Mwaka 2018 Uwe Mwaka wa Kujihatarisha.......
MWAKA 2018
UWE MWAKA WA KUJIHATARISHA ZAIDI ILI KUPATA MAFANIKIO
Wengi
wanashindwa kwa sababu hawafanyi kitu mpaka waone ni salama kabisa, hawaanzi
mradi mpaka waone ni faida tupu, tabia hii imezuia mafanikio ya wengi. Mwaka
jana niliingia kwenye biashara ya mtandaoni (online business) na kupata hasara
ya milioni nne, mwaka huo huo bila ya kukata tamaa nikaingia katika biashara
nyingine na kupata faida ya milioni nne! Ukipata hasara katika biashara moja
haina maana kwamba na biashara nyingine utapata hasara pia.
Kitabu
cha Mhubiri kinasema, “Mwenye
kuuangalia upepo hatapanda; Naye ayatazamaye mawingu hatavuna” Mhubiri
11:4. Ukichunguza chunguza sana huji kufanikiwa katika uwekezaji na maendeleo.
Kuna wakulima ambao wakijua ni msimu wa kilimo wanalima na hawa ndio
hufanikiwa. Na kuna wale ambao hata kama ni msimu wa kilimo wao huchunguza
chunguza mawingu na mwishowe wanashindwa kupanda mbegu zao.
Tabia
ya kujihatarisha ni njema na imewasaidia wengi. Fanya kitu kwa wakati uchunguzi
utakuja baadaye! Amesema Ratan Naval Tata mwanzilishi wa kampuni ya kutengeneza
mitambo na magari aina ya TATA, “I don’t believe in taking right decision, I
take decisions and then make them right” kwa tafsiri yangu amesema, “Siamini
katika kuchukua maamuzi sahihi, bali nafanya maamuzi na baadaye nayafanya kuwa
maamuzi sahihi”
Kujihatarisha
inaweza ikawa ni kuachana na uhusiano mbaya, inaweza ikawa ni kuhama mji mmoja
kwenda mwingine, inaweza ikawa ni kufunga na kuomba licha ya dalili za vidonda
vya tumbo. Inawezekana ikawa ni kurejea nyumbani usiku kila siku kwa sababu za
msingi, au ikawa ni kuamka mapema. Pia kujihatarisha inaweza ikawa ni kufanya
kinyume na walio wengi, kwenda katika upekee wako au katika njia ya ubunifu
ambayo wengi hawapiti. Vyovyote vile kama hatukujihatarisha kabisa hatutapata
badiliko lolote.
Matajiri
wengi akiwemo Bill Gates na Oprah Winfrey wamekuwa na sifa ya kukatiza masomo
au kuacha kabisa ili kwenda kutumikia ndoto zao. Hii nayo ni kujihatarisha,
kuacha kile ambacho dunia inaamini ni ufunguo wa maisha ilikuwa ni sawa na
kuyafunga maisha yao. Lakini pamoja na hatari ya kuacha shule bado wamefanikiwa
na wamewaajiri waliohudhuria vizuri shuleni. Kama kunamafanikio nje ya elimu
basi ni muhimu tukajua elimu si ufunguo pekee. Maisha ni zaidi ya vidato!
Maskini
wote wanachukia vurugu na hatari, hawapendi biashara nje ya kiyoyozi hata mara
moja hawajitumi kutembeza bidhaa. Wanapenda usalama, kulala mapema na kuchelewa
kuamka. Hawapendi kusafiri juu ya magari aina ya Fuso yanayokwenda minadani,
wanapenda usafiri tulivu na salama, hawataki usumbufu wa wachuuzi wadogo wadogo
wenye kutembeza biashara. Hawawazi kuajiri, wao wanataka kuajiriwa tu!
Nakumbuka
mwaka 2015 baada ya sala na maombi niliamua kuondoka nyumbani umbali wa mikoa mitano na kuhamia jijini Dar-es-salaam
na ndani ya miezi miwili nilipata nilichokuwa nahitaji kwa muda ule. Si kila
mtu atafanikiwa mjini wengine wanahitaji kurudi vijijini na wengine kwenda
mjini ili kukutana na mafanikio yao. Ili kukutana na ndoto zao wengine
itawalazimu kutoka Ulaya na kurejea katika nchi zao.
Unapopanga
mipango yako mipya weka na mipango yenye kukuhatarisha (bila kuvunja sheria) na ndiyo mipango ya mafanikio.
Take risks,
if possible take calculated risk……
0 comments :