Laiti kila mwenye dhambi angalitambua hili
LAITI KILA MWENYE DHAMBI ANGELITAMBUA HILI!
[Wana ujumbe nusu na hivyo hauleti maana kamili]
Kila
mwenye dhambi anajua fika kwamba yeye ni mwenye dhambi. Kujua kwamba tuna dhambi haitoshi, lazima
tujue kwamba, Mungu yuko tayari kutusamehe. Kujua kwamba, unadhambi kunaleta
uchungu lakini kujua kwamba, Mungu yuko tayari kusamehe kunaleta amani ikiwa
utalifanyia kazi wazo hilo. Kama kila mdhambi angelijua hilo angeliomba toba
mapema.
Mungu
hafanyi maandalizi ili ajiweke tayari kusamehe bali yuko tayari hata sasa
kusamehe. Laiti kama kila mwenye dhambi angelijua hili, wengi wangetubu, shida
yao wana ujumbe nusu, wanajua wazi ni wenye dhambi, bali hawajui kama Mungu yuko tayari kusamehe.
Yohana
8:1-8 inaeleza, nyakati zile Mafarisayo walipomkamata [mfumania] yule mwanamke
katika zinaa walimpeleka mbele za Yesu wakiwa na wazo la kumpiga kwa mawe mpaka
kufa kama ilivyokuwa katika sheria ya Musa. Lakini Yesu aliposema, “asiye na
dhambi na awe wa kwanza kumtupia jiwe”, biblia inasema, wote waliokuwa pale
kuanzia watoto wadogo mpaka wazee walishtakiwa mioyoni mwao, ikiwa na maana
mioyoni mwao walishuhudiwa kwamba, wao pia ni wenye dhambi. Hakuna mwenye
dhambi asiyejua kwamba yeye ni mwenye dhambi. {Yohana 8:7-8}
John
Newton mtunzi wa wimbo maarufu duniani, ‘amazing grace’ anasema, “nijualo mimi
ni hili, mimi ni mwenye dhambi mkuu, na Yesu Kristo ni Mwokozi mkuu”. Anajua
yeye ni mwenye dhambi na anaifahamu na tiba pia. Hakuna mwenye dhambi asiyejijua wala
asiyeijua hukumu yake. Imeandikwa: “Maana neno hili
mnalijua hakika, ya kwamba hakuna mwasherati wala mchafu wala mwenye tamaa,
ndiye mwabudu sanamu, aliye na urithi katika ufalme wa Kristo na Mungu.” Waefeso 5:5
Paulo
anasema, neno hilo tunalijua hakika, tunafanya tunachokijua, tunajua madhara
yake na hasara zake tunazijua pia. Je, ni nani hajui kama Mungu anachukia wizi,
udhalimu, uchafu na ubaya wote? Bila shaka sote tunajua.
Yesu
aliposema asiye na dhambi na awe wa kwanza kumtupia mwanamke huyu jiwe, biblia
inasema wote walisutwa nafsini mwao yaani, hakusalia hata mmoja asiyekuwa na
dhambi wala ambaye hakujua kwamba anadhambi. Kumbe kila mwenye dhambi anajua
anazo lakini hataki kuzipeleke kwa Yesu, maana hata hawa baada ya kushtakiwa
mioyoni mwao hawakumwendea Yesu, badala yake waliondoka zao wakamwacha Yesu na
yule mwanamke.
Ni
muda muafaka sasa tumejua kwamba tunadhambi na tunachukua uamuzi wa busara wa
kuzipeleka mbele za BWANA badala kukimbia au kuendelea kukaa nazo kama
walivyofanya wayahudi hawa. Mungu yuko tayari kusamehe muda wote ungalipo hai,
Mungu ni wa rehema na ni mwenye huruma nyingi; hatamdharau mtu mwenye dhambi
atubuye, wala hawezi kumwacha aliyeumizwa katika ukosaji. Napenda kukualika leo
mwendee kwa kusema maneno haya: “Ee BWANA uniwie radhi mimi mwenye dhambi,
nimejua makosa yangu na nimejua wokovu wako. Unioshe kwa damu yako na unioneshe
na wokovu wako leo. Amina”
Aksante
kwa kuja na kushiriki katika msimu wa nne [4] wa weekend of purpose, makala
zijazo tutakujuza mafundisho yatokanayo
na weekend of purpose kwa uchache.
0 comments :