Jitazame kama Mungu anavyokutazama
JITAZAME KAMA MUNGU ANAVYOKUTAZAMA
Sehemu
kubwa ya maisha ya mtu huathiriwa (influenced) sana na namna anavyojitazama.
Mara nyingi, mtazamo wa mtu juu ya maisha yake na nafsi yake huamua hatima
yake. Mtu anayejitazama kama aliyeshindwa (failure) katika jambo fulani; hakuna
namna ataweza kushinda au kufanikiwa katika jambo hilo. Hakuna mtu aliyeweza kwenda mbali zaidi ya mtizamo wake (jinsi
aonavyo nafsini mwake). Kumbuka, Jinsi
ujitazamavyo, ndio kikomo chako.
Suleimani,
Mwenye hekima wa kale na kiongozi wa taifa la Israeli amewahi kusema, “Maana aonavyo (mtu) nafsini
mwake ndivyo alivyo”. Akiwa na maana
kwamba, kiwango na aina ya maisha anayoishi mtu ni matokeo
ya namna mtu huyo anavyoona nafsini mwake. Kama mtu haridhishwi na aina ya
maisha anayoishi au kiwango cha maisha anayoishi, hatua ya kwanza kabisa sio kubadili kazi au biashara; bali kuangalia na kubadili
fikra na mtizamo wake uliomfikisha mahali alipo. Ndio maana wataalamu wa
sayansi ya fedha wanasema, mtaji wa kwanza kwa mtu sio fedha bali wazo (mtizamo/fikra)
jipya.
Tunaishi
katika nyakati ambazo kila asubuhi unasikia na kusoma habari mbaya, kuyumba kwa
uchumi, vita na majanga mbalimbali, ambayo kwa pamoja huleta hali ya kukata
tamaa na kujiona hatuwezi, kana kwamba hakuna tumaini; Lakini habari njema ni
kwamba, katikati ya vurugu za ulimwengu huu, unaweza kuchagua kuona tofauti;
kujiona kama Mungu anavyokuona.
Wakati
wa vita na tishio kwa taifa la Israeli kutoka kwa Goliati na majeshi ya Wafilisti,
kila mtu alikuwa amekata tamaa na kukosa tumaini, lakini Daudi alichagua
kujiona kama Mungu anavyomuona na mwisho wake ilikuwa ushindi mkuu kwake na kwa
taifa lake. (1 Samweli 17:33, 37, 45-47)
Wakati
wa tishio la Wamidiani, Gideoni alikuwa amejificha; Malaika akamtokea na
kusema, “Bwana yu pamoja nawe ee shujaa”. Bwana alikuwa pamoja naye; na alikuwa
anamuona na kumtambua Gideoni kama shujaa; Lakini Gideoni aliona Mungu hakuwa
pamoja naye (amemuacha) yeye na taifa lake, hivyo alijiona dhaifu na mtu asiye na msaada; ndio
maana alikuwa amejificha. Lakini ukweli
ni kwamba, changamoto alizokuwa nazo hazikuondoa ukweli na uhalisi wa kwamba
Bwana yu pamoja naye na kuwa yeye ni Shujaa (Waamuzi 6:2, 11-14, 16).
Changamoto zilizopo hazifuti wala kubadili msimamo na mtazamo wa Mungu juu ya
maisha yako.
Gideoni
hakufanywa shujaa wakati ule Malaika anamtokea, Malaika alimkuta Gideoni akiwa
shujaa; ndio maana alimsalimia ee Shujaa; alichofanya malaika sio kuondoa
changamoto za Wamidiani. Jambo la kwanza
alihitaji kubadili namna ambavyo Gideoni anajitazama; ili aanze kujiona kama
Mungu anavyomuona; ili aweze kuwa msaada kwa jamii yake pia. Naamini kabisa,
kama asingebadili mtizamo wake na kuanza kujiona kama Mungu anavyomuona; Mungu
angetafuta mtu mwingine wa kufanya naye kazi. Mpaka umejitazama kama Mungu anavyokutazama, kuna uwezekano mkubwa
changamoto ulionayo ikaendelea kuwepo.
Kuna watu
huomba na kusali kwa kushusha thamani yao kwa kujifananisha na vitu mbele za
BWANA. Kuomba na kusali kwa namna hii si sawa mbele za Mungu. Mungu ametufanya
kuwa watoto wake, warithi pamoja na Kristo Yesu (Joint heirs) na sisi ni matawi katika Mzabibu ambaye ni Yesu Kristo
yaani tunauzima ule ule ndani yetu alionao Kristo (kumbuka uhai uliopo kwenye shina la mti ndio uhai huo huo ulipo kwenye
matawi); Kwanini mtu ajione hana thamani mbele za Mungu aliyechagua kumvika
taji ya utukufu na heshima namna hii? (Zaburi
8:4-6). Sala za namna hii hazioneshi kiwango cha mtu cha unyenyekevu mbele
za Mungu, bali huoneshi kiwango cha ujinga (ukosefu wa maarifa) alicho nacho
mtu.
Mwimbaji
wa nyimbo za Injili, Sinach ameimba wimbo anasema “I know who I am (Ninajua/fahamu mimi ni nina)” swali
langu kwako, je unajua wewe ni nani? Je unajiona kama Mungu anavyokuona;
shujaa, mwana wa Mungu, mshindi, mwenye kuyaweza mambo yote katika Yeye,
unajiona kama Mkono wa Mungu uko upande wako, mrithi pamoja na Kristo?
Hakikisha unasikiliza vizuri wimbo wa mwanadada Sinach (unapatika youtube),
itakuwa ni mahali pazuri pa kuanzia.
See
you at the top
0 comments :