Bwana alipoamuru baraka
BWANA ALIPOAMURU BARAKA
MUDA MWAFAKA ENEO
MWAFAKA.
Katika mambo ambayo Mungu hata subiri
ufanye maandalizi ni hukumu na fursa. Kila siku unapaswa kuwa tayari, katika
eneo husika, mwenye maandalizi kamili, ndio maana ya lile neno kesheni. Si kila
eneo, si kila Mkoa, si kila medani wala si kila nchi itakuwa na Baraka zako;
liko eneo moja, iko aina ya biashara fulani, uko mkoa na pahala ambapo Mungu
ameamuru baraka zako zipatikane. Wakati mwingine tunachagua miji kwa macho ya
nyama na hivyo tunavyokwenda ndani yake hatufanikiwi sana. Si kila aliyeko
Ulaya anamafanikio, kuna wengine wako huko na wanaomba chakula, hawana uhakika
wa kupata milo mitatu.
Kuna watu ambao walikuwa jijini Dar es
salaam ilhali baraka yao ilikuwa Dodoma. Kwa vyovyote vile haikuwa rahisi
kuwapeleka watu hao Dodoma inawezekana walifikiri hakuna maisha bora nje ya
jiji la Dar es salaam. Lakini Mungu kwa
kutumia Tangazo la Serikali la kuhamia Dodoma amewawezesha pia maelfu ya
watanzania kwenda kwenye baraka yao iliyoamriwa mjini Dodoma. Tangu nyakati
za Yesu Kristo mpaka sasa matangazo mengi ya Serikali yamekuwa yakibeba
makusudi ya Mungu ya amani. Amani maana yake uchumi mzuri, Baraka na mafanikio.
Yanaweza matangazo hayo yakaonekana magumu na mabaya yenye kubeba usumbufu
lakini baadaye Mungu hujitwalia utukufu na watu wake hustawi.
Ukihamishwa
kwa Tangazo la Serikali usigome, Matangazo hayo hubeba baraka. Katika saa yako ya kusimama kiuchumi na
kiutumishi tangazo hilo halitaweza kukudhuru hata kama lilitolewa ili
kukuangamiza wewe. Tangazo la Herode la kuua watoto wote chini ya miaka miwili
halikuweza kumua Yesu maana ilikuwa ni wakati wa Yesu kung’aa na kuokoa, halikuweza
kumzuia.
Si miji peke yake, hata changamoto nyingine
za maisha zenye ukakasi ndani yake kuna
baraka pia. Wako watu ambao bila talaka wasingelipata wokovu, bila kuachwa
wasingelijua kusimama wenyewe, wako wale ambao bila kufeli masomo wasingeli
jaribu biashara ambazo leo zimewapandisha na kuwafanya wakuu.
Baraka hizo zisingepatikana ikiwa kila kitu
kingekuwa shwari, mara nyingi inapokuwa ni shwari watu hujisahau sana na
kufanya yasiyo ya msingi. Biblia inasema, “Katika shida yangu nalimwona BWANA”. Kuna nyakati ambapo ni kupitia shida
na usumbufu tunaweza kumwona Mungu. Ni methali ya zamani ya wazungu, “Bahari
shwari haitoi wanamaji hodari” ni kweli baharia hodari ni lazima atakuwa na
uzoefu wa kutatua shida za majini.
Usiogope sura ya mji, usiogope ukubwa wa
changamoto inayokukabiri; cha msingi hakikisha uko mahali sahihi ukisubiri
wakati sahihi wa kuinuliwa kwako. Mahali ambapo Mungu ameamuru baraka pana
changamoto lakini pia pana baraka nyingi. Kuwa mahali pa baraka haina maana
hapatakuwa na changamoto kabisa! Mara nyingi ustawi wako katika eneo hilo
utategemea pia namna unavyomkumbuka Mungu, kumkumbuka maana yake kushika amri
zake na kumshuhudia kwamba ni yeye ni Mungu aliyekufikisha hapo Sayuni yako.
Barikiwa na Endelea mbele…
0 comments :