Kuanzia viongozi .......
(Sote tunamuhitaji Yesu)
Sote
tunamuhitaji Yesu kuanzia viongozi wa dini kama Papa Francis mpaka Viongozi wa
siasa kama Barack Obama sote kwa ujumla tunamuhitaji mwokozi. Hakuna wokovu kwa
mtu awaye yote ila kwa Yesu Kristo tu. Nukuu za Alexender The Great ni simulizi
zenye mafunzo tele. Kuna nyakati alinukuliwa akisema, “Nitakapokufa nataka jeneza langu libebwe na madaktari bingwa, waweke
mikono yao juu ya jeneza langu ili watu wajue wazi kwamba kuna nyakati, hata
madaktari wazuri hawataweza kuokoa maisha.”
Madaktari
bingwa wanaposhindwa wanamfanya mwanadamu akumbuke kwamba, hakuna uzima kwa mtu
awaye yote isipokuwa kwa Yesu Kristo. Bill Graham anasema, “Hata wanasayansi
wasiomjua Mungu wala kumkiri wakishaugua saratani (cancer) huanza kukiri na
kusema Mungu nisaidie”. Biblia inamfananisha mwandamu na ua ambalo leo lipo na
kesho halipo tena. Hakuna la kudumu ndani ya mwanadamu.
Nje
ya Yesu Kristo mwanadamu ni kama kivuli punde hayupo tena. Mwandamu anapata uzima
ndani ya Kristo na si uzima tu unaokomeshwa na kifo bali uzima ulio juu ya
kifo. Kifo hakiwezi kukomesha maisha ya mtu amwaminiye Kristo Yesu. Iko wazi
katika 1Kor 15:55-56 Yesu Kristo alishinda kifo kwa ajili yetu hata ikaandikwa,
“Ku wapi, Ewe mauti, kushinda kwako? U
wapi, Ewe mauti, uchungu wako? 56 Uchungu wa
mauti ni dhambi, na nguvu za dhambi ni torati.”
Mauti imeshindwa, mauti imechoka na
uzima wa Yesu Kristo umetawala tena. Mauti ilipata nguvu kupitia dhambi naye
Yesu Kristo alipokwisha kutusamehe dhambi zetu basi aliivunja ile nguvu ya
mauti. Ndio maana watu wengi waliokuwa karibu na kufa alipowaambia wamesamehewa
dhambi waliponywa, maana nguvu ya mauti ni dhambi, dhambi ikiondolewa mauti
hukosa nguvu. Wamwaminio hawaogopi kifo.
Je, unahisi kufa? Je, unaogopa kifo?
Nguvu ya uhai inakuja kupitia msamaha. Wale wenye hakika kwamba, Mungu
amewasamehe dhambi zao kamwe hawaogopi kifo. Biblia inasema, “anaraha
aliyesamehewa dhambi”, kwa lugha nyingine anafuraha aliyesamehewa dhambi.
Waliosamehewa dhambi wamebarikiwa tena biblia inasema wanayo heri. Zaburi
32:1-2
Yesu aliishinda mauti kwa kupitia
kuishinda dhambi. Na hakuna mwandamu awaye yote aliyeishinda dhambi na
kuiharibu pale msalabani isipokuwa Yesu Kristo peke yake. Madaktari, walimu,
viongozi wa siasa, viongozi wa dini hawakuweza na hawataweza ni Yesu peke yake.
Mhimili (mzizi) wa kifo ni dhambi, unapotubu unafukuza mauti na hofu zake.
Tumaini la uhai na uzima wetu ni Kristo
peke yake. Kama tungelikuwa na uzima Yesu asingelikuja. Kama tungelikuwa wema
asingekuja pia. Kwa hiyo amekuja kwa sababu tulikuwa wafu kwa dhambi, watupu
kwa uovu wetu na wachafu kwa matendo yetu.
Mwimbaji mmoja anasema, “All I need is you” ni kweli tunamuhitaji
Yesu peke yake. Tunamuhitaji kila saa na kila wakati. Ni vema tusogelee mahali
anapokaa. Twende kitini pake kwa toba. Imeandikwa, “Basi na tukikaribie kiti cha neema kwa
ujasiri, ili tupewe rehema, na kupata neema ya kutusaidia wakati wa mahitaji. ” Waebrania 4:16
Yesu anapatikana katika kiti cha rehema
na biblia inasema, “wakati wa mahitaji”. Je! ni wakati gani huo tunaohitaji
neema na rehema? Ni kila saa na kila dakika. Mara kadhaa asubuhi nimekuwa
nikipiga magoti na kuomba neema ya siku husika, kwa kuwa najua ninahitaji neema
kila siku. Najua namuhitaji Yesu kwa uhai wangu.
Siku ukitenda dhambi unahitaji neema,
na siku usipotenda dhambi unahitaji neema pia. Na kama tunahitaji neema kila
siku na kila saa basi moja kwa moja tunamuhitaji Yesu kila siku na kila saa.
Yeye ndiye mtoaji wa neema hizo. Pata muda wa kuomba sote tunahitaji
neema...tukutane wiki ijayo mpendwa. Barikiwa
0 comments :