Mungu ni mwakilishi wetu

11:58:00 AM Unknown 0 Comments

 
MUNGU NI MWAKILISHI WETU.
(Anajua kupigana vizuri kuliko sisi)
Tunaishi kwenye ulimwengu wenye changamoto nyingi, watu wanafukuzwa kazi, yatima wanadhulumiwa; wanafunzi wanafeli, wazazi wanagombana, wapenzi wanaachana na vikao vya kazi havimaliziki kwa usalama.
Yote haya yanamfanya mwanadamu ajitahidi kuyakabili bila ya Mungu. Kuna kitu kinamwambia mwanadamu apigane mwenyewe, kuna msukumo usiotaka kumruhusu Mungu apigane.
Kwa nini tunashindwa kumruhusu Mungu aingilie kati? Ni kwa sababu tunadhani tunajua kupigana kuliko Yeye au ni kwa sababu tunafikiri atasahau. Ukweli ni kwamba Mungu anajibu kwa wakati, yuko makini kuliko wahudumu wa chumba cha watu mahututi.
Siku moja usiku baada ya kuona nyumba yangu imezingirwa na mambo yasiyofaa niliamua kumwita BWANA YESU na dakika ile ile shwari ilirejea. Namshangaa Mungu kwa maana amewapa mamlaka kuu wale wanaompigania. Hudson Taylor akijua fika atakwenda nchi ya mbali kwa uinjilishaji, alijifunza kumtegemea Mungu kwa kila jambo. Hata alipotaka pesa hakumwambia mkuu wake wa kazi bali alimwambia Mungu katika maombi. Ananukuliwa, “ni vema nijifunze kumwomba Mungu kwa kila jambo, maana huko China niendeko hakuna mtu wa kumwomba wala kumtegemea”.
Katika biblia tunaona Mungu amekuwa sauti ya wasio na sauti, amewakumbuka matabaka ya walioonewa. Yeye ni Mungu wa vita, anajua kupigana tena ameshinda vita zote. Kuomba ni kumchagua Mungu awe mwakilishi wako katika vita. Ndio maana biblia imeyaita maombi silaha. Waefeso 6:11
Uwezo wa mwanadamu unakikomo, hata akijitahidi hawezi kutuliza yote yanayomsonga. Taarifa ya habari si taarifa yenye habari za kutia tumaini bali ni taarifa yenye habari mbaya; mafuriko, njaa, migomo, ugomvi, kupunguzwa kazini, vifo na magonjwa.
Nakumbuka siku moja nilipopokea taarifa ya kutisha kwamba mpendwa wangu yuko mbioni kufa. Niliogopa sana! Moyo wangu ulizimia kwa hofu. Siku yangu ilikwenda mrama kabisa. Mara ghafla jioni rafiki yangu akanishauri na kutumia Zaburi 46:1-3. Na hapo nikapata nguvu, na hapo nikapata upenyo na hapo nikasimama tena. Na hapa nikajua kama ni vita si mimi nitakaye kufa, bali ni wenzangu ndio watafia nchi zao na falme zao.
“Mungu kwetu sisi ni kimbilio na nguvu, Msaada utakaoonekana tele wakati wa mateso.
Kwa hiyo hatutaogopa ijapobadilika nchi, Ijapotetemeka milima moyoni mwa bahari.
Maji yake yajapovuma na kuumuka, Ijapopepesuka milima kwa kiburi chake.” Zaburi 46:1-3
Nikamkimbilia Mungu kwa sala, tukashinda vita na mpendwa wangu akawa salama! Tishio la kifo, ajali, hukumu ya Mahakama, Waganga, Wachawi halina uwezo wowote kwa yule ajuaye kuliitia jina la BWANA, yule aliyepaka damu ya Yesu ya Pasaka.
Kujiambatanisha na Mungu ni kujiambatanisha na ushindi. Kama wakristo sisi ni washindi, maana tu uzao wa ushindi.
Mkimbilie Mungu ukiwa na cheti cha daktari, mwambie utaishi kwa neno lake wala si kwa chakula, wala si kwa neno la daktari. Ingawa tunaheshimu mchango wa kila taaluma lakini Bwana ndiye atakaya maneno yote, kwa kuwa Yeye ni mwanzo tena mwisho. Hata kama umetenda dhambi usisite kumwendea Mungu wakati wa changamoto yako. Yeye ni kimbilio wakati wa shida, shida zinaturejesha kwake.

0 comments :