UNATUMIA KIUNGO GANI KUTAZAMA MBALI?

 
UNATUMIA KIUNGO GANI KUTAZAMA MBALI?
Mwili wa binadamu unaviungo vingi kila kimoja kikiwa na kazi yake. Ipo pia milango ya fahamu ambayo kwa kuhisi, kunusa, kuonja na kwa kuona hufanya kazi. Viungo hivi na milango hii ya fahamu si tu kwamba ipo kwa binadamu bali hata wanyama, ndege na baadhi ya wadudu wamejaliwa na Mwenyezi kuwa nayo.
Binadamu ndiye mwenye jukumu la kuwatawala ndege, wanyama, wadudu na hata viumbe wasioonekana (mapepo, majini, malaika). Kitabu cha Waebrania kimeeleza malaika ni roho wanotuhudumia, pia mzaburi amenena wazi jinsi Mungu alivyomfanya mwanadamu punde tu kama yeye na amemvika utukufu na heshima.
Licha ya utukufu huo mwanadamu si kiumbe mwenye uwezo mkubwa wa kuona. Tai, mwewe na hata ndege wengine huona mbali zaidi kuliko mwanadamu. Ni watu wachache tu wenye macho makali ya kuona mita mia tano au zaidi.
Swali, Ni kwa nini macho ya wanadamu ambao kibiblia ndio watawala wa dunia hii yanazidiwa na hawa ndege? Jibu langu ni rahisi, Mungu hakutaka mwanadamu aishi kama tai, Hakutaka mwanadamu aone mbali kwa macho ya nyama bali atumie akili, fikra na imani katika kuona kwake. Kwa njia hizi ataona mbali zaidi ya tai na hivyo atamtawala mpaka tai.
Mwanadamu anauwezo wa kuona hata miaka 20 ijayo na akanunua shamba leo na kupanda miti. Mwanadamu wa leo anaweza kuona miaka 100 ijayo. Hayati Rais Kennedy wa Marekani anayetajwa katika simulizi za kwenda mwezini, aliwaita wanasayansi wake na kuwapa wazo hilo ambalo hawakuwa wamewahi kulisikia popote. Hebu waza unamka unaitwa na Rais na anakwambia, naomba uanze kufikria jinsi gani tutakwenda kwenye Mwezi au Jua. Wakati huo wewe hujawahi hata kuzifuatilia nyota za angani.
Baada ya wanasayansi hao kufanyia kazi wazo hilo kwa miaka kadhaa walifanikiwa na kwa sasa kwenda mwezini au kutuma vyombo kwenda huko si jambo la ajabu tena. Tofauti na hayati Rais Kennedy ambaye ni mtu wa fikra, Rev Martin Luther King Jr ambaye ni mwanaharakati, yeye katika harakati zake za kumkomboa mtu dhidi ya ubaguzi  wa rangi anaonekana kuona mbali kama nabii, na hii ni kwa sababu ya Imani yake ambayo mzizi wake ni neno la Mungu.
Alisema Fred Swaniker kwamba, Afrika inahitaji Moon shoot thinking, akimaanisha tunahitaji kufikiri mbali sana, tunahitaji kuruka kifikra (kimawazo) na kutua mbali, mahali ambapo kwa uhalisia macho ya kawaida hayapaoni ila kwa imani na fikra sahihi tunapaona.
Katika ulimwengu huu hata kipofu anaweza kufanikiwa kama ubongo wake umechangamka kuliko watu mia wenye macho makali lakini ubongo umelala. Kuna jambo linanishangaza katika taifa langu, vijana wengi ukiwahoji si watu wa fikra.
Siku 1000 za kwanza katika ukuaji wa mtoto zijulikanazo kama “mwanzo bora” zina mchango mkubwa katika uwezo wa kufikri wa mtoto. Utapia mlo ndio huzaa watu wenye mawazo mgando, na mawazo maji, yote ni matokeo ya mdororo wa chakula. Mfumo wetu wa elimu hauruhusu udadisi hasa kwa kuwa mwalimu ndio kila kitu, si rahisi mfumo wetu kuzalisha watu wanaofikiri kimkakati.
Ili tupate vijana wanaofikiri sawasawa basi ni muhimu tuwajenge kwa neno la Mungu ambalo litaleta imani, tuwape chakula bora cha akili yaani vitabu sahihi vya kiada na ziada, watoto wapewe mlo kamili ukijumuisha matunda, vyakula vya wanga, protini na maji mengi.

