UNATUMIA KIUNGO GANI KUTAZAMA MBALI?

8:22:00 PM Unknown 0 Comments

 
UNATUMIA KIUNGO GANI KUTAZAMA MBALI?
Mwili wa binadamu unaviungo vingi kila kimoja kikiwa na kazi yake. Ipo pia milango ya fahamu ambayo kwa kuhisi, kunusa, kuonja na kwa kuona hufanya kazi. Viungo hivi na milango hii ya fahamu si tu kwamba ipo kwa binadamu bali hata wanyama, ndege na baadhi ya wadudu wamejaliwa na Mwenyezi kuwa nayo.
Binadamu ndiye mwenye jukumu la kuwatawala ndege, wanyama, wadudu na hata viumbe wasioonekana (mapepo, majini, malaika). Kitabu cha Waebrania kimeeleza malaika ni roho wanotuhudumia, pia mzaburi amenena wazi jinsi Mungu alivyomfanya mwanadamu punde tu kama yeye na amemvika utukufu na heshima.
Licha ya utukufu huo mwanadamu si kiumbe mwenye uwezo mkubwa wa kuona. Tai, mwewe na hata ndege wengine huona mbali zaidi kuliko mwanadamu. Ni watu wachache tu wenye macho makali ya kuona mita mia tano au zaidi.
Swali, Ni kwa nini macho ya wanadamu ambao kibiblia ndio watawala wa dunia hii yanazidiwa na hawa ndege? Jibu langu ni rahisi, Mungu hakutaka mwanadamu aishi kama tai, Hakutaka mwanadamu aone mbali kwa macho ya nyama bali atumie akili, fikra na imani katika kuona kwake. Kwa njia hizi ataona mbali zaidi ya tai na hivyo atamtawala mpaka tai.
Mwanadamu anauwezo wa kuona hata miaka 20 ijayo na akanunua shamba leo na kupanda miti. Mwanadamu wa leo anaweza kuona miaka 100 ijayo. Hayati Rais Kennedy wa Marekani anayetajwa katika simulizi za kwenda mwezini, aliwaita wanasayansi wake na kuwapa wazo hilo ambalo hawakuwa wamewahi kulisikia popote. Hebu waza unamka unaitwa na Rais na anakwambia, naomba uanze kufikria jinsi gani tutakwenda kwenye Mwezi au Jua. Wakati huo wewe hujawahi hata kuzifuatilia nyota za angani.
Baada ya wanasayansi hao kufanyia kazi wazo hilo kwa miaka kadhaa walifanikiwa na kwa sasa kwenda mwezini au kutuma vyombo kwenda huko si jambo la ajabu tena. Tofauti na hayati Rais Kennedy ambaye ni mtu wa fikra, Rev Martin Luther King Jr ambaye ni mwanaharakati, yeye katika harakati zake za kumkomboa mtu dhidi ya ubaguzi  wa rangi anaonekana kuona mbali kama nabii, na hii ni kwa sababu ya Imani yake ambayo mzizi wake ni neno la Mungu.
Alisema Fred Swaniker kwamba, Afrika inahitaji Moon shoot thinking, akimaanisha tunahitaji kufikiri mbali sana, tunahitaji kuruka kifikra (kimawazo) na kutua mbali, mahali ambapo kwa uhalisia macho ya kawaida hayapaoni ila kwa imani na fikra sahihi tunapaona.
Katika ulimwengu huu hata kipofu anaweza kufanikiwa kama ubongo wake umechangamka kuliko watu mia wenye macho makali lakini ubongo umelala. Kuna jambo linanishangaza katika taifa langu, vijana wengi ukiwahoji si watu wa fikra.
Siku 1000 za kwanza katika ukuaji wa mtoto zijulikanazo kama “mwanzo bora” zina mchango mkubwa katika uwezo wa kufikri wa mtoto. Utapia mlo ndio huzaa watu wenye mawazo mgando, na mawazo maji, yote ni matokeo ya mdororo wa chakula. Mfumo wetu wa elimu hauruhusu udadisi hasa kwa kuwa mwalimu ndio kila kitu, si rahisi mfumo wetu kuzalisha watu wanaofikiri kimkakati.
Ili tupate vijana wanaofikiri sawasawa basi ni muhimu tuwajenge kwa neno la Mungu ambalo litaleta imani, tuwape chakula bora cha akili yaani vitabu sahihi vya kiada na ziada, watoto wapewe mlo kamili ukijumuisha matunda, vyakula vya wanga, protini na maji mengi.

0 comments :

Kuelekea Uhuru wa Kifedha - II

2:33:00 PM Unknown 0 Comments

 
KUELEKEA UHURU WA KIFEDHA II
(THE BIBLICAL LAWS OF MONEY)
Toleo lililopita tuliangazia kanuni moja muhimu sana ili kuelekea mafanikio ya kiuchumi katika maisha ya mtu; kanuni ya uzalishaji bidhaa au huduma. Kanuni hii huwa haimzungumziwi sana lakini ni kanuni muhimu sana kuelekea uhuru wa kifedha. Kumbuka, Fedha unazozitafuta zipo kwa watu, ili kuzipata lazima uwe na kitu cha kubadillishana (exchange). Hakuna namna utafikia uhuru wa kifedha endapo hakuna bidhaa wala huduma ambayo unaweza kutoa na watu wakakupa fedha.
Kwa mtu ambaye ameajiriwa maana yake anauza huduma, na hivyo mwisho analipwa mshahara. Mshahara unakuja kama matokeo baada ya kutoa huduma, vivyo hivyo mfanyabiashara au mjasiriamali au hata makampuni hupata fedha kutokana na bidhaa au huduma wanayozalisha.  Fedha ni matokeo ya bidhaa au huduma anayotoa mtu. Mwalimu wangu mmoja amewahi kusema, “If you don’t create or add value to others (through goods or service), you are not entitled to receive money” (Kama hauna bidhaa au huduma unayoweza kutoa kwa watu, haustahili kupokea fedha ya mtu: Tafsiri isiyo rasmi)
Mtu pekee anayeweza kuwa na uhakika wa kupata fedha bila kubadilishana na huduma au bidhaa moja kwa moja ni serikali, yenyewe inakusanya kodi. Hivyo watu watake au wasitake ni lazima serikali ikusanye fedha kutoka kwao kama kodi kwa mujibu wa sheria za nchi husika. Mimi na wewe hatukusanyi kodi, watu hawalazimiki kisheria kutupa fedha zao; hivyo basi ili kupata fedha zao lazima tuwe na kitu wanachokiitaji na kwa sababu hiyo wako tayari kukilipia ili kukipata kitu hicho. Na hapo ndipo tunapoweza kuona fedha inaingia mifukoni mwetu.
Swali unaloweza kujiuliza au unalotakiwa kujiuliza sasa, ni bidhaa gani au huduma gani unaweza kuizalisha au kutoa ambayo watu (jamii inayokuzunguka) wanahaja nayo na watakuwa tayari kuilipia ili kuipata? Iwe umeajiriwa au hujaajiriwa hili ni swali muhimu sana kama unataka kufikia uhuru wa kifedha (kutimiza mahitaji yako YOTE, na kupata ziada kwa ajili ya kufikia mahitaji mengine yanayokuzunguka; maana utamsaidiaje anayehitaji ‘chakula’ wakati hata wewe huna: Mathayo 25:37-40).
Sam Adeyemi amewahi kusema  It is not the absence of money that makes a person poor; it’s the absence of right idea (thought) that has value”. Yaani “Si ukosefu wa fedha ndio humfanya mtu kuwa masikini bali ukosefu wa wazo lenye thamani”. Hivyo kumbe fedha ni matokeo tu; yaani matokeo  ya wazo lenye thamani ambalo huzaa bidhaa au huduma; ambazo mtu hubadilishana (exchange) na fedha.
There’s a place for you at the top!

