Biblia ina majibu yote

2:07:00 PM Unknown 0 Comments

BIBLIA INAMAJIBU YOTE
ISOME!
Ni mwaka mpya sasa nuia idadi ya vitabu unavyopaswa kusoma mwaka 2018, zaidi ya yote usisahau mpango wa kusoma Biblia, yearly bible reading plan! Tatizo la kutokusoma linaendelea kuwatesa watu wa leo, kizazi hiki hakijajijengea tabia ya kujisomea. Majibu mengi ya matatizo yetu yanayotukumba katika maisha ya kila siku yako katika vitabu, bahati mbaya hatusomi.
Hivi karibuni nikiwa naelekea Bagamoyo kwenye daladala nilifarijika baada ya mtoto wa miaka kumi kuingia ndani ya gari na kisha kutoa kitabu na baada ya mwendo kidogo akaanza kusoma. Nilitamani kupiga naye picha (selfie) kwa furaha, kuona utamaduni ninao upenda umejengeka kwa mtoto yule. Miji na majiji yenye foleni hutoa fursa kwa watu kujisomea wakiwa barabarani. Nyumbani utasema watoto wasumbufu barabarani je? Furaha tunayoikosa vijiweni iko kitabuni, nguvu tunayoikosa pahala pa kazi iko vitabuni, knowledge is power!! Mwenye maarifa mengi ni mwenye nguvu nyingi hili halipingiki. Kile ambacho baba yangu hakusema vitabu vimeniambia, kile ambacho dini ilinificha vitabu vimeniweka bayana. What a royal friend!
Nakushauri usome vitabu, lakini soma zaidi Biblia. Katika neno la Mungu kuna umilele wote. Yesu akasema, “ninyi mmekuwa safi kwa sababu ya lile neno mliliosikia”. Lile neno la Mungu unalosikia linafanya unakuwa safi mwili na roho.
Neno la Mungu limebeba majibu ya hali unazopitia wewe binafsi na Taifa lako pia. Unapotazama uchumi wako na hali ya taifa lako usiende tu kwa kutumia elimu ya uchumi ya darasani, ni muhimu utazame kiroho pia. Ukiona hali ngumu ya uchumi kwenye nchi jiulize Mungu anataka nini kwa taifa lako, inawezekana kabisa anataka toba. Badala ya kwenda kuchukua shahada ya uzamili ya uchumi mara nyingine ni muhimu kusoma Biblia mfululuzo. Daniel kwa kusoma maandiko (neno la Mungu) aligundua nini kinaendelea kwenye taifa lake.
Jifunze kujua chanzo, anayejua chanzo halalamiki sana. Taifa linapopewa mtawala mkorofi ni lazima ujue kuna mahali dhambi ilitendeka katika Taifa hilo na Mungu amemweka mtawala huyo kwa makusudi yake ili watu wake watubu na kurejea. Katika hali kama hiyo kufanya kazi kwa bidii hakutasaidia ila toba ya kweli kwa wateule wote wa Mungu walioko kwenye taifa hilo inaweza kuleta suluhisho.
Moja ya njia kuu ambayo Mungu amekuwa akiitumia kuzungumza na nchi na watu binafsi ni hali ya uchumi. Ukiaona kuna mvua ya kutosha, tena kwa wakati wake ni lazima ujue kuna kitu kizuri Mungu anazungumza, ukiona ukame na watu wanakufa kwa njaa ujue kuna kitu Mungu anadai au ibada ya sanamu imekithiri, ukiona watu wengi wanakimbia nchi ujue kuna laana ya ukiwa.
Katika kila jambo lihusulo hali ya hewa, mahali pa kuishi, hali ya uchumi ni muhimu utafute makusudi ya Mungu katika Biblia. Mambo haya yote ndani yake kuna makusudi ya Mungu, ukiyatafute ndani ya neno la Mungu utayajua! Jipatie ufahamu uyajue yanayokuhusu na yanayohusu nchi yako kwa kusoma maandiko. Barikiwa.

0 comments :