Kuelekea Uhuru wa Kifedha - II

 
KUELEKEA UHURU WA KIFEDHA II
(THE BIBLICAL LAWS OF MONEY)
Toleo lililopita tuliangazia kanuni moja muhimu sana ili kuelekea mafanikio ya kiuchumi katika maisha ya mtu; kanuni ya uzalishaji bidhaa au huduma. Kanuni hii huwa haimzungumziwi sana lakini ni kanuni muhimu sana kuelekea uhuru wa kifedha. Kumbuka, Fedha unazozitafuta zipo kwa watu, ili kuzipata lazima uwe na kitu cha kubadillishana (exchange). Hakuna namna utafikia uhuru wa kifedha endapo hakuna bidhaa wala huduma ambayo unaweza kutoa na watu wakakupa fedha.
Kwa mtu ambaye ameajiriwa maana yake anauza huduma, na hivyo mwisho analipwa mshahara. Mshahara unakuja kama matokeo baada ya kutoa huduma, vivyo hivyo mfanyabiashara au mjasiriamali au hata makampuni hupata fedha kutokana na bidhaa au huduma wanayozalisha.  Fedha ni matokeo ya bidhaa au huduma anayotoa mtu. Mwalimu wangu mmoja amewahi kusema, “If you don’t create or add value to others (through goods or service), you are not entitled to receive money” (Kama hauna bidhaa au huduma unayoweza kutoa kwa watu, haustahili kupokea fedha ya mtu: Tafsiri isiyo rasmi)
Mtu pekee anayeweza kuwa na uhakika wa kupata fedha bila kubadilishana na huduma au bidhaa moja kwa moja ni serikali, yenyewe inakusanya kodi. Hivyo watu watake au wasitake ni lazima serikali ikusanye fedha kutoka kwao kama kodi kwa mujibu wa sheria za nchi husika. Mimi na wewe hatukusanyi kodi, watu hawalazimiki kisheria kutupa fedha zao; hivyo basi ili kupata fedha zao lazima tuwe na kitu wanachokiitaji na kwa sababu hiyo wako tayari kukilipia ili kukipata kitu hicho. Na hapo ndipo tunapoweza kuona fedha inaingia mifukoni mwetu.
Swali unaloweza kujiuliza au unalotakiwa kujiuliza sasa, ni bidhaa gani au huduma gani unaweza kuizalisha au kutoa ambayo watu (jamii inayokuzunguka) wanahaja nayo na watakuwa tayari kuilipia ili kuipata? Iwe umeajiriwa au hujaajiriwa hili ni swali muhimu sana kama unataka kufikia uhuru wa kifedha (kutimiza mahitaji yako YOTE, na kupata ziada kwa ajili ya kufikia mahitaji mengine yanayokuzunguka; maana utamsaidiaje anayehitaji ‘chakula’ wakati hata wewe huna: Mathayo 25:37-40).
Sam Adeyemi amewahi kusema  It is not the absence of money that makes a person poor; it’s the absence of right idea (thought) that has value”. Yaani “Si ukosefu wa fedha ndio humfanya mtu kuwa masikini bali ukosefu wa wazo lenye thamani”. Hivyo kumbe fedha ni matokeo tu; yaani matokeo  ya wazo lenye thamani ambalo huzaa bidhaa au huduma; ambazo mtu hubadilishana (exchange) na fedha.
There’s a place for you at the top!

