Jitazame kama Mungu anavyokutazama

11:38:00 AM Unknown 0 Comments

JITAZAME KAMA MUNGU ANAVYOKUTAZAMA 
Sehemu kubwa ya maisha ya mtu huathiriwa (influenced) sana na namna anavyojitazama. Mara nyingi, mtazamo wa mtu juu ya maisha yake na nafsi yake huamua hatima yake. Mtu anayejitazama kama aliyeshindwa (failure) katika jambo fulani; hakuna namna ataweza kushinda au kufanikiwa katika jambo hilo. Hakuna mtu aliyeweza kwenda mbali zaidi ya mtizamo wake (jinsi aonavyo nafsini mwake). Kumbuka, Jinsi ujitazamavyo, ndio kikomo chako.
Suleimani, Mwenye hekima wa kale na kiongozi wa taifa la Israeli  amewahi kusema, “Maana aonavyo (mtu) nafsini mwake ndivyo alivyo”.  Akiwa na maana kwamba, kiwango na aina ya maisha anayoishi mtu ni matokeo ya namna mtu huyo anavyoona nafsini mwake. Kama mtu haridhishwi na aina ya maisha anayoishi au kiwango cha maisha anayoishi, hatua ya kwanza kabisa sio kubadili kazi au biashara; bali kuangalia na kubadili fikra na mtizamo wake uliomfikisha mahali alipo. Ndio maana wataalamu wa sayansi ya fedha wanasema, mtaji wa kwanza kwa mtu sio fedha bali wazo (mtizamo/fikra) jipya.
Tunaishi katika nyakati ambazo kila asubuhi unasikia na kusoma habari mbaya, kuyumba kwa uchumi, vita na majanga mbalimbali, ambayo kwa pamoja huleta hali ya kukata tamaa na kujiona hatuwezi, kana kwamba hakuna tumaini; Lakini habari njema ni kwamba, katikati ya vurugu za ulimwengu huu, unaweza kuchagua kuona tofauti; kujiona kama Mungu anavyokuona.
Wakati wa vita na tishio kwa taifa la Israeli kutoka kwa Goliati na majeshi ya Wafilisti, kila mtu alikuwa amekata tamaa na kukosa tumaini, lakini Daudi alichagua kujiona kama Mungu anavyomuona na mwisho wake ilikuwa ushindi mkuu kwake na kwa taifa lake. (1 Samweli 17:33, 37, 45-47)
Wakati wa tishio la Wamidiani, Gideoni alikuwa amejificha; Malaika akamtokea na kusema, “Bwana yu pamoja nawe ee shujaa”. Bwana alikuwa pamoja naye; na alikuwa anamuona na kumtambua Gideoni kama shujaa; Lakini Gideoni aliona Mungu hakuwa pamoja naye (amemuacha) yeye na taifa lake, hivyo  alijiona dhaifu na mtu asiye na msaada; ndio maana alikuwa amejificha. Lakini ukweli ni kwamba, changamoto alizokuwa nazo hazikuondoa ukweli na uhalisi wa kwamba Bwana yu pamoja naye na kuwa yeye ni Shujaa (Waamuzi 6:2, 11-14, 16). Changamoto zilizopo hazifuti wala kubadili msimamo na mtazamo wa Mungu juu ya maisha yako.
Gideoni hakufanywa shujaa wakati ule Malaika anamtokea, Malaika alimkuta Gideoni akiwa shujaa; ndio maana alimsalimia ee Shujaa; alichofanya malaika sio kuondoa changamoto za Wamidiani. Jambo la kwanza alihitaji kubadili namna ambavyo Gideoni anajitazama; ili aanze kujiona kama Mungu anavyomuona; ili aweze kuwa msaada kwa jamii yake pia. Naamini kabisa, kama asingebadili mtizamo wake na kuanza kujiona kama Mungu anavyomuona; Mungu angetafuta mtu mwingine wa kufanya naye kazi. Mpaka umejitazama kama Mungu anavyokutazama, kuna uwezekano mkubwa changamoto ulionayo ikaendelea kuwepo.
Kuna watu huomba na kusali kwa kushusha thamani yao kwa kujifananisha na vitu mbele za BWANA. Kuomba na kusali kwa namna hii si sawa mbele za Mungu. Mungu ametufanya kuwa watoto wake, warithi pamoja na Kristo Yesu (Joint heirs) na sisi ni matawi katika Mzabibu ambaye ni Yesu Kristo yaani tunauzima ule ule ndani yetu alionao Kristo (kumbuka uhai uliopo kwenye shina la mti ndio uhai huo huo ulipo kwenye matawi); Kwanini mtu ajione hana thamani mbele za Mungu aliyechagua kumvika taji ya utukufu na heshima namna hii? (Zaburi 8:4-6). Sala za namna hii hazioneshi kiwango cha mtu cha unyenyekevu mbele za Mungu, bali huoneshi kiwango cha ujinga (ukosefu wa maarifa) alicho nacho mtu.
Mwimbaji wa nyimbo za Injili, Sinach ameimba wimbo anasema “I know who I am (Ninajua/fahamu mimi ni nina)” swali langu kwako, je unajua wewe ni nani? Je unajiona kama Mungu anavyokuona; shujaa, mwana wa Mungu, mshindi, mwenye kuyaweza mambo yote katika Yeye, unajiona kama Mkono wa Mungu uko upande wako, mrithi pamoja na Kristo? Hakikisha unasikiliza vizuri wimbo wa mwanadada Sinach (unapatika youtube), itakuwa ni mahali pazuri pa kuanzia.
See you at the top

0 comments :