Tazama zaidi ya uonanyo
TAZAMA ZAIDI YA UONAVYO
Watu
wanapokutana na ukinzani/changamoto
katika jambo, mambo mawili huweza kutokea; kukosa nguvu na ujasiri wa kuendelea mbele hadi kupata mpenyo, au kukosa
uvumili na hivyo kutafuta njia mbadala hata kama si salama ili kufikia
tamanio lake. Mtu wa namna hii huona changamoto kama mwisho au kikwazo cha
kufikia mafanikio yake. Mfalme Sauli alipokutana na Goliath, yeye na Israeli
yote isipokuwa Daudi walikosa nguvu na ujasiri wa kuendelea mbele [1Sam 17:11];
wakati Ibrahimu alipokutana na changamoto ya kupata mtoto, aliingia kwa
mfanyakazi wake kama njia mbadala ili kufikia matamanio yake, na gharama yake
ilikuwa kubwa.
Robert
H. Schuller, mwandishi wa kitabu cha “Tough
times never last but tough people do”, anasema “Tofauti ya mtu anayeshinda
na mtu anaishindwa katika changamoto [hiyo hiyo] wanayokutana nayo wote wawili
au mazingira hayo hayo, ni namna ambavyo watu hao wamechagua kulitazama jambo
hilo [Tafasiri ya mwandishi]”. Hivyo kumbe, namna ambavyo mtu anatazama au
kuchagua kuona jambo au changamoto iliyopo mbele yake ndio huamua hatima ya mtu
huyo katika jambo hilo; yaani kushinda au kushindwa kwake. [The ability to see beyond the situation is
the key to overcome the challenge/crisis].
Musa
alipokuta na vikwazo katika kuwakomboa wana wa Israeli kutoka katika utumwa wa Misri;
hakuona kama tatizo la kumrudisha nyumba, bali aliona nafasi kwa yeye kuona
Nguvu na Udhihirisho wa Mungu katika maisha yake na wana wa Israeli. Ndio maana
kila alipokutana na tatizo au changamoto alikimbilia mbele za Mungu, kwa kuwa
alijua ilikuwa ni fursa kwake ya kuona Ukuu wa Mungu; na kupitia ugumu wa
Farao, Mungu atukuzwe na watu wote wapate kujua kuwa Mungu Anaishi. Leo hii anajulikana kama mshindi [Kutoka
9:11, 29].
Wakati
kila mtu anamuona Goliath kama tatizo katika Israeli, Daudi alimuona Goliath
kama fursa ya kudhiirisha Ukuu na uweza wa Mungu; na ili dunia wapate kujua
yuko Mungu katika Israeli. Lakini pia kwake, aliona kama fursa kwa yeye kuoa mtoto
wa Mfalme bila kutoa mahari na mwanzo wa kuishi maisha bora, pia fursa kwa yeye
pamoja na familia yake kuishi huru [1Sam 17:25, 46-47]. Leo hii anajulikana
kama mshindi.
Mama
Teresa wa Calcutta, mshindi wa tuzo ya amani ya Nobel alipoona maskini na watu
wasio na msaada kule India; hakuona kama tatizo la kumkatisha tamaa, bali
aliona fursa ya kumtumikia Mungu kwa kugusa maisha ya watu. Leo hii anajulikana
kama mshindi.
Nimewahi
kusikia habari za mama mmoja ambaye alikuwa amempa Yesu maisha yake; na alikuwa
anafanyakazi katika kampuni fulani, lakini baada ya muda aliachishwa kazi;
akaenda kwa mchungaji wake analia, mchugaji wake akamuuliza kwanini alikuwa
analia!!!? Akamuuliza, “Je una kitu gani ambacho unaweza kufanya?” Yule mama
akamjibu kuwa anaweza kutengeneza keki tu. Baada ya mazungumzo na mchungaji
wake; akamuambia aende akatengeneze keki kisha apelekee pale alipoachishwa na
kuwagawia wafanyakazi wenzie bure kama sehemu ya kuagana nao; mara ya kwanza
hilo wazo halikuingia akilini mwa yule mama lakini akafanya kama alivyoambia na
mchungaji wake. Alipomaliza, wakati anarudi nyumbani, watu mbalimbali pale
ofisini wakamtafuta na kumuuliza kama anaweza kuwatengenezea keki kwa “oda”
maalumu, kwa kuwa keki zake ni nzuri. Baada ya muda kidogo yule mama alikuwa na
ofisi yake, akanunua mashine kubwa zaidi na kuajiri watu wengine katika ofisi
yake.
Mara
kadhaa tumesikia watu wakisema, “Tatizo sio tatizo bali tatizo ni namna ambavyo
mtu analitazama tatizo”; ukitafakari usemi huu utagundua kuna ukweli ndani
yake. Kumbe, hatua ya kwanza kwa mtu ili aweze kuvuka katika changamoto fulani,
ni kuangalia namna ambavyo analitazama jambo hilo vinginevyo mtu anaweza
kufanya kosa kama la Ibrahimu au kukubali kuwa dhaifu mbele ya changamoto kama
mfalme Sauli na wana Israeli . Wiki ijayo tutangalia mambo kadhaa ya kumsaidia mtu
aweze kuona zaidi ya anachoona ili kupata matokeo bora zaidi….
See you at the Top
0 comments :