0 comments :

Kuelekea Uhuru wa Kifedha

12:43:00 PM Unknown 0 Comments

 
KUELEKEA UHURU WA KIFEDHA
(THE BIBLICAL LAWS OF MONEY)
Tafiti mbalimbali zinaeleza kwamba, moja ya changamoto kubwa ulimwenguni hasa bara la Afrika ni umasikini mkubwa wa kipato. Ni ukweli unaosikitisha, na eneo hili ni moja ya maeneo ambayo hayana msisitizo mkubwa ndani ya mwili wa Kristo (kanisa). Eneo la maarifa kuhusu fedha au uchumi ili kumkomboa mtu kiuchumi ni kama limeachwa; Na kwa sehemu kubwa ukiona mahali fedha inatajwa kanisani au kikundi cha sala basi ujue ni sadaka inayozungumziwa. Ni watu wachache sana wanaozungumzia au kuhubiri au kufundisha maarifa kuhusu fedha na uchumi ili kumuwezesha mtu kupiga hatua katika eneo hilo kwenye maisha yake na jamii yake.
Jambo moja ambalo ni halisi na halikwepeki ni kwamba, ili kuishi katika ulimwengu huu wa sasa kila mtu anahitaji fedha za kutosha kumuweza kukidhi mahitaji yake na mahitaji ya wale wanaomzunguka. Kumbuka fedha haina dini, haijali kabila wala rangi yako; haiwezi kuja kwako kwa sababu wewe ni wa dini au dhehebu au rangi au kabila fulani (it is neutral). Na kwa sehemu kubwa, kiwango cha fedha au mafanikio ya kiuchumi ya mtu yanategemea kiwango cha maarifa na ufahamu sahihi alionao juu ya kanuni za fedha (The laws of money).
Nakumbuka siku moja wakati nipo sekondari niliwahi kuhudhuria kikundi cha sala mahali  fulani, na siku hiyo tukafundishwa kuwa ili kufanikiwa kifedha basi ni lazima tutoe sadaka ya kupanda ili makusudi tuvune mara mia kwa kigezo kwamba ukitoa utapokea mara mia ya ulichotoa (bila shaka unakumbuka hilo andiko). Na tena nikakumbuka lile andiko la kila apandacho mtu ndicho atakachovuna, basi nikapiga hesabu zangu pale, kwamba endapo nitatoa elfu moja basi nitarajie kupokea laki moja (bila shaka sijakuacha hata kama ulikimbia hesabu, elfu moja mara mia ni laki moja). Sijui kama unaelewa maana yake nini upo sekondari unatarajia kupokea laki moja ya kwako binafsi (hahahaha). Nikawaza tu nikiipata hiyo laki moja napanda elfu kumi, sasa piga hesabu hapo elfu kumi mara mia, mavuno ni kiasi gani? (tajiri mtoto anayechipukia).
Japo unaweza kucheka, inawezekana umewahi kuwaza hivyo pia. Kanuni moja muhimu sana kuhusu fedha ambayo huwa haifundishwi na leo nataka niigusie ni kanuni ya uzalishaji bidhaa au huduma (The law of production). Pamoja na kwamba sadaka na maombi ni muhimu sana kwa ustawi wa mtu; ni ukweli uliowaza kwamba hakuna aliyefanikiwa kiuchumi kwa mambo hayo TU (bila uzalishaji huduma na bidhaa) isipokuwa aliyepo upande wa kupokea.  Wazo kuu tunalotaka ulipate kwa siku ya leo ni kwamba, ukitaka kufanikiwa kiuchumi hauwezi kukwepa uzalishaji bidhaa au huduma kwa namna moja au nyingine.  Nioneshe anayeuza bidhaa au huduma, nikuoneshe mtu atakayefanikiwa kiuchumi. Zalisha huduma au bidhaa ambayo tunauhitaji nayo, na sisi tutakuwa tayari kukupa fedha kwa kuipata bidhaa/huduma hiyo kwa sababu tunaihitaji na hapo mafanikio ya kiuchumi yatakuwa dhahiri kwako.
Mungu ameahidi mvua ya Baraka, sio mvua ya fedha. Mungu ameahidi kushusha Baraka kwenye kazi ya mikono yako, kapu lako na chombo chako cha kukandia unga, mifugo yako, mazao shambani kwako, hakuna mahali ameahidi kushusha fedha toka juu. [Kumbukumbu la torati 28:4-5, 8]. Kusubiri mavuno ya sadaka uliyopanda tangu mwaka juzi ili utoke kwenye mkwamo wa kiuchumi uliona sasa, ni uvivu wa kufikiri, na ni kukosa uwajibikaji (irresponsibility).
There’s a place for you at the top!

0 comments :

