Uzuri unadanganya
UZURI UNADANGANYA.
(Beauty is
fleeting)
Nimewahi kupewa ushauri kutoka kwa watu
mbalimbali kuhusu masuala ya mahusiano na ndoa. Nimejitahidi pia kusoma walau
vitabu kadhaa. Yote kwa yote kuhusu ndoa na mahusiano sitasahau ushauri huu,
“uzuri/urembo unadanganya.” Kwa nini unadanganya? Kwa sababu si wa kudumu, na
si kitu utakachokihitaji kila siku.
Si vema kumpuuza mtu mwenye hekima
anapofumbua kinywa chake kusema kitu. Solomon mtu mwenye hekima sana ndiye
aliyesema katika Mithali 31:30, “uzuri si wa kudumu” Yaani sura, mpangilio wa
meno, rangi na umbo zuri havisemi kweli maana baada ya muda mtu huzeeka na
ngozi hukunjamana, na mara urembo wote hutoweka. Maana yake uonavyo leo sivyo
itakavyokuwa milele. Kwa lugha nyingi si mambo utakayoyahitaji baadaye. Baada
ya muda kupita utagundua haukuhitaji sura bali ulihitaji, upendo, ushirika,
amani na uaminifu. Kwa nyakati tofauti wachungaji na wenye hekima wameonya
kwamba,kufanya uamuzi kwa kujali mwonekano wa nje ni hatari.
Amesema mwenye hekima huyu, “Mwanamke
aliye na umbo zuri na sura nzuri pasina maarifa kichwani afaa kwa usiku mmoja,
lakini yule mwenye ufahamu na maarifa afaa kwa maisha yote.” Ndoa ni agano la
maisha si la usiku mmoja. Mwonekano wa nje hautoshi kutoa taswira ya ndani ya
utu, uchapakazi, uaminifu na upendo.
Urembo ukisimama peke yake hautoshi,
utanashati peke yake hausaidii. Haipasi kuwa urembo na utanashati, badala yake
inafaa kuwa urembo na akili, urembo na uchapakazi, urembo na ibada, urembo na
upendo, urembo na uaminifu.
Ili urembo usikudanganye basi ni lazima
uwe umeujua ukweli. Tafuta watu wanaoheshimika utagundua si kwa rangi zao wali
si kwa urembo na utanishati wao bali ni kwa kujitoa sadaka, kuishi maisha ya
heshima, uaminifu na utu wema.
Wewe si Mr. Tanzania unaanzaje kuoa Miss
Tanzania? Urembo unadanganya.
Tukutane kileleni………
0 comments :