Uvivu na Uuaji
UVIVU NA
UUAJI.
Maneno
haya mawili si rahisi kuyatenganisha, ni kama chanda na pete. Uvivu una hasara
kubwa sana na matokea yake ni uuaji. Utaua karama yako au kipaji chako, utaua
mtaji na pengine utapoteza yale ambayo wengine waliyasumbukia kwa muda mrefu na
walikupatia wewe uyaendeleze.
Uvivu
haufanyi tu ukose yale unayoyatamani kuyapata bali unakupokonya hata lile dogo
ulilonalo tayari. Muuzaji hodari atachukua wateja wa yule dhaifu na mvivu katika
biashara. Kile usichokitunza huondoka na hii ni kanuni wazi. Kile usichokilinda
kitaibwa hii haipingiki, ndio maana ikananenwa shika sana ulichonacho.
Nyakati
za mfalme Sulemani katika maandiko, yuko mama aliyemlalia mtoto wake na kumuua
kisha kugombea mtoto wa mwenzake. Alilala wakati wanawake wenzake hupumzika tu
maana wanajua mtoto ni muhimu kwao kwa saa 24. Ni uzembe wa hali ya juu
kusinzia hadi kuua mtoto uliyemsumbukia kwa muda mrefu (1Wafalme3:19).
Inawezekana wewe na mimi tukiendelea kulala kuna vitu vitakufa. Rafiki yangu
mmoja aliwahi kuniambia, “Alphonce, vijana hatulali tunapumzika tu” Ukipenda
usingizi utaua ndoto zako na hatma yako.
Siku
nyingine nikajifunza kuachana na neno sana. Nakushauri pia uondoe neno “sana”
katika misamiati yako. Nimechoka sana, nimesoma sana, nimetembea sana ni
sentensi zenye kuhalalishi na kutoa udhuru wa kutofanya kitu kinachotakiwa au
cha ziada. Hii ni dalili ya uvivu, neno sana lazima liondoke. Aliyechoka sana
atatamani kulala sana lakini aliyechoka atatamani kupumzika na kurejea tena
ulingoni. “So avoid using the word ‘very’
because it’s lazy”
Mwingine
anaweza kuwaza, Uvivu ni nini? Ni ile hali ya kughairisha mambo. Nitafanya
jioni, nitafanya kesho na hatimaye nitafanya mwakani. Uvivu pia ni hali ya
kushindwa kuzingatia jambo moja, ni kuitawanya akili katika mambo mengi ambayo
pengine si ya msingi. Uvivu pia ni ule uoga unakuja wakati wa kupanga mipango
mikubwa na migumu na hivyo mtu kwa kujihurumia anajipangia mipango midogo na ya
kawaida sana. Mvivu anakubali huondoka mapema hata kama kazi haijaisha, kamwe
hapambani mpaka mwisho. Kwa hiyo uvivu
ni ile hali ya kuishia njiani.
Inawezekana
umepoteza fursa nyingi na sasa huna cha kushika. Lile neno shika sana
ulichonacho halina tena nguvu kwako maana huna cha kushika. Usiogope, Yesu
Kristo aliye ufufuo na uzima na kweli anaouwezo wa kufufua yaliyokufa. Yeye
alimwita Lazaro aliyekufa na akatoka mzima. Kwake huyu Mungu mwenye nguvu, na
Mfalme wa ajabu twaweza kuomba, Ee Bwana fufua kazi zako ndani yetu.
Amka
sasa uangaze….
0 comments :