USIWAPELEKE MAHALI USIPOWEZA KUWATOA

10:09:00 PM Unknown 0 Comments

 
USIWAPELEKE MAHALI USIPOWEZA KUWATOA
Hili ni jambo la msingi kwa kiongozi wa ngazi yoyote ile, haijalishi ni ngazi ya familia, kata, kampuni, taasisi binafsi au kiongozi wa siasa. Kuna maeneo ukiwafikisha watu au ukiwapeleka unaowaongoza hautaweza kuwatoa wote kwa usalama. Kiongozi lazima awe na kipimo cha madhara na uathirika unaoweza kujitokeza kabla ya kuchukua uamuzi wake.
Kwenye biblia kuna kisa cha Lutu aliyemuita Ibrahimu mjomba. Huyu baada ya kuipeleka familia yake katika miji ya Sodoma na Gomora alishindwa kuwatoa wote. Huko alimpoteza mkewe.  Alitamani waokoke familia nzima kama walivyoingia lakini hakuweza. Ingawa haijaandikwa lakini nina hakika Lutu alijisikia vibaya kumpleleka mkewe mahali asipoweza kumtoa. Sodoma ilikuwa ni uchaguzi wa Lutu nyakati za kutengana na Ibrahamu, haukuwa uchaguzi wa mkewe Lutu. Lakini mkewe Lutu akatazama nyuma yake, akawa nguzo ya chumvi.” Mwanzo 19:26
Rais Obama aliyekuwa kinara katika kuangusha Serikali ya hayati Rais Gadafi wa Libya alinukuliwa akijutia kushindwa kuijenga Libya mpya. Obama amewafikisha watu wa Libya mahali ambapo hawezi kuwatoa. Mpaka ameondoka hajaweza kujenga Libya mpya aliyoahidi na badala yake imekuwa pango la magaidi na wapiganaji.
Amesisitiza mwenye hekima mmoja kwamba, “In life you cannot undo every action” akimaanisha, “Katika maisha si kila kitu unaweza kukirejesha tena katika uhalisia wake.” Kuna akili zilizoharibika, kuna familia zilizoharibika, kuna vikundi vilivyoharibika; kuna jamii zilizoharibika, pia kuna kampuni zilizoharibika na si wote watakao weza kufanya urejesho. Kwa kuwa zoezi la urejesho ni gumu na zito basi ni busara kuepuka uovu, tabia hatarishi na mazingira yake. Huwezi kuepuka moshi ikiwa unapika kwa kuni, kwa hiyo katika kubadilisha mwenendo huwezi kupuuza mchango wa mazingira yako. Mazingira hatarishi ya Sodoma na Gomora ndio chanzo cha uharibifu wa mke wa Lutu.
Kama baba wa familia au kiongozi (Lutu) ni lazima uogope maamuzi au maeneo ambayo huna uhakika kwamba, wale unaowaongoza watatoka salama. Yuko rafiki anayeweza kukufundisha tabia mbaya ambayo huwezi kuiacha, yako makundi mabaya ambayo yanaweza kukufundisha tabia hatarishi ambazo huwezi kuzikomesha. Je, unamkumbuka uathirika uliingia lini maishani mwako? Ulevi, ubwiaji wa unga na dawa za kulevya, utazamaji wa picha chafu na uasherati? Ni baada ya kujisamehe sisi wenyewe ndipo tunapoweza kumsogelea Yesu mwanamapinduzi ili atusamehe na kutupa upya.
Watu wengi wamekuwa wanamwogopa Yesu kwa kuwa ni mwanamapinduzi na wanajua wakimsogelea atapindua tabia zao na atapanda tabia njema. Mwanamke Msamaria aliyekutana na Yesu kwenye kisima cha Yakobo alikuwa na uathirika. Alikuwa amekuwa na wanaume watano, that was an addiction! Na kwa muda ule mfupi Yesu alipindua maisha yake.
Muda, afya njema, ufahamu, malezi ya watoto, umoja na mshikamano ni moja ya mambo ya kulinda sana kwa kuwa hayarejeshiki kirahisi na pengine hayarejesheki kabisa baada ya kuharibiwa.
Jilinde!

0 comments :

Utimilifu wa kusudi lako......

8:25:00 PM Unknown 0 Comments

 
UTIMILIFU WA KUSUDI LAKO UTAHITAJI MAFUNGO
Ni kwa zaidi ya miaka mitatu sasa Programu yetu (Life Minus Regret) imekuwa kazini katika kuwasaidia watu kujua makusudi ya kuumbwa kwao na kuyaishi. Tumekuwa tukiwahamasisha vijana wamjue Mungu ili naye awaambie wao (vijana) ni akina nani. Ni Mungu aliyemwambia Yeremia, “nimekuweka uwe nabii wa mataifa” ni Yesu aliyemwambia Petro, “lisha kondoo zangu”, na baadaye akamwambia tena, “chunga kondoo zangu.” Hawa wote walipata kuambiwa kazi zao na wito wao kwa sababu walitafuta kumjua Mungu na kuhusiana naye.
Mambo matatu ni muhimu katika kuhusiana na Mungu; kusali, kufunga na kutoa sadaka. Yesu akasema “nanyi msalipo…,” maana yake anategemea tutakuwa tunasali mara kwa mara, tena akasema, “nanyi mfungapo….” Pia akihimiza “nanyi mtoapo sadaka…” Haya matatu aliyafundisha kwa kuwa yote ni muhimu kufanyika mara kwa mara ili kumkamilisha mtu. Mathayo 5:2, 5, 6 na 16
Sala, sadaka na mafungo ni vitu muhimu katika kuhusiana na Mungu. Katika eneo la sala na sadaka wengi wanajitahidi, changamoto iko katika eneo la ushindi na mafanikio ambalo ni eneo la kufunga. Wengi hupanga kufunga na kabla siku haijafika hughairi na kufakamia chakula. Shetani hatoi ruhusa katika hili kwani anajua lina baraka, tena halijali idadi.
Mafungo ni muhimu kwa ajili ya huduma yako na kusudi lako. Kama Yesu angeweza kutimiza kusudi lake bila mafungo asingelifunga. Alifunga siku 40 kwa sababu ilikuwa muhimu. Huduma nyingi huzaliwa kipindi cha mafungo. Huduma ya mitume waliotengwa yaani, Barnaba na Sauli ilikuwa ni baada ya maombi na mafungo. Matendo ya Mitume 13:2
Jentezen Franklin katika kitabu chake cha: “Fasting” anakiri huduma yake ilizaliwa kipindi cha mafungo, Mchungaji Oyadepo na wengine wengi huelezea jinsi mafungo yalivyofungua njia katika wito wao na makusudi ya Mungu maishani mwao.
Ukiweza unaweza kukataa kula chochote kile kwa muda fulani. Pia katika kufunga unaweza kataa chakula cha nguvu yaani, wanga na ukashinda siku yako yote ukinywa maji tu au chai tu. Siku hizi nikifunga huwa nakunywa maji tu, hii huondoa maswali kwa wanaonizunguka kujua kwamba nimefunga au sikufunga. Usifunge na kujinyima vimiminika kiasi cha kukosa nguvu ya kuomba. Unaweza kunywa chai au juice pekee kwa saa 12 au 24 na hayo ni mafungo mazuri kwani nina hakika utakuwa na nguvu katika kuomba na kusali wala hutaomba kwa ulegevu.
Usichokijua nyuma ya mafanikio ya watu wengi wakuu ni yako mafungo na sadaka. Mafungo hufanya mwili na nafsi visielekee kwenye chakula na badala yake vimwelekee Mungu. Kuna jambo bado halijatimia katika huduma na wito wako nalo litahitaji mafungo. Ni muhimu kwa kukupa upenyo na kukufungulia yaliyofungwa.
Barikiwa

0 comments :

