Rafiki Mpya, Mambo Mapya

11:29:00 AM Unknown 0 Comments

  
RAFIKI MPYA, MAMBO MAPYA
(Angalia ingizo la rafiki mpya)
Imenenwa katika Mithali 28:24: “Aibaye mali ya babaye au mamaye, na kusema, Si kosa; Mwana huyo ni rafiki wa mtu mharibifu.”  Ziko tabia au mambo ambayo yanapotokea kwako au kwa rafiki yako yanataka kukuonesha kwamba umejiunga na rafiki mwovu au kikundi kibaya.

Mtoto akipata rafiki wabaya atamwibia babaye, kadhalika mtumishi akipata marafiki wabaya ataiba mali ya ofisi (mali ya BOSS). Kuchukua kitu cha nyumbani kwenu bila ridhaa ya wazazi ni wizi, kuchukua mali ya ofisi bila utaratibu si haki. Ukiona mtu anamkono mrefu, anaiba mali za kwao au ya kampuni inayomlipa mshahara ujue amepata marafiki wabaya.
Ukiona mtazamo wako juu ya amri za Mungu unabadilika (huoni yaliyokatazwa) basi jiulize ni nani ameingia katika maisha yako. Ukiona mtazamo wako juu ya mume/mke wa mtu unabadilika basi jiulize ni nani unashinda naye kila siku.  Rafiki mpya huleta tabia mpya, nzuri au mbaya.
Kuna watu wanasema kuiibia serikali si dhambi, hawa ni rafiki ya watu waovu, kuna wanaosema mume/mke ni wa kwako akiwa ndani tu, hawa nao ni rafiki ya waasherati. Biblia inakataa kitendo cha kuiba na kusema ni kosa, yuko mwizi anayejua wizi ni kosa na yuko mwizi aliyehalalisha wizi na haumii tena kwa sababu kitendo hicho kwake si dhambi.
Marafiki wabaya hufanya hata dhambi ionekane kama si kosa, humbadilisha mtu akili ili autazame uovu kama wema. Biblia inasema, “aibaye na kusema, si kosa, ni rafiki ya mtu mharibifu.” Mharibifu wa nini? Mharibifu wa akili. Mithali 28:24
Yuko pia aziniye na kusema si kosa, yuko atoaye rushwa na kusema si kosa, yuko atorokaye shuleni na kusema si kosa, yuko pia adanganyaye na kusema si kosa!
Wazazi wengi wamekataa watoto wao wasihusiane na vijana waharibifu. Wanaharibu akili, wanageuza moyo, na hivyo mtu huangamia bila kujua. Katika kuwapima marafiki tujifunze kwa Yesu: Hawa ni wanafunzi watatu marafiki wa Yesu; Petro mtu wa imani ndiyo yule Kefa, mwanafunzi msemaje aliyesema kuwa, Yesu ni Kristo, Yohana alikuwa mtu wa upendo sana ndiyo yule aliyelala kifuani pa Yesu, na Yokobo mtu mwenye tumaini saana ndiye yule alitufundisha dini njema ya kuona wagonjwa na kulisha masikini. Kwa kuzungukwa na hawa watatu Yesu alichagua kuwa salama ki akili. Alizungukwa na mwenye upendo, imani na tumaini.
Wewe pia ni wastani wa watu wako watano wa karibu, Angalia tabia zako mpya, ujue mchango na uwekezaji wa kitabia ulifanywa na rafiki zako katika maisha yako. Ikiwa haiwezekani kuwashauri kubadilika achana nao, Cut off the link! Usitoe muda wako kwa marafiki wabaya, Mungu akupe neema ya kuachana nao na kujitenga.
Tukutane juu pamoja na watu wako watano wa karibu sana.

0 comments :