Kuelekea Uhuru wa Kifedha

 
KUELEKEA UHURU WA KIFEDHA
(THE BIBLICAL LAWS OF MONEY)
Tafiti mbalimbali zinaeleza kwamba, moja ya changamoto kubwa ulimwenguni hasa bara la Afrika ni umasikini mkubwa wa kipato. Ni ukweli unaosikitisha, na eneo hili ni moja ya maeneo ambayo hayana msisitizo mkubwa ndani ya mwili wa Kristo (kanisa). Eneo la maarifa kuhusu fedha au uchumi ili kumkomboa mtu kiuchumi ni kama limeachwa; Na kwa sehemu kubwa ukiona mahali fedha inatajwa kanisani au kikundi cha sala basi ujue ni sadaka inayozungumziwa. Ni watu wachache sana wanaozungumzia au kuhubiri au kufundisha maarifa kuhusu fedha na uchumi ili kumuwezesha mtu kupiga hatua katika eneo hilo kwenye maisha yake na jamii yake.
Jambo moja ambalo ni halisi na halikwepeki ni kwamba, ili kuishi katika ulimwengu huu wa sasa kila mtu anahitaji fedha za kutosha kumuweza kukidhi mahitaji yake na mahitaji ya wale wanaomzunguka. Kumbuka fedha haina dini, haijali kabila wala rangi yako; haiwezi kuja kwako kwa sababu wewe ni wa dini au dhehebu au rangi au kabila fulani (it is neutral). Na kwa sehemu kubwa, kiwango cha fedha au mafanikio ya kiuchumi ya mtu yanategemea kiwango cha maarifa na ufahamu sahihi alionao juu ya kanuni za fedha (The laws of money).
Nakumbuka siku moja wakati nipo sekondari niliwahi kuhudhuria kikundi cha sala mahali  fulani, na siku hiyo tukafundishwa kuwa ili kufanikiwa kifedha basi ni lazima tutoe sadaka ya kupanda ili makusudi tuvune mara mia kwa kigezo kwamba ukitoa utapokea mara mia ya ulichotoa (bila shaka unakumbuka hilo andiko). Na tena nikakumbuka lile andiko la kila apandacho mtu ndicho atakachovuna, basi nikapiga hesabu zangu pale, kwamba endapo nitatoa elfu moja basi nitarajie kupokea laki moja (bila shaka sijakuacha hata kama ulikimbia hesabu, elfu moja mara mia ni laki moja). Sijui kama unaelewa maana yake nini upo sekondari unatarajia kupokea laki moja ya kwako binafsi (hahahaha). Nikawaza tu nikiipata hiyo laki moja napanda elfu kumi, sasa piga hesabu hapo elfu kumi mara mia, mavuno ni kiasi gani? (tajiri mtoto anayechipukia).
Japo unaweza kucheka, inawezekana umewahi kuwaza hivyo pia. Kanuni moja muhimu sana kuhusu fedha ambayo huwa haifundishwi na leo nataka niigusie ni kanuni ya uzalishaji bidhaa au huduma (The law of production). Pamoja na kwamba sadaka na maombi ni muhimu sana kwa ustawi wa mtu; ni ukweli uliowaza kwamba hakuna aliyefanikiwa kiuchumi kwa mambo hayo TU (bila uzalishaji huduma na bidhaa) isipokuwa aliyepo upande wa kupokea.  Wazo kuu tunalotaka ulipate kwa siku ya leo ni kwamba, ukitaka kufanikiwa kiuchumi hauwezi kukwepa uzalishaji bidhaa au huduma kwa namna moja au nyingine.  Nioneshe anayeuza bidhaa au huduma, nikuoneshe mtu atakayefanikiwa kiuchumi. Zalisha huduma au bidhaa ambayo tunauhitaji nayo, na sisi tutakuwa tayari kukupa fedha kwa kuipata bidhaa/huduma hiyo kwa sababu tunaihitaji na hapo mafanikio ya kiuchumi yatakuwa dhahiri kwako.
Mungu ameahidi mvua ya Baraka, sio mvua ya fedha. Mungu ameahidi kushusha Baraka kwenye kazi ya mikono yako, kapu lako na chombo chako cha kukandia unga, mifugo yako, mazao shambani kwako, hakuna mahali ameahidi kushusha fedha toka juu. [Kumbukumbu la torati 28:4-5, 8]. Kusubiri mavuno ya sadaka uliyopanda tangu mwaka juzi ili utoke kwenye mkwamo wa kiuchumi uliona sasa, ni uvivu wa kufikiri, na ni kukosa uwajibikaji (irresponsibility).
There’s a place for you at the top!