Furahia Maisha Yako

11:09:00 AM Unknown 0 Comments

 
FURAHIA MAISHA YAKO!!
Mungu ametuumba si tu kwa ajili ya ibada na kazi, bali hata kwa ajili ya kufurahia maisha haya. Kutembelea fukwe, kula vizuri, kusafiri, kushiriki matukio ya furaha na pengine hata kuwa na mitoko ya hapa na pale kwa wale wapendanao. Alisema Ratan Tata yule mmiliki wa kiwanda cha kutengeneza magari ya TATA, “Hakuna faida yoyote ikiwa utapanda cheo siku ambayo mnatengana na mpenzi wako…maisha hayahitaji uwe shupavu na makini kiasi hicho” alimaanisha mafanikio ya kazini yaende sambamba na furaha ya nyumbani, tukichukulia maisha kuwa magumu sana kila siku itakuwa ni mapambano bila ya pumziko.
Biblia inaweka wazi katika kitabu cha Mhubiri 3:13, “tena ni karama ya Mungu kila mtu apate kula na kunywa, na kujiburudisha kwa mema katika kazi yake yote.” Napenda mstari ulivyotafisiriwa kwa lugha nyingine, “It is a gift of God to enjoy the good of all his labor”.
Mungu anapenda kila mtu apate muda wa kufurahia matokeo ya kazi zake. Baada ya kazi nzito ni furaha, partying and enjoying!!! Hatuna maana kwamba mioyo yetu izame katika anasa la hasha! Bali kuwe na muda wa kupumzika na kufurahia maisha ambayo ni zawadi kutoka kwa Mungu.
Maneno ya Reba Mc Entire huwa ni ya kuchekesha lakini yana maana alisema, “to succeed in life you just need a wishbone, backbone and a funny bone”. Ni kweli kabisa kila siku ni lazima tuwe na msingi wa kutumaini na kutamani yajayo lakini ni lazima ucheshi na furaha viwe kama uti wa mgongo wa mafanikio yetu.
Namna rahisi ya kufurahia haya maisha ni kuwa sababu ya wengine kufurahi. Katika mchakato wa kufanya watoto, majirani, mke, mume, binti wa kazi, au mfanyakazi mwenzio afurahi utajikuta wewe mwenyewe unafurahi. Furaha inatabia ya kurudi kwenye chanzo chake, hakikisha unakuwa chanzo cha furaha.
Maisha haya si marefu kiasi kwamba tukumbatie huzuni, ukiishi miaka 50 unamapumziko ya Jumamosi na Jumapili 2500 tu na inawezekana zimeshapungua, kama una mika 25 umeshatumia nusu ya majuma hayo. Jipange.
Enjoy…………
Kwa makala nyingine nyingi kama hizi tembelea; www.lifeminusregeret.blogspot.com

0 comments :

Uvivu na Uuaji

2:30:00 PM Unknown 0 Comments

UVIVU NA UUAJI.
Maneno haya mawili si rahisi kuyatenganisha, ni kama chanda na pete. Uvivu una hasara kubwa sana na matokea yake ni uuaji. Utaua karama yako au kipaji chako, utaua mtaji na pengine utapoteza yale ambayo wengine waliyasumbukia kwa muda mrefu na walikupatia wewe uyaendeleze.
Uvivu haufanyi tu ukose yale unayoyatamani kuyapata bali unakupokonya hata lile dogo ulilonalo tayari. Muuzaji hodari atachukua wateja wa yule dhaifu na mvivu katika biashara. Kile usichokitunza huondoka na hii ni kanuni wazi. Kile usichokilinda kitaibwa hii haipingiki, ndio maana ikananenwa shika sana ulichonacho.
Nyakati za mfalme Sulemani katika maandiko, yuko mama aliyemlalia mtoto wake na kumuua kisha kugombea mtoto wa mwenzake. Alilala wakati wanawake wenzake hupumzika tu maana wanajua mtoto ni muhimu kwao kwa saa 24. Ni uzembe wa hali ya juu kusinzia hadi kuua mtoto uliyemsumbukia kwa muda mrefu (1Wafalme3:19). Inawezekana wewe na mimi tukiendelea kulala kuna vitu vitakufa. Rafiki yangu mmoja aliwahi kuniambia, “Alphonce, vijana hatulali tunapumzika tu” Ukipenda usingizi utaua ndoto zako na hatma yako.
Siku nyingine nikajifunza kuachana na neno sana. Nakushauri pia uondoe neno “sana” katika misamiati yako. Nimechoka sana, nimesoma sana, nimetembea sana ni sentensi zenye kuhalalishi na kutoa udhuru wa kutofanya kitu kinachotakiwa au cha ziada. Hii ni dalili ya uvivu, neno sana lazima liondoke. Aliyechoka sana atatamani kulala sana lakini aliyechoka atatamani kupumzika na kurejea tena ulingoni. “So avoid using the word ‘very’ because it’s lazy
Mwingine anaweza kuwaza, Uvivu ni nini? Ni ile hali ya kughairisha mambo. Nitafanya jioni, nitafanya kesho na hatimaye nitafanya mwakani. Uvivu pia ni hali ya kushindwa kuzingatia jambo moja, ni kuitawanya akili katika mambo mengi ambayo pengine si ya msingi. Uvivu pia ni ule uoga unakuja wakati wa kupanga mipango mikubwa na migumu na hivyo mtu kwa kujihurumia anajipangia mipango midogo na ya kawaida sana. Mvivu anakubali huondoka mapema hata kama kazi haijaisha, kamwe hapambani mpaka mwisho.  Kwa hiyo uvivu ni ile hali ya kuishia njiani.
Inawezekana umepoteza fursa nyingi na sasa huna cha kushika. Lile neno shika sana ulichonacho halina tena nguvu kwako maana huna cha kushika. Usiogope, Yesu Kristo aliye ufufuo na uzima na kweli anaouwezo wa kufufua yaliyokufa. Yeye alimwita Lazaro aliyekufa na akatoka mzima. Kwake huyu Mungu mwenye nguvu, na Mfalme wa ajabu twaweza kuomba, Ee Bwana fufua kazi zako ndani yetu.
Amka sasa uangaze….


0 comments :

Wapi niende kujenga fikra mpya

3:06:00 PM Unknown 0 Comments

WAPI NIENDE KUJENGA FIKRA MPYA
Renew your Thinking
Kwa wiki mbili mfululizo tumekuwa tukiandika kuhusu Fikra. Wapi uende, nini ufanye na kwa nini kubadilisha mfumo wa kufikiri. Kesho yetu haitaweza kubadilika kama bado fikra zetu zinafanana na jana.
Tunavaa mavazi tuliyoyawaza jana usiku, tunaenda mahali tulipowaza kabla ya kwenda. Usipobadili mfumo wa kufikiri huwezi kubadili mwenendo wa maisha. Kwanza, ni muhimu kuwa walau na dakika kumi kila siku jioni au asubuhi kwa ajili ya kukaa kimya na kufikiri. Ni muhimu kila siku upate muda wa upekee na ukimya (shut from the world) ili uweze kujitathmini na kufikiri kwa upana.
Fikra ni chakula inategemea unakula wapi. Ukila picha za ngono utakuwa mjinga, ukila udaku utakuwa na mambo yakufanana na udaku, ukila majarida ya matangazo ya pombe utakuwa mtumwa wa pombe.
Twende kwenye jambo safi, tujifunze kwenye kitabu kizuri, channel safi ya Luninga, kikundi cha busara cha WhatsApp. Usione haya kutoka kwenye kundi ambalo halina maadili. Usiogope kuchana na kuchome picha na majarida yenye kuharibu akili. Mambo ya uasherati na ulevi huharibu akili.
Imenenwa, “aziniye na mwanamke hana akili kabisa” tena ikanenwa, “mambo ya ulevi huharibu ufahamu” mambo haya huharibu ufahamu na kufanya uwezo wa mwanadamu wa kuamua na kufikri kupungua.
Hatupaswi kutafakari kila jambo, bali yale tu tuliyojifunza na kuyaona yanafaa kwa kutafakari. Ushindi wote wa mwandamu uko katika tafakari. Mungu alimwambia Joshua atafakari neno lake mchana na usiku na azungumze hilo neno kila siku. Kwa kufanya hivyo ushindi ulidhihirika katika maisha ya Joshua mwana wa Nuni. Joshua 1:8
Dunia inataka watu wajanja. Lakini maandiko yanataka kabla hatujawa wajanja tuwe watu safi, wasio na waa lolote mbele za Mungu. Daniel ni mmoja wa watu safi, alionekana na akili mara kumi kuliko waganga na wachawi. Mtume Paulo amesisitiza nini tufikiri kama tunataka kuwa wajanja na safi (pure and smart in all our way) “Mambo mliyojifunza kwangu na kuyapokea, na kuyasikia na kuyaona kwangu, yatendeni hayo; na Mungu wa amani atakuwa pamoja nanyi.” Flp 4:9
Mazoezi ya kutenga muda wa kufikiri, kujizoeza kusoma neno la Mungu na kuacha makundi mabaya kutabadilisha kabisa namna yako ya kufikiri. Barikiwa.

