisha ya mtu kuliko anavyoweza kufikiri. Ningeweza kusema, kushukuru kunavuta wingu la upendeleo wa Ki-Mungu (God’s favor); lakini Moyo wa shukrani hushikilia wingu la upendeleo wa Ki-Mungu ili kukaa katika maisha ya mtu (cause it to dwell).

0 comments :