Nani analeta maana...!
NANI ANALETA MAANA KATIKA MAISHA
YETU
(Mungu ndiye huleta maana katika maisha ya mwanadamu)
Siku
moja nilisoma mtandaoni mtu ameandika kiboko ya wachungaji wenye walinzi
binafsi (board guards) ni hii Zaburi ya 127:1-2, nikacheka sana. Ninachoweza
kuandika ni kwamba, hata kama wanadamu wanahusika Mungu lazima ahusishwe
pia. Imeandikwa, “1. Bwana
asipoijenga nyumba Waijengao wafanya kazi bure. Bwana asipoulinda mji Yeye
aulindaye akesha bure. 2. Kazi yenu ni
bure, mnaoamka mapema, Na kukawia kwenda kulala, Na kula chakula cha taabu;
Yeye humpa mpenzi wake usingizi.”
Tafsiri ya huo mstari ni kwamba, usiingie
kwenye mradi (project) ambao Mungu haufanyi. Usiwekeze nguvu zako mahali ambapo
Mungu hawekezi. Usilinde asipolinda, ukisikia analinda basi hapo na wewe
kalinde. Kwa lugha nyingine ni kwamba, fanya pamoja na Mungu. Shirikiana na
Mungu katika kazi zako, Do not try to
work alone! Ukishaona Mungu hayumo katika mchakato fulani lazima ujue
matokeo yatakuwa sifuri. Magumu na mabaya yaliyowapata Adamu na Eva yalitokana
na kutengana na Mungu. Hata asingewalaani kwa kinywa chake bado matokeo ya kazi
zao na maisha yao ingekuwa ni sifuri. Alama ya juu unayoweza kuipata unapotenda
jambo bila ya Mungu ni sifuri (bure). Petro alionja sehemu ya laana ya hawa wazazi wa kale yaani, Adamu na Eva baada
ya kukesha usiku kucha katika uvuvi na kuambulia sifuri. We need Jesus! Luka 5:5
Zamani
niliona nembo (logo) ya shule moja imeandika, Life – Jesus = 0 yaani, maisha bila Yesu ni sifuri. BWANA Yesu
ndiye anayeleta maana ya michakato yote ya maisha yetu. Mfumo wetu wa elimu
bila Yesu ni bure, mfumo wetu wa ulinzi bila Yesu ni bure. Kazi bila
Yesu ni sifuri, utajiri bila ya Mkono wa BWANA ni sifuri pia. Hakuna jambo
ambalo linamuhusu mwanadamu ambalo Mungu hataki kushiriki. Kwa kuwa linamhusu
mwanadamu linamhusu Mungu pia. Yesu alikwenda harusini kana ya Galilaya (Yohana
2), Yesu alikwenda msibani Lazaro alipokufa (Yohana 11), Yesu alikwenda kazini
kwa Petro ambapo ni baharini kwa kuwa alikuwa mvuvi. Yesu alikwenda kushinda
nyumbani kwa Zakayo na mara nyingine kwa Martha na Mariamu.
Ingawa
kanisa lilikabidhiwa kwa Petro bado Kristo ndiye alikuwa mjenzi. Alimwambia,
“Na juu ya mwamba huu nitalijenga kanisa langu” yaani, mjenzi ni Kristo (Mathayo16:18).
Neno nitalijenga linaonesha wazi si Petro ambaye atajenga bali ni Yesu
aliyemmiliki wa kanisa ndio atakayejenga; maana anasema, na juu ya mwamba huu (Petro)
nitalijenga kanisa langu. Anahusika na furaha na huzuni zetu, anahusika na
taaluma na siasa zetu. Ni BWANA wa watu wote tena ni BWANA wa vitu vyote. Nadhani unafahamu mwenye
nyumba anaweza hata asishike tofali lakini kwa kuwa ndiye aliyenunua kila kitu
na ndiye anayetoa vitendea kazi huhesabika kuwa anajenga. Utasikia najenga huko
mbezi au Madale. Anayetoa nguvu, vitendea kazi, ramani na maelekezo ndiyo mjenzi.
Kristo ndiye mjenzi wa Kanisa wala si mtume, nabii, mchungaji wala kasisi.
Tunapotenda
tukiwa na Mungu matokeo huwa makubwa na kazi huwa nyepesi kama usingizi. Tukiwa
na Mungu tunaweza kupata matokeo makubwa (Big
Results Now BRN); maandiko husema, “Yeye huwapa wapenzi wake usingizi.” Ni
kama Petro alivyopata matokeo makubwa baada ya kutii, Utii wetu kwa Kristo ni
mwisho wa laana. Hakuna hukumu wala laana kwa waliondani ya Kristo. Luka 5:5
Paulo
anasema kuishi kwake ni Kristo, vipi wewe? Kuishi kwako ni anasa, ulevi au ni
kazi yako? Kuishi kwako ni mumeo au
rafiki yako wa kiume au wa kike? Ni pale tu ambapo kuishi kwako ni Kristo ndipo
uko salama. Ni rahisi kusema kuishi kwako ni Kristo kwa kuwa unalijua andika,
lakini je, Kristo ndio maisha yako? Mpaka
umekubali kuishi kwako kuwe Kristo, maisha yako hayataleta maana. Kuishi kwetu
ni bure ikiwa tuko nje ya Kristo. Flp 1:21
Tafakari
na acha maisha yako yalete maana kwa kujitoa kwa Yesu.
0 comments :