Enendeni mkabadilishe .....

3:18:00 PM Unknown 0 Comments


ENENDENI MKABADILISHE UTAMADUNI WAO
(Mbingu duniani)
 “Akawaambia, Enendeni ulimwenguni mwote, mkaihubiri Injili kwa kila kiumbe.” Marko 16:15
Wakristo wa sasa wanaogopa ulimwengu na mifumuo yake, ilhali BWANA ameagiza akisema enendeni ulimwenguni kote. Kanisa linalopatikana ulimwenguni ndilo kanisa lenye bidii. Kanisa lazima lipenyeze katikati ya mifumo ya kifedha, utawala, ulinzi, elimu, habari, sayansi, bunge na tasnia nyingine zote.
Kanisa limeokolewa ili likaokoe, ‘she was delivered to deliver’, wakristo hawapaswi kujifungia ndani bali wanapaswa kuonekana mitaani, misibani, redioni, magazetini, mashuleni, vyuoni na katika maeneo ya kazi wakimshuhudia Yesu kwamba, ni Kristo.
Jijini Dar-es-Salaam maeneo ya Tegeta kwa ndevu kuna mkusanyiko wa watu na pembezoni mwa ile barabara liko kanisa moja. Jioni watu wa kanisa lile hutoka nje na kuanza kuhubiri, na kwa kuwa kanisa lao liko karibu na soko na maduka injili yao husikiwa na wengi. Mkao wa lile kanisa [ingawa liko katika hifadhi ya barabara] unatufundisha sisi sote kama wanakanisa namna tunavyotakiwa kukaa kiroho kwa ushuhuda katikati ya jamii zetu. Kanisa halina tofauti na wamachinga katika kuenenda kwake kiroho lisikubali kwenda pasipokuwa na watu.
John Wesley ni moja ya wahubiri wa injili na wahudumu waliofanya kazi kubwa katika kumtangaza Yesu Kristo. Moja ya kauli zake alisema, “Naona Dunia yote kama parokia yangu.” Alikua na kiu ya kuinjilisha iliyomfanya asione mipaka iliyopo ulimwenguni. Unapotazama dunia kama parokia yako maana yake unajipa wajibu mkubwa wa kuwahudumia na kuwalisha kondoo wa BWANA. Cha kushangaza ni kwamba, wakati Wesley anapanga kuinjilisha dunia yote wengi hawana mpango wa kuinjilisha hata familia zao. Hawataki kujisumbua kupeleka ujumbe katika kijiji chao, shuleni aliposoma au katika jumuiya anayosali.
Yesu aliposema twende ulimwenguni alitaka utamaduni wa mbinguni uje duniani (Heaven on Earth). Agizo lake lililenga mapinduzi ya utamaduni. Alitaka wakristo waende katika sehemu tisa muhimu kwa kila taifa na kuweka sura ya injili katika nyanja hizo zote.
Kila taifa lina vitu (componentxs) vifuatavyo ambavyo ni kazi yetu kupeleka nuru katika maeneo haya:
  1. Familia -Ndiyo msingi wa kila jamii na taifa na ni mahali ambapo tunu huzaliwa. Utamaduni wa ki-kristo unapaswa uanzie hapa.
  2. Habari na mawasiliano - kazi yao ni kutangaza na kukuza tunu zilizokubaliwa na jamii ambayo msingi wake ni familia. Wakristo ni lazima wamiliki vyombo vya habari ama wawe watangazaji ili watangaze tunu za Kimungu. Kilichopo sasa ni vikaptura na miziki ya hovyo.
  3. Elimu - Hurithisha tunu na maarifa yaliyokubaliwa na jamii hiyo kutoka kizazi hadi kizazi. Mchungaji Oyadepo na Mesa Otabil wamefanya vizuri kwa kufungua vyuo vikuu ili maadili ya kikristo yajulikane kwa wanafunzi.
  4. Ulinzi na Usalama -Hulinda taifa na mifumo yake, mara nyingine majeshi yamewasaidia waovu kumiliki na kutawala. Ni kutokana na watu wa Mungu kutokuwepo katika nyanja hiyo.
  5. Dini - Kila taifa linafanya ibada. Wakristo wanamwakilisha Mungu wa kweli katika mataifa yao hivyo ni lazima Mungu wetu aheshimiwe kupitia sisi kama nyakati za Eliya. Gidioni alivunja sanamu za baba yake na Nabii Eliya aliwachinja manabii wa baali na baali hakuweza kuwatetea. Mungu wetu ni Mkuu kupita miungu yote.
  6. Bunge - Si tu kwamba bunge hutunga sheria bali wabunge pia hutunga yale wanayopendeza mbele za Mungu wao. Mfano mzuri ni suala la mahakama ya kadhi nchini Tanzania, kama idadi ya wabunge wakristo ingekuwa ndogo leo tungeongea lugha nyingine. Kuna umuhimu wa wakristo kuwa wabunge.
  7. Mahakama - Huhusika na utoaji wa haki. Katika ulimwengu huu wenye vitisho, rushwa na uchawi ni watoto wa Mungu tu ndio huweza kusimamia haki. Wana sheria wadhalximu ni wengi, vijana tusome sheria tukamtetee Yesu kisheria na kuwapa watu haki zao bila ya kuwabagua.
  8. Kazi na Biashara - Ndiyo siri ya utajiri ilipo. Watu hawaheshimiwi kwa upako tu, bali kazi pia huleta heshima. Hekima ya masikini hudharauliwa, wakristo wafanye kazi (halali); wawe matajiri, wakitumia mali zao kusukuma gurudumu la injili. Luka 8:3
  9. Sayansi na Teknolojia - Ndiyo uwanja au jukwaa la kisasa. Zamani tulikutana uwanjani leo hii mamilioni ya watu wanakutana katika mitandao ya kijamii. Huwezi kuinjilisha kwa ufanisi wa juu kabisa ikiwa unachukia facebook na twitter. Kanisa linatakiwa liende ulimwengu uliko, leo hii vijana wengi wako mixtandaoni, kanisa halinabudi kuwafuata huko na kuwasaidia. Kanisa linapaswa liwe la kisasa ili liwainjilishe watu wa sasa kwa njia za sasa.  
WITO:
Wakristo wakikaa katika Nyanja hizo tisa utamaduni wa dunia hii utapotea na ule wa mbinguni utachukua nafasi. Ukiwa ni mkristo na uko katika vyombo hivi ujue cha kwanza kwako si mshahara bali ni ufalme wa Mungu na haki yake. Wakristo mjitokeze katika kuanzisha na kumiliki vyuo vya elimu na vyombo vya habari.
Life Minus Regret team inakutakia mwaka wenye Baraka zote kutoka kwa BWANA 2017.

0 comments :