Uaminifu! Tabia gani bora kama hii?

11:37:00 AM Unknown 0 Comments


UAMINIFU! TABIA GANI BORA KAMA HII?
(Si vema kufanana na watu wa dunia hii)

Ilikuwa mchana wakati wa chakula na nilikuwa nikibadilishana mawazo na wafanyakazi wenzangu kutoka taasisi mbalimbali za Serikali. Mkononi mwangu kama ilivyoada nilikuwa na kitabu kizuri, “Money won’t Make You Rich” kilichoandikwa na mchungaji Sunday Adelaja.
Na mara rafiki mmoja akaniambia nimweleze kanuni za kumsaidia kufanikiwa kiuchumi, na mimi kwa haraka kama daktari fedha vile nikaanza kumweleza. Kanuni zote nilizomweleza zilikuwa zikikubaliana na neno Mungu. Mwishowe akazikataa kanuni zangu na akazitaja za kwake za kufanikiwa haraka ambazo ni, kuuza dawa za kulevya, meno ya tembo na ufisadi. Akasisitiza bila magendo huwezi kuwa tajiri.
Ndivyo walivyo watu wa ulimwengu, wanadai bila kuiba hakuna mafanikio, bila uasherati kabla ya ndoa hakuna ndoa wanasisitiza bila uchafu hakuna usafi. Ibrahimu, Ayubu na Daudi wote walikuwa matajiri katika Biblia na maandiko hayatuoneshi wizi au udanganyifu katika maisha yao, badala yake neno la Mungu linaonesha jinsi walivyokuwa waaminifu.
Mali ya mtu au ya serikali ni kipimo chako cha kuona kama unaweza kuaminiwa na kupewa mali yako mwenyewe. Siku za karibuni nimekuwa katika nafasi mbalimbali za kijamii na kikazi zinazoniwezesha kushika pesa za watu na za Serikali. Na kwa kweli nimekuwa mwaminifu, na Roho wa Mungu amekuwa akinitia moyo kwamba, ukiwa mwaminifu kwa mali ya mtu Mungu atakupa ya kwako mwenyewe, ukiwa mwaminifu katika pesa kidogo Mungu atakupa nyingi. Hujawahi  kuona wauzaji waaminifu huishia kumiliki mali na amana zao wenyewe. Mara nyingi imetokea sawa sawa na neno la Bwana. “Aliye mwaminifu katika lililo dogo sana, huwa mwaminifu katika lililo kubwa pia; na aliye dhalimu katika lililo dogo, huwa dhalimu katika lililo kubwa pia. Basi, kama ninyi hamkuwa waaminifu katika mali ya udhalimu, ni nani atakayewapa amana mali ya kweli” Luka 16:10-11
Kwa lugha nyingine kila unapoiba huwa unamwambia Mungu siko tayari kumiliki mali yangu mwenyewe. Vivyo hivyo kila unapozini na kusema uongo huwa unamwambia Mungu kwamba, “sifai kuwa tajiri.” Ni ukweli uliowazi maana kilichozungumzwa ni uaminifu ambao ni zaidi ya kutokuiba. Yusufu alipimwa uaminifu wake kwa kutaka kubakwa na mke wa Potifa. Kitendo cha Yusufu kukimbia na kukataa uovu huo kilituma ujumbe kwa Mungu kama huu, “Yusufu yuko tayari kuwa tajiri mpatie.”
Matajiri wengi wanafanikiwa kama kuku. Kuku akilishwa vizuri na kunawiri ni ili achinjwe. Matajiri wengi wako tayari kwa kuchinjwa. Utasikia amejinyonga, utasikia amechomwa kisu, utasikia amekufa kwa sababu ya kansa ya koo iletwayo kwa kupitia kuvuta sigara. They get rich only to die young!
Ni heri maskini mwaminifu kama Lazaro kuliko tajiri mwizi na fisadi. Dunia inadanganya inasema kipagani eti, ni sawasawa kuiba ili kuendelea, “The pagan society says,’ its okay, to lie, steal and cheat to get ahead’.” Uaminifu unazawadi yake, raha yake na fahari yake. Watu dhaifu na legelege hawawezi kuwa waaminifu, uaminifu ni haiba ya juu kabisa si rahisi kuipata kwa watu ambao hawajaunganika na Mungu.
Nakutakia msimu mzuri wa Krismas na mwaka mpya 2017, barikiwa tena Mungu na akuhifadhi daima.

0 comments :