0 comments :

Kama si Kompyuta Basi ni Roboti

9:56:00 PM Unknown 0 Comments

 
KAMA SI KOMPYUTA BASI NI ROBOTI
(Tumia akili yako kufikiri vema)
Dunia iko kwenye kasi kubwa ya mabadiliko ya sayansi na teknolojia. Mabadiliko haya ni muhimu sana, nchi ambazo ziko mbele katika mabadiliko haya watu wake huishi maisha marefu. Si ajabu kwa Japan, Korea kusini na Kaskazini raia wake kuwa na wastani wa umri mrefu wa kuishi. Mabadiliko haya humpa mwanadamu muda wa kupumzika kwa kuwa humwondoa kwenye majukumu ya kutumia nguvu na kumwachia jukumu zito la kufikiri. Sayansi na teknolojia ni muhimu katika afya ya binadamu, usindikaji na ujenzi wa miundombinu.
Kazi kubwa ambayo mwanadamu anapaswa kubaki nayo ni kufikiri. Mabadiliko na mapinduzi hayawezi kutokea ikiwa hatukupindua sehemu iliyoko katikati ya sikio la kulia na sikio la kushoto yaani, ubongo. Kazi za mazoea kama vile kubeba mizigo, kubaki mizigo, kuandika hati, kusikiliza na nyinginezo zifananazo na hizi zinaweza kufanywa vizuri kama sina kompyuta basi ni roboti.
Hivi karibuni Japan wamezindua roboti ambaye huangalia watoto nyakati za usiku. Bila shaka roboti huyu akifika Afrika atanyang’anya kazi za watu wengi katika shule na maeneo ya malezi ya watoto. Kupitia masomo ya walimu wabobezi yaliyoko mitandaoni, “you tube” na katika maeneo mengine ya kuhifadhia itafika mahali hatutahitaji tena kukutana na mwalimu ana kwa ana. Mungu alitaka tuishi kwa kufikiri, tutumie utashi wetu. Kufikiri hakupitwi na wakati, mwenye fikra njema anaweza kushinda kipimo cha muda (time test).
Tabia za mazoea na kazi za mazoea ni rahisi kufanya kwa kutumia teknolojia pasipo kumhitaji mtu awaye yote. Tabia hizi za mazoea huua ubunifu na uwezo wetu wa kufikiri. Wastaafu wengi wanaotoka kwenye kazi zisizosumbua ubongo hushindwa kumudu maisha mapya ambayo huhitaji fikra mpya na mawazo mkakati. Fedha yao ya kustaafu huwa kama magurudumu mapya katika injini iliyoharibika kabisa. Ni wazi Teknolojia inawafukuza watu wengi kazini kuliko tumbua tumbua ya vyeti feki. Uzuri wake ni kwamba inarahisisha utendaji na ina ajiri watu wengi zaidi wanaoifahamu zaidi ya wale inaowafukuza.
Ni muhimu tuusukume ubongo na ufahamu wetu ili tupate mawazo na fikra endelevu za kutuwezesha kwenda sambamba na sayansi na teknolojia. Ni muhimu kukumbatia teknohama kuliko shahada za vyuo vikuu. Nchi za wenzetu zinapunguza udahiri vyuo na zinahimiza ufundi ili tu zikuze ujuzi na matumizi ya sayansi na teknolojia katika maisha ya kila siku.
Ile kwamba, mtakula kwa jasho haikuzuii kufunga kiyoyozi na kula kwa damu ya Yesu iliyovunja laana zote. Jasho ni matokeo ya ugumu wa kazi ni muhimu fikra zetu zituletee njia rahisi, zenye kugharimu muda mchache, rasilimali chache na ubora wa juu. Tukutane katika msimu mpya wa Weekend of Purpose. Barikiwa!!  

0 comments :

