Wote wametenda dhambi

6:17:00 PM Unknown 0 Comments


WOTE WAMETENDA DHAMBI
(“kwa sababu wote wamefanya dhambi, na kupungukiwa na utukufu wa Mungu;” Rum 3:23)
Biblia inasema, wote, haisemi kabila fulani au nchi fulani tu ndiyo imetenda dhambi. Hakuna kabila wala nchi ya wenye dhambi, sote tumetenda dhambi. Kupitia dhambi ya Adam makabila yote, wanadamu wote na nchi zote ziliingizwa katika hali ya dhambi. Hapa hakuna wa kumbagua mwingine.
Nimewahi kusikia watu wakibaguana kikabila wakisema usioe kule na wengine wakidai usiolewe katika kabila lile. Kigezo chao ni dhambi ambazo hata wao na nchi zao, na jamaa zao wanatenda. Katika agano jipya tunapata makundi mawili tu ya watu, waaminio na wasio amini. Biblia inasema, waaminio wataokoka na wasio amini wamekwisha hukumiwa. Imani ndiyo kigezo cha kuungana na mtu fulani au kutokuungana naye.
Nadhani mstari huu ni mstari ambao haujaeleweka miongoni mwa wengi. Sote tuliumbwa kwa sura na mfano wa Mungu ambao kwangu mimi nasema sura hiyo ni utukufu. Biblia inasema, wametenda dhambi na kupungukiwa na utukufu; kwa hiyo sura ya Mungu ambayo ni utukufu wake katika maisha yetu ilipungua kwa sababu ya dhambi. Rum 3:23
Kuna mtazamo wa kuitazama nchi ya Israeli kama bora kuliko nyingine, na wengine hudhani kwamba, ni Baraka kwenda Israel jambo ambalo si kweli kabisa. Wakristo hatuna hija ya kusafiri bali ya imani katika Yesu Kristo. Israel kama taifa hawakumkubali Yesu na ndio sababu iliyomfanya Mungu aachane na wito wa ngazi ya taifa na kuelekea kwa ngazi ya mtu binafsi kama yanenavyo maandiko, “bali wote waliompokea…” Yohane 1:12
Je, unataka kuungane na mtu? Je, unataka kuwa na uhusiano na mtu kibiashara? Unataka kumdhamini mtu? Kigezo si kabila ya au rangi yake, bali unapaswa kuangalia kama ni mmoja kati ya wale wamwaminio Yesu Kristo au lah! Biblia inasema, “Tusifungiwe nira isivyosawasawa na mtu asiye amini.” Inakataza kuunganishwa au kuungana isivyo faa na mtu asiye amini.
Badala ya kunyoosheana vidole ni vema wote tungefika alipofika John Newton yule mwandishi wa wimbo wa, ‘amazing grace’ aliyesema, “Ninachojua mimi ni mwenye dhambi mkuu, Na Yesu Kristo ni mwokozi mkuu.”
Kama unaamini Yesu alikufa kwa ajili yako basi ni muhimu pia uamini ulikuwa uu, mwenye dhambi, kama usingelikuwa na dhambi asingekufa kwa ajili yako. Nina amini hakuna aliyezaidi ya mwingine kikabila, kimataifa wala kiukoo, sote tumetenda dhambi na kupoungukiwa na utukufu na hivyo tunamuhitaji Yesu Kristo, Great Saviour!  Mpaka wiki ijayo shallomu.

0 comments :