Utimilifu wa kusudi lako......
UTIMILIFU WA KUSUDI
LAKO UTAHITAJI MAFUNGO
Ni kwa zaidi ya miaka mitatu sasa Programu
yetu (Life Minus Regret) imekuwa kazini katika kuwasaidia watu kujua makusudi ya
kuumbwa kwao na kuyaishi. Tumekuwa tukiwahamasisha vijana wamjue Mungu ili naye
awaambie wao (vijana) ni akina nani.
Ni Mungu aliyemwambia Yeremia, “nimekuweka uwe nabii wa mataifa” ni Yesu
aliyemwambia Petro, “lisha kondoo zangu”, na baadaye akamwambia tena, “chunga
kondoo zangu.” Hawa wote walipata kuambiwa kazi zao na wito wao kwa sababu
walitafuta kumjua Mungu na kuhusiana naye.
Mambo matatu ni muhimu katika kuhusiana na
Mungu; kusali, kufunga na kutoa sadaka. Yesu akasema “nanyi msalipo…,” maana
yake anategemea tutakuwa tunasali mara kwa mara, tena akasema, “nanyi
mfungapo….” Pia akihimiza “nanyi mtoapo sadaka…” Haya matatu aliyafundisha kwa
kuwa yote ni muhimu kufanyika mara kwa mara ili kumkamilisha mtu. Mathayo 5:2, 5,
6 na 16
Sala, sadaka na mafungo ni vitu muhimu
katika kuhusiana na Mungu. Katika eneo la sala na sadaka wengi wanajitahidi,
changamoto iko katika eneo la ushindi na mafanikio ambalo ni eneo la kufunga.
Wengi hupanga kufunga na kabla siku haijafika hughairi na kufakamia chakula.
Shetani hatoi ruhusa katika hili kwani anajua lina baraka, tena halijali idadi.
Mafungo ni muhimu kwa ajili ya huduma yako
na kusudi lako. Kama Yesu angeweza kutimiza kusudi lake bila mafungo
asingelifunga. Alifunga siku 40 kwa sababu ilikuwa muhimu. Huduma nyingi
huzaliwa kipindi cha mafungo. Huduma ya mitume waliotengwa yaani, Barnaba na
Sauli ilikuwa ni baada ya maombi na mafungo. Matendo ya Mitume 13:2
Jentezen Franklin katika kitabu chake cha:
“Fasting” anakiri huduma yake ilizaliwa kipindi cha mafungo, Mchungaji Oyadepo
na wengine wengi huelezea jinsi mafungo yalivyofungua njia katika wito wao na
makusudi ya Mungu maishani mwao.
Ukiweza unaweza kukataa kula chochote kile
kwa muda fulani. Pia katika kufunga unaweza kataa chakula cha nguvu yaani,
wanga na ukashinda siku yako yote ukinywa maji tu au chai tu. Siku hizi
nikifunga huwa nakunywa maji tu, hii huondoa maswali kwa wanaonizunguka kujua
kwamba nimefunga au sikufunga. Usifunge na kujinyima vimiminika kiasi cha
kukosa nguvu ya kuomba. Unaweza kunywa chai au juice pekee kwa saa 12 au 24 na
hayo ni mafungo mazuri kwani nina hakika utakuwa na nguvu katika kuomba na
kusali wala hutaomba kwa ulegevu.
Usichokijua nyuma ya mafanikio ya watu
wengi wakuu ni yako mafungo na sadaka. Mafungo hufanya mwili na nafsi
visielekee kwenye chakula na badala yake vimwelekee Mungu. Kuna jambo bado
halijatimia katika huduma na wito wako nalo litahitaji mafungo. Ni muhimu kwa
kukupa upenyo na kukufungulia yaliyofungwa.
Barikiwa
0 comments :