Jina lako nani?

1:14:00 PM Unknown 0 Comments


JINA LAKO NANI?
( Unajionaje nafsini mwako )
Zamani tulifuga mbwa na tuliwita jina kaburu, tulitaka awe mkali kama wale makaburu wa Afrika ya kusini. Makaburu hawakuwa na sifa njema, waliwatesa sana watu weusi kule nchini Afrika kusini. Waliwatendea kwa ukali na kwa ukatili mkubwa na hata kuwaua.
Mbwa yule alikuwa mkali sawa sawa na jina lake, alipokwenda kung’ata hakupiga kelele aling’ata kimya kimya. Mbwa yule alituletea kesi kadhaa za kuuma watu nyakati za asubuhi. Iko nguvu ya ajabu katika jina na katika namna unavyojiona wewe mwenyewe. Mtu hufanana na namna anavyojitazama ndani yake.
Unapoitwa jina lenye kukupinga au lenye kuashiria ulegevu na laana unapaswa kulikataa, au kuwa na mtazamo mpya ndani yako ili maisha yako yafanane na jina lako. Ukiitwa jina Shida, Mwadawa, Maganga, Sikitu, Lameck na majina mengine yafananayo na hayo ni lazima uyakatae na kuchagua jina jema. Hata kama watu wasiojua wataendelea kukuita kwa majina mabaya lakini tayari ndani yako utakuwa unajua wewe ni mtu tofauti. Utakuwa unajua wewe ni hodari, wewe ni tariji, wewe ni taifa takatifu na tena ni mtu wa mafanikio.
Moja ya watu wanaofanikiwa sana katika utawala ni wale wenye majina ya Benjamini tafsiri ya hili jina ni, mtu wa mkono wa kuume au kwa lugha nyingine ni mtu mkubwa. Mimi nawafahamu Benjamin wachache tu ambao walifanikiwa kuwa watu wakuu, Benjamin Mkapa alikuwa Rais wa Tanzani, Benjamin Franklin aliongoza huko Marekani na hata sasa Benjamin Natanyahu anaongoza huko Israel.
Wakati wa kuzaa kwake Raheli mke wa Yakobo alishikwa na utungu mkuu, na katika kujifungua kwake huko alifariki. Ikawa wakati wa kutoa roho yake alimwita mtoto wake jina Benoni, maana yake mwana wa uchungu wangu lakini Yakobo babaye alikataa asiitwe Benoni akasema aitwe Benjamini maana yake, mtoto wa mkono wangu wa kuume (mtawala) na tazama Benjamin alikuwa mtu mkubwa. Mwanzo 34:18
Na Yakobo anapombariki Benjamin anamfananisha na mbwa mwitu, mtu imara na mwenye nguvu ya kutafuta asubuhi na usiku, mtu asiyeishiwa chakula. Ninaamini kama angeliitwa Benoni asingeliweza kuwa shupavu na mwenye akili kama namna alivyokuwa. Mwanzo 49:27
Kabila la Benjamin lilikuwa na heshima na umahiri mkubwa (brave and active) kwa kuwa liliambiwa litaketi mkono wa kuume ambao ni mkono wa heshima kuliko kushoto (Zaburi 80:17). Ni kabila lililopigana vita mara nyingi na kushinda na kujitwalia nyara kama mbwa mwitu anayejitajirisha kwa vitoweo. Kila kilichonenwa katika jina la Benjamini, kilitokea katika kabila la Benyamini. Watu wake walikuwa hodari na watawala wenye nguvu vitani. Sauli na Yonathani mwanaye moja ya viongozi na mashujaa kutoka katika kabila la Benjamin na wasomaji wa Biblia wanajua jinsi walivyokuwa watu hodari kwa vita na katika uongozi. {1Samweli 9:1, Waamuzi 20:21-25, 3:15, 5:14,}
Wewe ni mtu muhimu sana katika kujenga Ufalme wa Mungu hapa duniani. Jina lako linabeba lile kusudi (mission) ambalo Mungu alilokuumbia ulitekeleze. Chunguza maana ya jina lako.  Kataa maana mbaya zote za jina lako, litakase kwa damu ya Yesu na nenea mazuri jina lako.

0 comments :