Mungu Hahitaji Kufikiri

11:50:00 AM Unknown 0 Comments

 
MUNGU HAHITAJI KUFIKIRI
MIMI NA WEWE TUNAPASWA KUFIKIRI
Mungu mwenyezi anazo sifa nyingi, ni Mungu aliyeumba majira na nyakati, nchi na vyote viijazavyo ni kazi ya mikono yake na ni mali yake. Hakuna historia wala yajayo ambayo yamefichika machoni pake. Anayejua mambo yote ya sasa, yajayo na yaliyopita. Ni Mungu wa nyakati zote, za sasa na zijazo. Mbele yake hakuna siri. Ndio maana imeandikwa, “maana naijua mipango niliyonayo kuwahusu ninyi, asema BWANA, ni mipango mizuri si mibaya” (Tafsiri yangu kutoka Yeremia 29:11)
Mwanadamu anahitaji kufikiri ili kuleta majibu kwenye changamoto inayomkabiri au inayokikabiri kizazi chake. Kunapokuwa na namna tatu, mwanadamu anahitaji kufikiri ili kupata namna moja ambayo ni bora zaidi. Kunapokuwa na njia tatu, mwanadamu anahitaji kufikiri ili kupata njia moja ambayo itampendeza Mungu, haitaharibu mazingira wala hamtamdhuru jirani yake. Baada ya kufanikiwa kupiga hatua kubwa kwenye mambo teknohama dunia sasa inahitaji kufikiri kuhusu usalama wa mazingira, hali ya joto Duniani na usalama wa vizazi vijavyo.
Fikra sahihi zinatupa nafasi ya kufanya maandalizi ya mambo yajayo. Usipofikiri kuhusu yajayo yatakapokuja yatakukuta huna maandalizi yoyote, kwa hiyo hautaweza kusimama katika nyakati hizo. Kwa mtu makini hakuna nyakati za furaha kama nyakati za mwisho ambazo tumezoea kuziita, “future
Tabia za mazoea huua uwezo wa kufikiri. Kuna mambo ambayo hujulikana na yamezoeleka haya hayadai fikra mpya katika utekelezaji wake. Wale wanafunzi ambao huamka, hula chakula, huenda darasani, kisha kuoga na kulala huwa hawana jipya maana hurudia matendo hayo kila siku. Wale ambao huamka, hufanya sala, kisha zoezi, kisha usafi, kisha masomo, kisha kuimba kwaya, kisha siasa za shuleni, kisha uongozi wa shule huwa watu bora zaidi kuliko wale wenye mambo machache na madogo kama sisimizi.
Kizazi cha sasa kinahitaji mageuzi makubwa kifikra, walio wengi wanalipwa kwa sababu ya muda wanaotumia kazini. Hawalipwi kwa sababu ya matokeo, wala kwa sababu ya akili bali wanalipwa kwa sababu ya mahudhurio yaani, muda fulani mpaka muda fulani. Tunahitaji kuhama, Shift from being paid for your time to being paid for your mind!
Akili inachuja na kuchekecha, inapima na inatoa majibu. Akili inakupa uwezo wa kufika mahali kimawazo  ambapo miguu yako haijawahi kupakanyaga kimwili. Biblia iliposema, “ uishi na mwanamke kwa akili” ilitaka ujue kwamba, hauna taarifa za kutosha kumuhusu kwa maana wewe si Mungu wake, ilitaka ufike mahali kimawazo ikiwezekana kabla yeye hajafikia maana akikutangulia kufika inawezekana usimwelewe, ilikutaka ujizoeze kufikiri, kuchambua, na kupima matakwa yake na mazingira yake. Kwa kufikiri unaweza kupambanua kati uongo na ukweli.
Kwa uzoefu wangu mdogo vijana wale walikuwa na ufinyu wa fikra miaka ile tulipokuwa shuleni hata sasa mtaani utawakuta na kibano cha fikra na mara nyingi hawa watu ni watiifu sana kwa historia, dini za mababu na ni wapesi kurithi mila na desturi zilizopo, wala hawajisumbui kuzikosoa pale zinapopwaya, mara nyingi watu hawa hupenda sana kusifia watawala, they cannot challenge the conventional knowledge!
Kwa nini tunahitaji kufikiri? Katikaa kitabu cha, “Teach your Child How to Think” mwandishi Edward de Bono ameeleza wazi, “Tunahitaji kufikiri kwa sababu hatuna taarifa za uhakika kuhusu mambo ya baadaye, tukiwa na taarifa kamili na mambo yote yakiwa wazi na utupu mbele yetu hatutakuwa na haja ya kufikiri maana kila kitu kitakuwa wazi”. Hii ndio sababu imenifanya niamini Mungu hahitaji kufikiri, hawezi kujiuliza itakuwaje ilhali anajua kila kitu.
Karibu katika, Weekend of Purpose ya April, 2018 na tuandikie katika email na blog yetu.
Bwana Mungu Akubariki,

0 comments :