Wapi niende kujenga fikra mpya

3:06:00 PM Unknown 0 Comments

WAPI NIENDE KUJENGA FIKRA MPYA
Renew your Thinking
Kwa wiki mbili mfululizo tumekuwa tukiandika kuhusu Fikra. Wapi uende, nini ufanye na kwa nini kubadilisha mfumo wa kufikiri. Kesho yetu haitaweza kubadilika kama bado fikra zetu zinafanana na jana.
Tunavaa mavazi tuliyoyawaza jana usiku, tunaenda mahali tulipowaza kabla ya kwenda. Usipobadili mfumo wa kufikiri huwezi kubadili mwenendo wa maisha. Kwanza, ni muhimu kuwa walau na dakika kumi kila siku jioni au asubuhi kwa ajili ya kukaa kimya na kufikiri. Ni muhimu kila siku upate muda wa upekee na ukimya (shut from the world) ili uweze kujitathmini na kufikiri kwa upana.
Fikra ni chakula inategemea unakula wapi. Ukila picha za ngono utakuwa mjinga, ukila udaku utakuwa na mambo yakufanana na udaku, ukila majarida ya matangazo ya pombe utakuwa mtumwa wa pombe.
Twende kwenye jambo safi, tujifunze kwenye kitabu kizuri, channel safi ya Luninga, kikundi cha busara cha WhatsApp. Usione haya kutoka kwenye kundi ambalo halina maadili. Usiogope kuchana na kuchome picha na majarida yenye kuharibu akili. Mambo ya uasherati na ulevi huharibu akili.
Imenenwa, “aziniye na mwanamke hana akili kabisa” tena ikanenwa, “mambo ya ulevi huharibu ufahamu” mambo haya huharibu ufahamu na kufanya uwezo wa mwanadamu wa kuamua na kufikri kupungua.
Hatupaswi kutafakari kila jambo, bali yale tu tuliyojifunza na kuyaona yanafaa kwa kutafakari. Ushindi wote wa mwandamu uko katika tafakari. Mungu alimwambia Joshua atafakari neno lake mchana na usiku na azungumze hilo neno kila siku. Kwa kufanya hivyo ushindi ulidhihirika katika maisha ya Joshua mwana wa Nuni. Joshua 1:8
Dunia inataka watu wajanja. Lakini maandiko yanataka kabla hatujawa wajanja tuwe watu safi, wasio na waa lolote mbele za Mungu. Daniel ni mmoja wa watu safi, alionekana na akili mara kumi kuliko waganga na wachawi. Mtume Paulo amesisitiza nini tufikiri kama tunataka kuwa wajanja na safi (pure and smart in all our way) “Mambo mliyojifunza kwangu na kuyapokea, na kuyasikia na kuyaona kwangu, yatendeni hayo; na Mungu wa amani atakuwa pamoja nanyi.” Flp 4:9
Mazoezi ya kutenga muda wa kufikiri, kujizoeza kusoma neno la Mungu na kuacha makundi mabaya kutabadilisha kabisa namna yako ya kufikiri. Barikiwa.

0 comments :