Ongeza maarifa katika eneo maalum
ONGEZA
MAARIFA KATIKA ENEO MAALUMU
Kama ilivyo kawaida, mwanzoni mwa mwaka
kila mtu anaweka malengo yake au mambo anayotaka afanikiwe au afanikishe katika
kipindi cha mwaka huo. Pamoja na kwamba si kila mtu ana utaratibu wa kuandika
malengo yake ya mwaka, lakini karibu kila mtu huwa na malengo au mambo
analiyopanga kufanikisha katika mwaka. Nafahamu
baadhi yetu tumeweka malengo ya kusoma vitabu katika mwaka huu mpya (kama
hujaweka lengo la kusoma vitabu, basi hujachelewa kufanya hivyo), hili ni jambo
jema kwa kila mwenye uwezo wa kusoma.
Pamoja na mipango na malengo yako mengi
uliyojiwekea kwa mwaka huu mpya, leo nataka nikupe hamasa juu ya jambo moja,
nalo ni kuweka nia au malengo ya kuongeza maarifa/ujuzi na ufahamu katika eneo mahususi au maalumu katika maisha yako.
Yaani badala ya kuweka lengo la kusoma tu, weka pia ni eneo gani unalotaka
kuongeza ujuzi au maarifa ili kuliboresha.
Mwenyehekima mmoja amewahi kusema "Usishibishe
njaa yako, shibisha maono yako [don’t feed your hunger, feed your vision]";
huu ni ushauri mmoja wa hekima ambao nimewahi kuupata kuhusu usomaji katika
kuishi kwangu. Lengo hapa ni kukuepusha na tabia ya kusoma kila kinachokuja
mbele yako bila malengo mahususi wala mpangilio utakao kusaidia kupiga hatua
zaidi katika maisha ya kila siku. Mtu anaweza kupanga mwaka huu nataka nisome
vitabu 30 au 20, lakini ukimuuliza unataka kusoma kuhusu nini au kuhusu eneo
gani, ni wachache sana wanamajibu yanayoeleweka (concrete answer)
Ili kusoma kwetu kulete badiliko katika
maisha yetu na mazingira tuliyopo ni muhimu ukachagua cha kusoma ukilenga
kuboresha eneo mahususi katika maisha yako. Na hapa utapata fursa ya kufanya
tathmini kuona kama unasogea, na kama kusoma kwako kuna kuletea faida inayoweza
kupimwa [measurable results].
Kumbuka, huwezi kusoma vitabu vyote
vilivyoandikwa, hivyo basi lazima ujue nini cha kusoma na nini cha kuacha hata
kama kina sura nzuri, ili mwisho wa mwaka useme kwa kusoma vitabu au kwa
kujifunza ujuzi fulani nimepiga hatua hii; kiuchumi, kiroho, mahusiano, ufanisi
kazi, huduma, ubora wa kazi zangu n.k
There’s a place for you at the Top
0 comments :