UNATUMIA KIUNGO GANI KUTAZAMA MBALI?

8:22:00 PM Unknown 0 Comments

 
UNATUMIA KIUNGO GANI KUTAZAMA MBALI?
Mwili wa binadamu unaviungo vingi kila kimoja kikiwa na kazi yake. Ipo pia milango ya fahamu ambayo kwa kuhisi, kunusa, kuonja na kwa kuona hufanya kazi. Viungo hivi na milango hii ya fahamu si tu kwamba ipo kwa binadamu bali hata wanyama, ndege na baadhi ya wadudu wamejaliwa na Mwenyezi kuwa nayo.
Binadamu ndiye mwenye jukumu la kuwatawala ndege, wanyama, wadudu na hata viumbe wasioonekana (mapepo, majini, malaika). Kitabu cha Waebrania kimeeleza malaika ni roho wanotuhudumia, pia mzaburi amenena wazi jinsi Mungu alivyomfanya mwanadamu punde tu kama yeye na amemvika utukufu na heshima.
Licha ya utukufu huo mwanadamu si kiumbe mwenye uwezo mkubwa wa kuona. Tai, mwewe na hata ndege wengine huona mbali zaidi kuliko mwanadamu. Ni watu wachache tu wenye macho makali ya kuona mita mia tano au zaidi.
Swali, Ni kwa nini macho ya wanadamu ambao kibiblia ndio watawala wa dunia hii yanazidiwa na hawa ndege? Jibu langu ni rahisi, Mungu hakutaka mwanadamu aishi kama tai, Hakutaka mwanadamu aone mbali kwa macho ya nyama bali atumie akili, fikra na imani katika kuona kwake. Kwa njia hizi ataona mbali zaidi ya tai na hivyo atamtawala mpaka tai.
Mwanadamu anauwezo wa kuona hata miaka 20 ijayo na akanunua shamba leo na kupanda miti. Mwanadamu wa leo anaweza kuona miaka 100 ijayo. Hayati Rais Kennedy wa Marekani anayetajwa katika simulizi za kwenda mwezini, aliwaita wanasayansi wake na kuwapa wazo hilo ambalo hawakuwa wamewahi kulisikia popote. Hebu waza unamka unaitwa na Rais na anakwambia, naomba uanze kufikria jinsi gani tutakwenda kwenye Mwezi au Jua. Wakati huo wewe hujawahi hata kuzifuatilia nyota za angani.
Baada ya wanasayansi hao kufanyia kazi wazo hilo kwa miaka kadhaa walifanikiwa na kwa sasa kwenda mwezini au kutuma vyombo kwenda huko si jambo la ajabu tena. Tofauti na hayati Rais Kennedy ambaye ni mtu wa fikra, Rev Martin Luther King Jr ambaye ni mwanaharakati, yeye katika harakati zake za kumkomboa mtu dhidi ya ubaguzi  wa rangi anaonekana kuona mbali kama nabii, na hii ni kwa sababu ya Imani yake ambayo mzizi wake ni neno la Mungu.
Alisema Fred Swaniker kwamba, Afrika inahitaji Moon shoot thinking, akimaanisha tunahitaji kufikiri mbali sana, tunahitaji kuruka kifikra (kimawazo) na kutua mbali, mahali ambapo kwa uhalisia macho ya kawaida hayapaoni ila kwa imani na fikra sahihi tunapaona.
Katika ulimwengu huu hata kipofu anaweza kufanikiwa kama ubongo wake umechangamka kuliko watu mia wenye macho makali lakini ubongo umelala. Kuna jambo linanishangaza katika taifa langu, vijana wengi ukiwahoji si watu wa fikra.
Siku 1000 za kwanza katika ukuaji wa mtoto zijulikanazo kama “mwanzo bora” zina mchango mkubwa katika uwezo wa kufikri wa mtoto. Utapia mlo ndio huzaa watu wenye mawazo mgando, na mawazo maji, yote ni matokeo ya mdororo wa chakula. Mfumo wetu wa elimu hauruhusu udadisi hasa kwa kuwa mwalimu ndio kila kitu, si rahisi mfumo wetu kuzalisha watu wanaofikiri kimkakati.
Ili tupate vijana wanaofikiri sawasawa basi ni muhimu tuwajenge kwa neno la Mungu ambalo litaleta imani, tuwape chakula bora cha akili yaani vitabu sahihi vya kiada na ziada, watoto wapewe mlo kamili ukijumuisha matunda, vyakula vya wanga, protini na maji mengi.

0 comments :