USIWAPELEKE MAHALI USIPOWEZA KUWATOA
USIWAPELEKE MAHALI
USIPOWEZA KUWATOA
Hili ni jambo la msingi kwa kiongozi wa
ngazi yoyote ile, haijalishi ni ngazi ya familia, kata, kampuni, taasisi
binafsi au kiongozi wa siasa. Kuna maeneo ukiwafikisha watu au ukiwapeleka
unaowaongoza hautaweza kuwatoa wote kwa usalama. Kiongozi lazima awe na kipimo
cha madhara na uathirika unaoweza kujitokeza kabla ya kuchukua uamuzi wake.
Kwenye biblia kuna kisa cha Lutu aliyemuita
Ibrahimu mjomba. Huyu baada ya kuipeleka familia yake katika miji ya Sodoma na
Gomora alishindwa kuwatoa wote. Huko alimpoteza mkewe. Alitamani waokoke familia nzima kama
walivyoingia lakini hakuweza. Ingawa haijaandikwa lakini nina hakika Lutu
alijisikia vibaya kumpleleka mkewe mahali asipoweza kumtoa. Sodoma ilikuwa ni
uchaguzi wa Lutu nyakati za kutengana na Ibrahamu, haukuwa uchaguzi wa mkewe
Lutu. “Lakini mkewe
Lutu akatazama nyuma yake, akawa nguzo ya chumvi.” Mwanzo 19:26
Rais Obama aliyekuwa kinara katika
kuangusha Serikali ya hayati Rais Gadafi wa Libya alinukuliwa akijutia
kushindwa kuijenga Libya mpya. Obama amewafikisha watu wa Libya mahali ambapo
hawezi kuwatoa. Mpaka ameondoka hajaweza kujenga Libya mpya aliyoahidi na
badala yake imekuwa pango la magaidi na wapiganaji.
Amesisitiza mwenye hekima mmoja kwamba, “In life you cannot undo every action”
akimaanisha, “Katika maisha si kila kitu unaweza kukirejesha tena katika
uhalisia wake.” Kuna akili zilizoharibika, kuna familia zilizoharibika, kuna
vikundi vilivyoharibika; kuna jamii zilizoharibika, pia kuna kampuni
zilizoharibika na si wote watakao weza kufanya urejesho. Kwa kuwa zoezi la
urejesho ni gumu na zito basi ni busara kuepuka uovu, tabia hatarishi na
mazingira yake. Huwezi kuepuka moshi ikiwa unapika kwa kuni, kwa hiyo katika
kubadilisha mwenendo huwezi kupuuza mchango wa mazingira yako. Mazingira
hatarishi ya Sodoma na Gomora ndio chanzo cha uharibifu wa mke wa Lutu.
Kama baba wa familia au kiongozi (Lutu) ni
lazima uogope maamuzi au maeneo ambayo huna uhakika kwamba, wale unaowaongoza
watatoka salama. Yuko rafiki anayeweza kukufundisha tabia mbaya ambayo huwezi
kuiacha, yako makundi mabaya ambayo yanaweza kukufundisha tabia hatarishi
ambazo huwezi kuzikomesha. Je, unamkumbuka uathirika uliingia lini maishani
mwako? Ulevi, ubwiaji wa unga na dawa za kulevya, utazamaji wa picha chafu na
uasherati? Ni baada ya kujisamehe sisi wenyewe ndipo tunapoweza kumsogelea Yesu
mwanamapinduzi ili atusamehe na kutupa upya.
Watu wengi wamekuwa wanamwogopa Yesu kwa
kuwa ni mwanamapinduzi na wanajua wakimsogelea atapindua tabia zao na atapanda
tabia njema. Mwanamke Msamaria aliyekutana na Yesu kwenye kisima cha Yakobo
alikuwa na uathirika. Alikuwa amekuwa na wanaume watano, that was an addiction! Na kwa muda ule mfupi Yesu alipindua
maisha yake.
Muda, afya njema, ufahamu, malezi ya
watoto, umoja na mshikamano ni moja ya mambo ya kulinda sana kwa kuwa
hayarejeshiki kirahisi na pengine hayarejesheki kabisa baada ya kuharibiwa.
Jilinde!
0 comments :