Mungu Anakutazama

10:05:00 AM Unknown 0 Comments

MUNGU ANAKUTAZAMA
(Maovu na mema yote hutendeka mbele ya macho ya Mungu)
Katika tasnia ya michezo, wengi wetu tumezoea kucheza vizuri mahali ambapo mashabiki au watazamaji ni wengi. Si wachezaji wengi wanaweza kujituma na kucheza kwa bidii sirini. Wengi hupenda kucheza vizuri wakiwa wanatazamwa na maelfu ya mashabiki jukwaani. Si ajabu ndio maana viwanja kama Old Trafford na Stanford Bridge (viwanja vya soka) huchukua mashabiki wengi, na wachezaji hujiona wabarikiwa wakisakata katika nyasi hizo.
Lakini ni lazima tujue wazi kwamba, Mungu ni mkuu kuliko watazamaji, anaona ndani ya mioyo yetu na hata nafsini mwetu. Ufanisi wake katika kuyatazama maisha yetu ni mkubwa kuliko mamilioni ya mashabiki wasioweza kutazama mpaka moyoni. Mwenye hekima mmoja anasema, “You’re for an audience of one: GOD ” akimaanisha, “Tunaishi kwa ajili ya kusanyiko la mtazamaji mmoja; MUNGU.” Tunapaswa kulenga kumpendeza yeye na kumtukuza yeye peke yake ambaye kwa nyakati zote hutuona.
Ikiwa kusanyiko unalolenga kulipendeza ni la watu, basi uwe na hakika mwenendo wako utakuwa mbaya katika nyakati ambazo hawakuoni, na ikiwa unalenga kumpendeza Mungu mwenendo wako utakuwa safi nyakati zote. Mungu akiwa ndio kusanyiko lako, basi utaishi vema maana yeye anapatikana mahali kote, si uwanjani wala ukumbini tu; bali yuko nasi gizani na nuruni, asubuhi, mchana jioni hata usiku.
Kitendo cha Adam na Eva (kabla ya anguko) kuishi bila nguo, tena bila ya kuona aibu kilikuwa ni alama ya uaminifu na hali ya kuwa bila hatia mbele za Mungu. Hawakuwa na kitu cha kuficha mbele za Mungu, hawakusongwa na jambo lolote ambalo lingewafanya waone aibu mbele za Mungu. Mwanzo 2:25
Kundi kubwa leo tumekuwa na sura tatu, ile ambayo jamii inaijua, ile ambayo sisi na Mungu tunaijua, na ile ambayo Mungu peke yake huijua. Ni muhimu kuwa na sura moja isiyobadilika, ni vema kutokuwa vuguvugu tena ni muhimu kukataa unafiki ambao tafrisiri yake rahisi ni kuwa na sura nyingi (many faces).
Mtu mmoja alisifika sana ofisini ilhali nyumbani kwake hawakuwa na furaha naye kabisa, alikuwa mwema kwa watu wasio wake na aliwatesa walio wake. Sura yake ya nyumbani ilikuwa tofauti na u-malaika aliouonesha ofisini. Ni msemo wa kutisha na usiotakiwa, “saint at abroad and devil at home.” Yaani, “Mtakatifu akiwa mbali, shetani nyumbani.” Ni muhimu kutafuta sura moja, nyumbani na ugenini, usiku na mchana, chumbani na nje ya chumba.
Dhambi zote hutendeka mbele ya macho ya Mungu. Tafakari hili neno, mbele ya macho yake. Kila dhambi tutendayo tunamkosea Mungu peke yake. Maumivu ya dhambi humwelekea Mungu ndio maana kuna nyakati hushindwa kuvumilia. Usije fikiri hata mara moja kwamba, unajikosea au unamkosea jirani, mara nyingi tunapokosa tunamkosea Mungu. Unapomtendea jirani yako uovu unamtendea Mungu. Inatisha kwani mabaya yote hutendeka mbele ya macho yake.
Tafakari na kuchukua hatua, Mungu yuko tayari kusamehe nyakati zote.

0 comments :