USIWAPELEKE MAHALI USIPOWEZA KUWATOA

 
USIWAPELEKE MAHALI USIPOWEZA KUWATOA
Hili ni jambo la msingi kwa kiongozi wa ngazi yoyote ile, haijalishi ni ngazi ya familia, kata, kampuni, taasisi binafsi au kiongozi wa siasa. Kuna maeneo ukiwafikisha watu au ukiwapeleka unaowaongoza hautaweza kuwatoa wote kwa usalama. Kiongozi lazima awe na kipimo cha madhara na uathirika unaoweza kujitokeza kabla ya kuchukua uamuzi wake.
Kwenye biblia kuna kisa cha Lutu aliyemuita Ibrahimu mjomba. Huyu baada ya kuipeleka familia yake katika miji ya Sodoma na Gomora alishindwa kuwatoa wote. Huko alimpoteza mkewe.  Alitamani waokoke familia nzima kama walivyoingia lakini hakuweza. Ingawa haijaandikwa lakini nina hakika Lutu alijisikia vibaya kumpleleka mkewe mahali asipoweza kumtoa. Sodoma ilikuwa ni uchaguzi wa Lutu nyakati za kutengana na Ibrahamu, haukuwa uchaguzi wa mkewe Lutu. Lakini mkewe Lutu akatazama nyuma yake, akawa nguzo ya chumvi.” Mwanzo 19:26
Rais Obama aliyekuwa kinara katika kuangusha Serikali ya hayati Rais Gadafi wa Libya alinukuliwa akijutia kushindwa kuijenga Libya mpya. Obama amewafikisha watu wa Libya mahali ambapo hawezi kuwatoa. Mpaka ameondoka hajaweza kujenga Libya mpya aliyoahidi na badala yake imekuwa pango la magaidi na wapiganaji.
Amesisitiza mwenye hekima mmoja kwamba, “In life you cannot undo every action” akimaanisha, “Katika maisha si kila kitu unaweza kukirejesha tena katika uhalisia wake.” Kuna akili zilizoharibika, kuna familia zilizoharibika, kuna vikundi vilivyoharibika; kuna jamii zilizoharibika, pia kuna kampuni zilizoharibika na si wote watakao weza kufanya urejesho. Kwa kuwa zoezi la urejesho ni gumu na zito basi ni busara kuepuka uovu, tabia hatarishi na mazingira yake. Huwezi kuepuka moshi ikiwa unapika kwa kuni, kwa hiyo katika kubadilisha mwenendo huwezi kupuuza mchango wa mazingira yako. Mazingira hatarishi ya Sodoma na Gomora ndio chanzo cha uharibifu wa mke wa Lutu.
Kama baba wa familia au kiongozi (Lutu) ni lazima uogope maamuzi au maeneo ambayo huna uhakika kwamba, wale unaowaongoza watatoka salama. Yuko rafiki anayeweza kukufundisha tabia mbaya ambayo huwezi kuiacha, yako makundi mabaya ambayo yanaweza kukufundisha tabia hatarishi ambazo huwezi kuzikomesha. Je, unamkumbuka uathirika uliingia lini maishani mwako? Ulevi, ubwiaji wa unga na dawa za kulevya, utazamaji wa picha chafu na uasherati? Ni baada ya kujisamehe sisi wenyewe ndipo tunapoweza kumsogelea Yesu mwanamapinduzi ili atusamehe na kutupa upya.
Watu wengi wamekuwa wanamwogopa Yesu kwa kuwa ni mwanamapinduzi na wanajua wakimsogelea atapindua tabia zao na atapanda tabia njema. Mwanamke Msamaria aliyekutana na Yesu kwenye kisima cha Yakobo alikuwa na uathirika. Alikuwa amekuwa na wanaume watano, that was an addiction! Na kwa muda ule mfupi Yesu alipindua maisha yake.
Muda, afya njema, ufahamu, malezi ya watoto, umoja na mshikamano ni moja ya mambo ya kulinda sana kwa kuwa hayarejeshiki kirahisi na pengine hayarejesheki kabisa baada ya kuharibiwa.
Jilinde!

