Mara nyingi sana
(Saba mara sabini)
Wanaofuatilia
huduma ya Uinjilisti watakuwa wanamfahamu au kumsikia ndugu Jimmy Swaggart,
yeye hupenda kujiita brother Swaggart, ni mwinjilisti mwenye alama ya aina yake
na mwenye kutembea mwendo mrefu kwa miaka kadhaa katika huduma aliyopewa.
Ameonja kuanguka na kusimama na hapa anatoa funzo: “Msalaba wa Yesu kila siku
unatenda kazi kamwe haushindwi, ni mimi na wewe tunaoweza kushindwa. Sisemi
kama ikitokea ukianguka (maana utaanguka kweli) kama hautaacha kumwamini Yesu
hata katika anguko lako, Yeye Bwana Yesu hatakuacha na mwishowe atakusimamisha
maana hujaacha kumwamini hata katika kuanguka kwako.”
Kwa
tafsiri yangu Jimmy anasema, kuanguka kupo, ndio maana haoni sababu ya kusema
ikitokea ukianguka maana anajua itatokea. Katika huduma yake ameanguka na
kusimama, anajua machungu ya kuanguka, anasisitiza tusikate tamaa maana msalaba
wa Yesu unauweza wa kuokoa nyakati zote. Asubuhi moja nikiwa katika Studio za
Ileje Fm radio msikilizaji aliniuliza kama, Mungu anaweza kusamehe dhambi
kubwa. Nilimjibu, “Ndiyo anaweza, mara nyingi tu.” Si tu kwamba Mungu anasamehe
bali anasamehe mara nyingi. Many times!
Baadaye
nilimpa mfano tuliopewa na paroko kanisani kwetu, nanukuu: “mtu mmoja
alimuuliza padre mmoja akisema, ‘padri nimemuua bosi wangu, Je! naweza
kusamehewa? Padri akamjibu akasema, ‘unaweza kusamehewa bila shaka’ yule bwana
akaendelea akasema, ‘wakati nikimuua bosi wangu dereva wake aliniona, ili
kufuta ushahidi nikamuua na dereva je, naweza kusamehewa? Akamjibu ndiyo bila
shaka. Akamwambia, ‘Padri niwie radhi kwani, nilipokuwa nikimuua dereva mke wa
bosi aliniona ikabidi nimchinje na yeye pia. Vipi na hilo nalo Mungu anaweza
kusamehe? Padri akajibu ndiyo bila shaka.’”
Usikate
tamaa Mungu anaweza kukusamehe
haijalishi umefanya nini. Somo kuu la mfano hapo juu ni hili; Si kwamba Mungu
anaweza kusamehe tu, bali anaweza kusamehe mara nyingi zaidi.
Mungu
ni upendo. Maandiko yanasema upendo husitiri dhambi nyingi. Usipokata tamaa
Mungu hatakuacha, na hata ukikata tamaa yeye ataendelea kukutafuta maana wokovu
wako ni muhimu. Si sisi tuliomtuma mjumbe aende mbinguni kumshusha Yesu ili aje
atuokoe bali ni Mungu aliyemtuma Yesu ashuke kutuletea wokovu.
Kila
mtu anaweza kusamehe lakini si kila mtu anaweza kusamehe mara nyingi. Tabia kuu
ya kimungu (great godly character) haiko
katika kusamehe tu, bali iko katika kusamahe mara nyingi zaidi. Hata wapagani
kuna nyakati husamehe, lakini hawawezi kufanya hivyo zaidi ya mara saba. Mitume
walidhani, unaweza kusamehe mara saba tu, na kumbe ni zaidi ya hapo.
Msamaha
unaponya mahusiano, unaponya ndoa, unaponya kanisa na nchi kwa ujumla. Asiye
mfuasi wa msamaha ni mfuasi wa vita. Kuna wengine husema jino kwa jino, hili
linawezekana ikiwa tu aliyekukosea ni mdogo. Ikiwa unapenda kulipiza kisasi
badala ya kusamehe napenda kukuuliza, Je, utafanya nini ikiwa aliyekukosea
anazo nguvu kuliko wewe? Je, utafanya nini ikiwa aliyekukosea ni mkuu sana?
Naamini utamwachia Bwana maana, kisasi ni juu yake. Kama hatuwezi kusamehe
hatuwezi kumwachia Mungu, kwani tutaona kama vile Mungu hawezi kumwadhibu
vizuri mhusika. Jifunze kusamehe mara
nyingi zaidi, tamka msamaha sirini na hadharani pia, wewe uliyesamehewa makosa
yako unawezaje kushindwa kusamehe wengine? Mathayo 6:14-15
Leo ninakuachia kazi ya nyumbani (home work) ifuatayo, piga simu, tuma
meseji ya kusamehe na kama aliyekukosea yuko karibu mwambia nimekusamehe.
BARIKIWA
0 comments :