Mheshimu Rais Wako
MHESHIMU
RAIS WAKO
(Ni kwa
Heshima ya aliyemweka katika kiti hicho)
Ukiwa mtawala au
mmiliki wa biashara unaweza kumweka yeyote asimamie biashara hiyo kwa niaba
yako, asimame kama mwakilishi wako. Mwakilishi huyu bila shaka atakuwa na amri (authority
and power) kwa wale utakao waweka chini yake ili awaongoze na kuwasimamia vema.
Mwakilishi huyu akidharauliwa bila shaka wewe uliyemweka umedharauliwa pia. Serikali haziwekwi na wapiga kura, zinawekwa na Mungu.
Maeneo mengi tumeshuhudia wenye kura nyingi wakikosa Urais. Wanademokrasia
wenye imani wanaelewa hili.
Tunapaswa kuwaheshimu
viongozi si kwa sababu ni wema au ni wabaya bali, ni kwa heshima ya yule
aliyewaweka watuongoze yaani, Mungu Baba. Ameandika Mchungaji Kenneth Copeland,
“Hakukuwa
na Serikali korofi kama ile ya wakati wa Yesu Kristo, lakini bado Yesu alitaka
iheshimiwe na akasema, ‘yaliyo ya Kaisari apewe Kaisari.’” Kwa maneno
mengine Kristo aliwataka watu walipe kodi kwenye Serikali ambayo kimsingi
ilikuwa inawakandamiza, hata wao hawakuamini kama Yesu amesema waheshimiwe kama
Serikali. Serikali yaweza kuwa dhalimu lakini Mungu aliyeiweka kwa majira
husika si dhalimu, na anamakusudi nayo.
Muda mzuri
wa kuiheshimu Serikali ni pale inapofanya vibaya, maana ikifanya vema hata
wapagani huiheshimu (Luka 6:28).
Muda mzuri wa kubariki ni pale watu watakapo kulaani. Katika agano la kale
Serikali ya Farao yule wa wakati wa Musa ilikuwa korofi na yenye kiburi hata
mbele za Mungu, lakini Mungu alisema ni yeye aliyeiweka kwa makusudi yake. Kuna
kusudi kwa serikali yako. Serikali haijiweki madarakani inawekwa. Katika Warumi
9:17 neno nimekusimamisha linaweza kuwa na maana, nimekuweka. “Kwa maana
maandiko yasema juu ya Farao, ya kwamba, Nilikusimamisha kwa kusudi hili, ili
nionyeshe nguvu zangu kwako, jina langu likatangazwe katika nchi yote.” Warumi
9:17
Tunamuheshimu mkuu wa
nchi kwa sababu tunayo hofu ya Mungu
aliyemweka. Si kila Mtawala (Boss) anastahili heshima kutokana na tabia yake,
wengine wanatabia mbaya. Pamoja na hayo kila Mkristo anapaswa kutoa heshima kwa
kila mtawala bila kujali tabia yake.
Angalizo:
Katika kumtii kiongozi
lazima tuhakikishe hatumkosei Mungu, kiongozi asigeuke sanamu moyoni mwetu.
Sauti ya kiongozi ikiwa kinyume na injili ya Kristo na ipuuzwe. Mijadala mambo
ya mapenzi ya jinsia moja, mauji ya holela, utoaji wa mimba unaohalalishwa
kisheria, ndoa za mitala ni mambo ambayo ni kinyume na injili. Yapuuzwe hata
kama msemaji atakuwa ni mkuu wa Nchi.
Mungu anaweza
kubadilisha moyo wa kiongozi ikiwa watu watasimama kuomba. Maombi kwa Mungu
mwenye nguvu yanaweza kuelekeza nchi wapi ielekee ikiwa mwombaji ataomba kwa
bidii. Mungu anaendesha mioyo ya watawala kupitia maombi ya watakatifu.
Endelea
kuombea nchi yako….., Shallom Israel, Shallom Tanzania….
0 comments :