Mungu Hahitaji Kufikiri

11:50:00 AM Unknown 0 Comments

 
MUNGU HAHITAJI KUFIKIRI
MIMI NA WEWE TUNAPASWA KUFIKIRI
Mungu mwenyezi anazo sifa nyingi, ni Mungu aliyeumba majira na nyakati, nchi na vyote viijazavyo ni kazi ya mikono yake na ni mali yake. Hakuna historia wala yajayo ambayo yamefichika machoni pake. Anayejua mambo yote ya sasa, yajayo na yaliyopita. Ni Mungu wa nyakati zote, za sasa na zijazo. Mbele yake hakuna siri. Ndio maana imeandikwa, “maana naijua mipango niliyonayo kuwahusu ninyi, asema BWANA, ni mipango mizuri si mibaya” (Tafsiri yangu kutoka Yeremia 29:11)
Mwanadamu anahitaji kufikiri ili kuleta majibu kwenye changamoto inayomkabiri au inayokikabiri kizazi chake. Kunapokuwa na namna tatu, mwanadamu anahitaji kufikiri ili kupata namna moja ambayo ni bora zaidi. Kunapokuwa na njia tatu, mwanadamu anahitaji kufikiri ili kupata njia moja ambayo itampendeza Mungu, haitaharibu mazingira wala hamtamdhuru jirani yake. Baada ya kufanikiwa kupiga hatua kubwa kwenye mambo teknohama dunia sasa inahitaji kufikiri kuhusu usalama wa mazingira, hali ya joto Duniani na usalama wa vizazi vijavyo.
Fikra sahihi zinatupa nafasi ya kufanya maandalizi ya mambo yajayo. Usipofikiri kuhusu yajayo yatakapokuja yatakukuta huna maandalizi yoyote, kwa hiyo hautaweza kusimama katika nyakati hizo. Kwa mtu makini hakuna nyakati za furaha kama nyakati za mwisho ambazo tumezoea kuziita, “future
Tabia za mazoea huua uwezo wa kufikiri. Kuna mambo ambayo hujulikana na yamezoeleka haya hayadai fikra mpya katika utekelezaji wake. Wale wanafunzi ambao huamka, hula chakula, huenda darasani, kisha kuoga na kulala huwa hawana jipya maana hurudia matendo hayo kila siku. Wale ambao huamka, hufanya sala, kisha zoezi, kisha usafi, kisha masomo, kisha kuimba kwaya, kisha siasa za shuleni, kisha uongozi wa shule huwa watu bora zaidi kuliko wale wenye mambo machache na madogo kama sisimizi.
Kizazi cha sasa kinahitaji mageuzi makubwa kifikra, walio wengi wanalipwa kwa sababu ya muda wanaotumia kazini. Hawalipwi kwa sababu ya matokeo, wala kwa sababu ya akili bali wanalipwa kwa sababu ya mahudhurio yaani, muda fulani mpaka muda fulani. Tunahitaji kuhama, Shift from being paid for your time to being paid for your mind!
Akili inachuja na kuchekecha, inapima na inatoa majibu. Akili inakupa uwezo wa kufika mahali kimawazo  ambapo miguu yako haijawahi kupakanyaga kimwili. Biblia iliposema, “ uishi na mwanamke kwa akili” ilitaka ujue kwamba, hauna taarifa za kutosha kumuhusu kwa maana wewe si Mungu wake, ilitaka ufike mahali kimawazo ikiwezekana kabla yeye hajafikia maana akikutangulia kufika inawezekana usimwelewe, ilikutaka ujizoeze kufikiri, kuchambua, na kupima matakwa yake na mazingira yake. Kwa kufikiri unaweza kupambanua kati uongo na ukweli.
Kwa uzoefu wangu mdogo vijana wale walikuwa na ufinyu wa fikra miaka ile tulipokuwa shuleni hata sasa mtaani utawakuta na kibano cha fikra na mara nyingi hawa watu ni watiifu sana kwa historia, dini za mababu na ni wapesi kurithi mila na desturi zilizopo, wala hawajisumbui kuzikosoa pale zinapopwaya, mara nyingi watu hawa hupenda sana kusifia watawala, they cannot challenge the conventional knowledge!
Kwa nini tunahitaji kufikiri? Katikaa kitabu cha, “Teach your Child How to Think” mwandishi Edward de Bono ameeleza wazi, “Tunahitaji kufikiri kwa sababu hatuna taarifa za uhakika kuhusu mambo ya baadaye, tukiwa na taarifa kamili na mambo yote yakiwa wazi na utupu mbele yetu hatutakuwa na haja ya kufikiri maana kila kitu kitakuwa wazi”. Hii ndio sababu imenifanya niamini Mungu hahitaji kufikiri, hawezi kujiuliza itakuwaje ilhali anajua kila kitu.
Karibu katika, Weekend of Purpose ya April, 2018 na tuandikie katika email na blog yetu.
Bwana Mungu Akubariki,

0 comments :

Ongeza maarifa katika eneo maalum

5:37:00 PM Unknown 0 Comments

ONGEZA MAARIFA KATIKA ENEO MAALUMU
Kama ilivyo kawaida, mwanzoni mwa mwaka kila mtu anaweka malengo yake au mambo anayotaka afanikiwe au afanikishe katika kipindi cha mwaka huo. Pamoja na kwamba si kila mtu ana utaratibu wa kuandika malengo yake ya mwaka, lakini karibu kila mtu huwa na malengo au mambo analiyopanga kufanikisha katika mwaka.  Nafahamu baadhi yetu tumeweka malengo ya kusoma vitabu katika mwaka huu mpya (kama hujaweka lengo la kusoma vitabu, basi hujachelewa kufanya hivyo), hili ni jambo jema kwa kila mwenye uwezo wa kusoma.
Pamoja na mipango na malengo yako mengi uliyojiwekea kwa mwaka huu mpya, leo nataka nikupe hamasa juu ya jambo moja, nalo ni kuweka nia au malengo ya kuongeza maarifa/ujuzi na ufahamu katika eneo mahususi au maalumu katika maisha yako. Yaani badala ya kuweka lengo la kusoma tu, weka pia ni eneo gani unalotaka kuongeza ujuzi au maarifa ili kuliboresha.
Mwenyehekima mmoja amewahi kusema "Usishibishe njaa yako, shibisha maono yako [don’t feed your hunger, feed your vision]"; huu ni ushauri mmoja wa hekima ambao nimewahi kuupata kuhusu usomaji katika kuishi kwangu. Lengo hapa ni kukuepusha na tabia ya kusoma kila kinachokuja mbele yako bila malengo mahususi wala mpangilio utakao kusaidia kupiga hatua zaidi katika maisha ya kila siku. Mtu anaweza kupanga mwaka huu nataka nisome vitabu 30 au 20, lakini ukimuuliza unataka kusoma kuhusu nini au kuhusu eneo gani, ni wachache sana wanamajibu yanayoeleweka (concrete answer)
Ili kusoma kwetu kulete badiliko katika maisha yetu na mazingira tuliyopo ni muhimu ukachagua cha kusoma ukilenga kuboresha eneo mahususi katika maisha yako. Na hapa utapata fursa ya kufanya tathmini kuona kama unasogea, na kama kusoma kwako kuna kuletea faida inayoweza kupimwa [measurable results].
Kumbuka, huwezi kusoma vitabu vyote vilivyoandikwa, hivyo basi lazima ujue nini cha kusoma na nini cha kuacha hata kama kina sura nzuri, ili mwisho wa mwaka useme kwa kusoma vitabu au kwa kujifunza ujuzi fulani nimepiga hatua hii; kiuchumi, kiroho, mahusiano, ufanisi kazi, huduma, ubora wa kazi zangu n.k
There’s a place for you at the Top

0 comments :

