Ubongo hauna rangi

7:37:00 PM Unknown 0 Comments

  
UBONGO HAUNA RANGI
(Brain has no colour)
Hakuna utofauti wa akili kati ya bara moja na lingine, hakuna utofauti katika kuumbwa kwa Mzungu na Mwafrika, sote tu sura na mfano wa Mungu. Hakuna tofauti kati ya watu wa magharibi na watu wa kusini. Kila mtu anaweza kuwa atakavyo, na anaweza mambo yote. Kila mwasisi wa Taifa ana nafasi ya kulifanya taifa lake kuwa nambari moja kwa maendeleo.
Ulipopewa rangi nyeusi ya mwili si kwamba umepewa ubongo mweusi. Ubongo hauna rangi, mtu mweusi hana ubongo mweusi, wala mtu mweupe hana ubongo mweupe, ubongo ni ubongo tu. Ukikuta ubongo mweusi basi ni wewe mwenyewe umeupaka rangi nyeusi. Wakati Wright Brothers wanavumbua urushaji wa ndege wengine wanarogana. Wakati mmoja anaun’garisha ubongo wake kwa kusoma kitabu kizuri mwingine anatazama picha za ngono na hivyo anauchafua zaidi. Sote tumefanya hayo lakini leo makala hii ni simu ya kukuamsha, Brain has no colour!
Ben Carson, Usain Bolt, Hayati Dr Myles Munroe ni miongoni mwa wachache walioihakikishia dunia kwamba, wana ngozi nyeusi lakini hawana ubongo mweusi. Hofu, mashaka, kutokujiamini, uchoyo, ubinafsi, uchafu, uchawi, ulevi, ulafi, uasherati na vingine vingi huchafua ubongo na kufanya uwe na rangi nyeusi. Ili uhakikishe hili, chunguza na utagundua jamii nyingi zenye mambo ya kishirikina ziko nyuma kielimu, na familia za kuhusudu ulevi huwa hazisongi mbele.
Kwa asili mwanadamu anazaliwa akiwa na ubongo wenye kumpa akili ya kutenda mambo yote, kuweza kila kitu kwa wakati. Yale yasiyofaa ambayo mwanadamu huona na kusikia huendelea kumharibu na kufanya awe na hofu, kujidharau, kujiwekea mipaka ya kiutendaji. Wafilipi 4:13
Usimfundishe mwanao kuwatukuza wazungu, bali mwambie ana ubongo sawa na wao na anaweza kufanya zaidi ya wao. Darasa moja, mwalimu mmoja na shule moja lakini matokeo ya watoto huwa tofauti kwa sababu ya vizuizi tunavyowawekea. Mwingine anaambiwa anga ndio kuzuizi chake mwingine anaambiwa ajira, ukiajiriwa tu inatosha mwanangu! Huna wa kuajiriwa hawezi jihusisha na tafiti za kurusha vyombo kwenda mwezini au kupasua vichwa vya watu, hii ni kwa sababu upatikanaji wa ajira ni rahisi na hivyo kufikiri kwenda mwezini au kuwa daktari bingwa ni kama kupoteza muda.
Tatizo lolote ikiwamo la ajira, kabla halijawa la Serikali ni la wazazi wa mtoto, baadaye ni la mtoto mwenyewe, na mwisho ni la nchi. Ubongo wetu unapakwa matope na mafuta machafu ya mawazo mgando ndio maana tunashindwa kufikiri kimkakati.
 Tunashindwa kupenya katika majadiliano yenye maslahi makubwa. Mawazo mabaya si kuzini na kuua watu tu, bali ni uoga. Tunaogopa kuanza, tunaogopa kugombea, tunaogopa kuamka mapema, tunaogopa kusafiri, tunaogopa kukopa, tunaogopa kuacha kazi, tunaogopa kusimamia mawazo yetu, tunaogopa kweda nchi za mbali. Ukienda uwanja wa Ndege utaona wanaoingia kwetu ni wengi kuliko wanaotoka, sisi tunaogopa wao wanakuja. Hawajui lugha yetu, wala hawajui asili yetu ila wanakuja kisha wanafanikiwa na wanaondoka. Jifunze kwa wachina waliojazana Kariakoo Dar es salaam.
Ubongo hauchakai kwa sababu unautumia sana, bali unachakaa kwa sababu hautumii akili. Ni kweli hukupata muda wa kwenda shule sawa, Je, hujapata hata muda wa kufikiri? Tofauti kati ya msomi na mtu ambaye hakusoma ipo kwenye kufikiri. Ukiweza kufikiri vizuri na kupanga kimkakati basi wewe ni msomi. Ni vijana wachache ambao hufikiri kimkakati yaani akapanda au akawekeza katika mradi utakao mlipa baada ya miaka hamsini.
Azimio la Arusha lilikuwa tunda la akili ya mwalimu Nyerere, Tuzo ya Nobel ni mtoto wa akili ya Mzee Alfered Nobel aliyesikia sifa zake mbaya na kubadilika. Afrika kusini huru ni mtoto wa akili wa Hayati Nelson Mandela, Microsoft Cooperation ni mtoto wa Bill Gate, TANU si ni mtoto wa Mwalimu Nyerere.
Je, akili yako imetuzalia nini cha maana? What is your brain child?
Wanaotumia akili zao vizuri hubuni, huanzisha na huvumbua. Huasisi mataifa, huanzisha viwanda na makampuni, huanzisha taasisi zao. Hawafi wakiwa wamelala kitandani, hufa wakiwa katika mapambano ya kukamilisha azma na wito wao.

0 comments :