Inachukua Muda....

5:32:00 PM Unknown 0 Comments

 
Inachukua Muda...

Tunaishi katika ulimwengu ambao karibu kila eneo watu hutaka huduma kwa haraka; usafiri wa haraka (mwendokasi), chakula cha haraka (fast food), mikopo ya haraka, huduma za kifedha na afya kwa haraka (fast track) n.k ! Hakuna anayetaka kukaa muda mrefu kwenye foleni kusubiria huduma. Maendeleo ya sayansi na tekinolojia yamerahisisha upatikana wa huduma nyingi katika jamii na kwa haraka zaidi wakati huu, kuliko miaka kumi iliyopita.
Pamoja na mchango mkubwa wa sayansi na tekinolojia katika upatikanaji wa huduma, watu wengi wamesahau baadhi ya kanuni muhimu za mafanikio ya kweli; katika ulimwengu huu wa haraka haraka, jamii imesahau kuwa mafanikio ya kudumu huchukua muda kuyajenga. Kanuni hii ni rahisi sana kusahaulika katika ulimwengu wa haraka.  Ya kwamba mahusiano mazuri yanachukua muda kuyajenga, familia nzuri inachukua muda kuijenga, mafanikio ya kifedha, huduma, taaluma pamoja na 'career' haya yote huchukua muda kuyajenga.
Ni mwanafunzi anayeamini katika ulimwengu wa haraka kwenye taalumu hufanya bidii aweze kuiba au kuibia kwenye mtihani, ni kijana anayeamini tu katika ulimwengu wa haraka hushinda kijiweni "akibeti" ili kufikia mafanikio ya kifedha. Ndio maana ni rahisi kwa mtu kwenda kucheza "desi" ili apokee mara asilimia mia tatu (300%) kuliko kuwekeza kwenye ufugaji wa kuku, kwa sababu anaona hatapata hiyo asilimia mia tatu haraka. Hutaka kupata kwa haraka bila kufanyia kazi. Nitajie tajiri aliyeko kwenye orodha ya matajiri kwa sababu alishida bahati nasibu au desi; go back to Work!!
Watu ambao hawajui kuwa mahusiano bora na imara huchukua muda kuyajenga wakitofautiana kidogo huvunja uhusiano huo na kama ni wana ndoa hutishia kutengana kabisa. Mzazi ambaye anayeamini katika ulimwengu wa haraka katika malezi, hana muda wa kukaa  na watoto kuwafundisha na kufuatilia malezi yao kwa karibu; wakishapotea na kuharibika kimwenendo hukimbilia kwa watumishi wamuombee ili wapone na kurudi kwenye njia sahihi kwa haraka, amesahau alikuwa na nafasi katika kujenga mwenendo bora kabla.
Anayejenga nyumba juu ya mwamba hutumia muda kuijenga, na kwa sababu hiyo nyumba hiyo itakuwa imara kuliko anayejenga juu ya mchanga.  Kuna baadhi ya maeneo ulimwengu wa haraka hauleti matokeo bora, bali kanuni ya muda!  Mwenyehekima mmoja amewahi kusema "usikimbie mahali panapokutaka kutembea; na usitembee mahali panapokutaka kukimbia "
Mali iliyopatikana kwa haraka itapunguka; Bali yeye achumaye kidogo kidogo atazidishiwa-Mithali 13 :11
There's a place for you at the top

0 comments :