Roho ya Batromayo Kipofu

10:25:00 PM Unknown 0 Comments

 
ROHO YA BATROMAYO KIPOFU
“ONA FURSA”
Batromayo aliona watu kama miti. Watu wengi wanasumbuliwa na roho hii hawaoni picha halisi, picha yao haijatulia. Ni kama vile ungo wao wa kudakia mawimbi haujatulia, hawapati picha halisi. Ni muhimu sana mwaka huu 2018 sote tumuombe Mungu afungue macho yetu tuweze kuona fursa!
Kwa uzoefu mdogo nathubutu kusema, “fursa haziwezekani bila imani”. Macho ya mwili hayotoshi, ile kwamba macho yetu yanaona taa za barabarani na tunavuka salama haina maana kama tunaona fursa pembezoni mwa barabara. Mtu anayeweza kufikiri kimkakati “strategic thinking” anaweza kuona fursa na kuzitumia. Kufikiri kimkakati kutakuwezesha uone miaka kumi ijayo na zaidi.
Kwa kukosa imani watu hauza mambo ambayo baadaye yangekuwa fursa kubwa, kwa uhaba wa imani watu huogopa kuanza jambo ambalo halijazoeleka. Anayewekeza miaka mia moja ijayo anaamini kwamba, Mungu atamlinda na kumpa uhai, ndani yake mtu huyo hamna hofu ya kifo. Fursa inataka imani katika sura tatu, kwanza mwamini Mungu muumba wako, jiamini na kisha amini wazo lako.  Adui mkubwa wa fursa ni hofu, uwekezaji unakwenda na ujasiri.
Zamani walituambia, “wasiwasi ndio akili” si kweli. Nenda msituni utagundua mnyama mfalme wa msitu ni simba ambaye ni mnyama jasiri. Njoo duniani utagundua mataifa makubwa yana ujasiri mkubwa pia. Alisema msemaji wa Marekani wa mambo ya nje wakati huo John carry, “Dola ya Washington haitatikisika” alisema hayo kwa ujasiri sana akionya taifa moja alilolitazama kama adui. Hatuna sababu ya kuogopa amesisitiza Shiv Khera katika kitabu cha, Unaweza Kushinda: “Losers want security, winners seek opportunity. Losers more afraid of life than death…”.
Tunawezaje kuona fursa? Maana kama hatukuijua fursa kabla ya kukutana nayo, siku ikitokea tutaiona kama mkosi. Lazima ujifunze kuhusu fursa na uzifahamu ili siku ukikutana nayo uitambue kirahisi. Wewe si tajiri ila jitahidi usome kuhusu utajiri. Leo wewe si mfanya biashara lakini jitahidi kusoma na kujifunza kuhusu biashara. Soma wasifu wa wafanya biashara kama; Mohamed Dewji, Warren Buffet, Reginard Mengi, Ratan Naval Tata, Alhaji Dangote, Said Bakhresa na wengine wenye ushawishi kwako.
Watu wengi wanapenda kushinda ila ni wachache tu ambao wanapenda maandalizi kwa ajili ya kushinda. Fursa zinakutaka ufanye maandalizi. Wewe ndiye unapaswa kuisubiri fursa kwani fursa haina nafasi ya kumsubiri mtu! Fursa huja kwa waliojiandaa. Preparation is the Key!
Sala: Ee Mungu Baba Muumbaji wetu, utufungue macho ili mwaka huu 2018 sote kwa umoja wetu tuweze kuona fursa. Katika Jina la Yesu Nimeomba. Amina.
Usisite kutuandikia kwa anuani yetu kwa maoni, ushauri na maombi. Barikiwa!

0 comments :

Biblia ina majibu yote

2:07:00 PM Unknown 0 Comments

BIBLIA INAMAJIBU YOTE
ISOME!
Ni mwaka mpya sasa nuia idadi ya vitabu unavyopaswa kusoma mwaka 2018, zaidi ya yote usisahau mpango wa kusoma Biblia, yearly bible reading plan! Tatizo la kutokusoma linaendelea kuwatesa watu wa leo, kizazi hiki hakijajijengea tabia ya kujisomea. Majibu mengi ya matatizo yetu yanayotukumba katika maisha ya kila siku yako katika vitabu, bahati mbaya hatusomi.
Hivi karibuni nikiwa naelekea Bagamoyo kwenye daladala nilifarijika baada ya mtoto wa miaka kumi kuingia ndani ya gari na kisha kutoa kitabu na baada ya mwendo kidogo akaanza kusoma. Nilitamani kupiga naye picha (selfie) kwa furaha, kuona utamaduni ninao upenda umejengeka kwa mtoto yule. Miji na majiji yenye foleni hutoa fursa kwa watu kujisomea wakiwa barabarani. Nyumbani utasema watoto wasumbufu barabarani je? Furaha tunayoikosa vijiweni iko kitabuni, nguvu tunayoikosa pahala pa kazi iko vitabuni, knowledge is power!! Mwenye maarifa mengi ni mwenye nguvu nyingi hili halipingiki. Kile ambacho baba yangu hakusema vitabu vimeniambia, kile ambacho dini ilinificha vitabu vimeniweka bayana. What a royal friend!
Nakushauri usome vitabu, lakini soma zaidi Biblia. Katika neno la Mungu kuna umilele wote. Yesu akasema, “ninyi mmekuwa safi kwa sababu ya lile neno mliliosikia”. Lile neno la Mungu unalosikia linafanya unakuwa safi mwili na roho.
Neno la Mungu limebeba majibu ya hali unazopitia wewe binafsi na Taifa lako pia. Unapotazama uchumi wako na hali ya taifa lako usiende tu kwa kutumia elimu ya uchumi ya darasani, ni muhimu utazame kiroho pia. Ukiona hali ngumu ya uchumi kwenye nchi jiulize Mungu anataka nini kwa taifa lako, inawezekana kabisa anataka toba. Badala ya kwenda kuchukua shahada ya uzamili ya uchumi mara nyingine ni muhimu kusoma Biblia mfululuzo. Daniel kwa kusoma maandiko (neno la Mungu) aligundua nini kinaendelea kwenye taifa lake.
Jifunze kujua chanzo, anayejua chanzo halalamiki sana. Taifa linapopewa mtawala mkorofi ni lazima ujue kuna mahali dhambi ilitendeka katika Taifa hilo na Mungu amemweka mtawala huyo kwa makusudi yake ili watu wake watubu na kurejea. Katika hali kama hiyo kufanya kazi kwa bidii hakutasaidia ila toba ya kweli kwa wateule wote wa Mungu walioko kwenye taifa hilo inaweza kuleta suluhisho.
Moja ya njia kuu ambayo Mungu amekuwa akiitumia kuzungumza na nchi na watu binafsi ni hali ya uchumi. Ukiaona kuna mvua ya kutosha, tena kwa wakati wake ni lazima ujue kuna kitu kizuri Mungu anazungumza, ukiona ukame na watu wanakufa kwa njaa ujue kuna kitu Mungu anadai au ibada ya sanamu imekithiri, ukiona watu wengi wanakimbia nchi ujue kuna laana ya ukiwa.
Katika kila jambo lihusulo hali ya hewa, mahali pa kuishi, hali ya uchumi ni muhimu utafute makusudi ya Mungu katika Biblia. Mambo haya yote ndani yake kuna makusudi ya Mungu, ukiyatafute ndani ya neno la Mungu utayajua! Jipatie ufahamu uyajue yanayokuhusu na yanayohusu nchi yako kwa kusoma maandiko. Barikiwa.

0 comments :