Utimilifu wa kusudi lako......

 
UTIMILIFU WA KUSUDI LAKO UTAHITAJI MAFUNGO
Ni kwa zaidi ya miaka mitatu sasa Programu yetu (Life Minus Regret) imekuwa kazini katika kuwasaidia watu kujua makusudi ya kuumbwa kwao na kuyaishi. Tumekuwa tukiwahamasisha vijana wamjue Mungu ili naye awaambie wao (vijana) ni akina nani. Ni Mungu aliyemwambia Yeremia, “nimekuweka uwe nabii wa mataifa” ni Yesu aliyemwambia Petro, “lisha kondoo zangu”, na baadaye akamwambia tena, “chunga kondoo zangu.” Hawa wote walipata kuambiwa kazi zao na wito wao kwa sababu walitafuta kumjua Mungu na kuhusiana naye.
Mambo matatu ni muhimu katika kuhusiana na Mungu; kusali, kufunga na kutoa sadaka. Yesu akasema “nanyi msalipo…,” maana yake anategemea tutakuwa tunasali mara kwa mara, tena akasema, “nanyi mfungapo….” Pia akihimiza “nanyi mtoapo sadaka…” Haya matatu aliyafundisha kwa kuwa yote ni muhimu kufanyika mara kwa mara ili kumkamilisha mtu. Mathayo 5:2, 5, 6 na 16
Sala, sadaka na mafungo ni vitu muhimu katika kuhusiana na Mungu. Katika eneo la sala na sadaka wengi wanajitahidi, changamoto iko katika eneo la ushindi na mafanikio ambalo ni eneo la kufunga. Wengi hupanga kufunga na kabla siku haijafika hughairi na kufakamia chakula. Shetani hatoi ruhusa katika hili kwani anajua lina baraka, tena halijali idadi.
Mafungo ni muhimu kwa ajili ya huduma yako na kusudi lako. Kama Yesu angeweza kutimiza kusudi lake bila mafungo asingelifunga. Alifunga siku 40 kwa sababu ilikuwa muhimu. Huduma nyingi huzaliwa kipindi cha mafungo. Huduma ya mitume waliotengwa yaani, Barnaba na Sauli ilikuwa ni baada ya maombi na mafungo. Matendo ya Mitume 13:2
Jentezen Franklin katika kitabu chake cha: “Fasting” anakiri huduma yake ilizaliwa kipindi cha mafungo, Mchungaji Oyadepo na wengine wengi huelezea jinsi mafungo yalivyofungua njia katika wito wao na makusudi ya Mungu maishani mwao.
Ukiweza unaweza kukataa kula chochote kile kwa muda fulani. Pia katika kufunga unaweza kataa chakula cha nguvu yaani, wanga na ukashinda siku yako yote ukinywa maji tu au chai tu. Siku hizi nikifunga huwa nakunywa maji tu, hii huondoa maswali kwa wanaonizunguka kujua kwamba nimefunga au sikufunga. Usifunge na kujinyima vimiminika kiasi cha kukosa nguvu ya kuomba. Unaweza kunywa chai au juice pekee kwa saa 12 au 24 na hayo ni mafungo mazuri kwani nina hakika utakuwa na nguvu katika kuomba na kusali wala hutaomba kwa ulegevu.
Usichokijua nyuma ya mafanikio ya watu wengi wakuu ni yako mafungo na sadaka. Mafungo hufanya mwili na nafsi visielekee kwenye chakula na badala yake vimwelekee Mungu. Kuna jambo bado halijatimia katika huduma na wito wako nalo litahitaji mafungo. Ni muhimu kwa kukupa upenyo na kukufungulia yaliyofungwa.
Barikiwa