Bwana alipoamuru baraka

10:22:00 PM Unknown 0 Comments

 
BWANA ALIPOAMURU BARAKA
MUDA MWAFAKA ENEO MWAFAKA. 
Katika mambo ambayo Mungu hata subiri ufanye maandalizi ni hukumu na fursa. Kila siku unapaswa kuwa tayari, katika eneo husika, mwenye maandalizi kamili, ndio maana ya lile neno kesheni. Si kila eneo, si kila Mkoa, si kila medani wala si kila nchi itakuwa na Baraka zako; liko eneo moja, iko aina ya biashara fulani, uko mkoa na pahala ambapo Mungu ameamuru baraka zako zipatikane. Wakati mwingine tunachagua miji kwa macho ya nyama na hivyo tunavyokwenda ndani yake hatufanikiwi sana. Si kila aliyeko Ulaya anamafanikio, kuna wengine wako huko na wanaomba chakula, hawana uhakika wa kupata milo mitatu.
Kuna watu ambao walikuwa jijini Dar es salaam ilhali baraka yao ilikuwa Dodoma. Kwa vyovyote vile haikuwa rahisi kuwapeleka watu hao Dodoma inawezekana walifikiri hakuna maisha bora nje ya jiji la Dar es salaam. Lakini Mungu kwa kutumia Tangazo la Serikali la kuhamia Dodoma amewawezesha pia maelfu ya watanzania kwenda kwenye baraka yao iliyoamriwa mjini Dodoma. Tangu nyakati za Yesu Kristo mpaka sasa matangazo mengi ya Serikali yamekuwa yakibeba makusudi ya Mungu ya amani. Amani maana yake uchumi mzuri, Baraka na mafanikio. Yanaweza matangazo hayo yakaonekana magumu na mabaya yenye kubeba usumbufu lakini baadaye Mungu hujitwalia utukufu na watu wake hustawi.
Ukihamishwa kwa Tangazo la Serikali usigome, Matangazo hayo hubeba baraka.  Katika saa yako ya kusimama kiuchumi na kiutumishi tangazo hilo halitaweza kukudhuru hata kama lilitolewa ili kukuangamiza wewe. Tangazo la Herode la kuua watoto wote chini ya miaka miwili halikuweza kumua Yesu maana ilikuwa ni wakati wa Yesu kung’aa na kuokoa, halikuweza kumzuia.
Si miji peke yake, hata changamoto nyingine za maisha zenye ukakasi  ndani yake kuna baraka pia. Wako watu ambao bila talaka wasingelipata wokovu, bila kuachwa wasingelijua kusimama wenyewe, wako wale ambao bila kufeli masomo wasingeli jaribu biashara ambazo leo zimewapandisha na kuwafanya wakuu.
Baraka hizo zisingepatikana ikiwa kila kitu kingekuwa shwari, mara nyingi inapokuwa ni shwari watu hujisahau sana na kufanya yasiyo ya msingi. Biblia inasema, “Katika shida yangu nalimwona BWANA”.  Kuna nyakati ambapo ni kupitia shida na usumbufu tunaweza kumwona Mungu. Ni methali ya zamani ya wazungu, “Bahari shwari haitoi wanamaji hodari” ni kweli baharia hodari ni lazima atakuwa na uzoefu wa kutatua shida za majini.
Usiogope sura ya mji, usiogope ukubwa wa changamoto inayokukabiri; cha msingi hakikisha uko mahali sahihi ukisubiri wakati sahihi wa kuinuliwa kwako. Mahali ambapo Mungu ameamuru baraka pana changamoto lakini pia pana baraka nyingi. Kuwa mahali pa baraka haina maana hapatakuwa na changamoto kabisa! Mara nyingi ustawi wako katika eneo hilo utategemea pia namna unavyomkumbuka Mungu, kumkumbuka maana yake kushika amri zake na kumshuhudia kwamba ni yeye ni Mungu aliyekufikisha hapo Sayuni yako.
Barikiwa na Endelea mbele…

0 comments :

Mwaka 2018 Uwe Mwaka wa Kujihatarisha.......

11:25:00 AM Unknown 0 Comments

 
MWAKA 2018 UWE MWAKA WA KUJIHATARISHA ZAIDI ILI KUPATA MAFANIKIO
Wengi wanashindwa kwa sababu hawafanyi kitu mpaka waone ni salama kabisa, hawaanzi mradi mpaka waone ni faida tupu, tabia hii imezuia mafanikio ya wengi. Mwaka jana niliingia kwenye biashara ya mtandaoni (online business) na kupata hasara ya milioni nne, mwaka huo huo bila ya kukata tamaa nikaingia katika biashara nyingine na kupata faida ya milioni nne! Ukipata hasara katika biashara moja haina maana kwamba na biashara nyingine utapata hasara pia.
Kitabu cha Mhubiri kinasema, “Mwenye kuuangalia upepo hatapanda; Naye ayatazamaye mawingu hatavuna” Mhubiri 11:4. Ukichunguza chunguza sana huji kufanikiwa katika uwekezaji na maendeleo. Kuna wakulima ambao wakijua ni msimu wa kilimo wanalima na hawa ndio hufanikiwa. Na kuna wale ambao hata kama ni msimu wa kilimo wao huchunguza chunguza mawingu na mwishowe wanashindwa kupanda mbegu zao.
Tabia ya kujihatarisha ni njema na imewasaidia wengi. Fanya kitu kwa wakati uchunguzi utakuja baadaye! Amesema Ratan Naval Tata mwanzilishi wa kampuni ya kutengeneza mitambo na magari aina ya TATA, “I don’t believe in taking right decision, I take decisions and then make them right” kwa tafsiri yangu amesema, “Siamini katika kuchukua maamuzi sahihi, bali nafanya maamuzi na baadaye nayafanya kuwa maamuzi sahihi”
Kujihatarisha inaweza ikawa ni kuachana na uhusiano mbaya, inaweza ikawa ni kuhama mji mmoja kwenda mwingine, inaweza ikawa ni kufunga na kuomba licha ya dalili za vidonda vya tumbo. Inawezekana ikawa ni kurejea nyumbani usiku kila siku kwa sababu za msingi, au ikawa ni kuamka mapema. Pia kujihatarisha inaweza ikawa ni kufanya kinyume na walio wengi, kwenda katika upekee wako au katika njia ya ubunifu ambayo wengi hawapiti. Vyovyote vile kama hatukujihatarisha kabisa hatutapata badiliko lolote.
Matajiri wengi akiwemo Bill Gates na Oprah Winfrey wamekuwa na sifa ya kukatiza masomo au kuacha kabisa ili kwenda kutumikia ndoto zao. Hii nayo ni kujihatarisha, kuacha kile ambacho dunia inaamini ni ufunguo wa maisha ilikuwa ni sawa na kuyafunga maisha yao. Lakini pamoja na hatari ya kuacha shule bado wamefanikiwa na wamewaajiri waliohudhuria vizuri shuleni. Kama kunamafanikio nje ya elimu basi ni muhimu tukajua elimu si ufunguo pekee. Maisha ni zaidi ya vidato!
Maskini wote wanachukia vurugu na hatari, hawapendi biashara nje ya kiyoyozi hata mara moja hawajitumi kutembeza bidhaa. Wanapenda usalama, kulala mapema na kuchelewa kuamka. Hawapendi kusafiri juu ya magari aina ya Fuso yanayokwenda minadani, wanapenda usafiri tulivu na salama, hawataki usumbufu wa wachuuzi wadogo wadogo wenye kutembeza biashara. Hawawazi kuajiri, wao wanataka kuajiriwa tu!
Nakumbuka mwaka 2015 baada ya sala na maombi niliamua kuondoka nyumbani umbali wa  mikoa mitano na kuhamia jijini Dar-es-salaam na ndani ya miezi miwili nilipata nilichokuwa nahitaji kwa muda ule. Si kila mtu atafanikiwa mjini wengine wanahitaji kurudi vijijini na wengine kwenda mjini ili kukutana na mafanikio yao. Ili kukutana na ndoto zao wengine itawalazimu kutoka Ulaya na kurejea katika nchi zao.
Unapopanga mipango yako mipya weka na mipango yenye kukuhatarisha (bila kuvunja sheria) na ndiyo mipango ya mafanikio.
Take risks, if possible take calculated risk……

0 comments :