ONGEZA
MAARIFA KATIKA ENEO MAALUMU
Kama ilivyo kawaida, mwanzoni mwa mwaka
kila mtu anaweka malengo yake au mambo anayotaka afanikiwe au afanikishe katika
kipindi cha mwaka huo. Pamoja na kwamba si kila mtu ana utaratibu wa kuandika
malengo yake ya mwaka, lakini karibu kila mtu huwa na malengo au mambo
analiyopanga kufanikisha katika mwaka. Nafahamu
baadhi yetu tumeweka malengo ya kusoma vitabu katika mwaka huu mpya (kama
hujaweka lengo la kusoma vitabu, basi hujachelewa kufanya hivyo), hili ni jambo
jema kwa kila mwenye uwezo wa kusoma.
Pamoja na mipango na malengo yako mengi
uliyojiwekea kwa mwaka huu mpya, leo nataka nikupe hamasa juu ya jambo moja,
nalo ni kuweka nia au malengo ya kuongeza maarifa/ujuzi na ufahamu katika eneo mahususi au maalumu katika maisha yako.
Yaani badala ya kuweka lengo la kusoma tu, weka pia ni eneo gani unalotaka
kuongeza ujuzi au maarifa ili kuliboresha.
Mwenyehekima mmoja amewahi kusema "Usishibishe
njaa yako, shibisha maono yako [don’t feed your hunger, feed your vision]";
huu ni ushauri mmoja wa hekima ambao nimewahi kuupata kuhusu usomaji katika
kuishi kwangu. Lengo hapa ni kukuepusha na tabia ya kusoma kila kinachokuja
mbele yako bila malengo mahususi wala mpangilio utakao kusaidia kupiga hatua
zaidi katika maisha ya kila siku. Mtu anaweza kupanga mwaka huu nataka nisome
vitabu 30 au 20, lakini ukimuuliza unataka kusoma kuhusu nini au kuhusu eneo
gani, ni wachache sana wanamajibu yanayoeleweka (concrete answer)
Ili kusoma kwetu kulete badiliko katika
maisha yetu na mazingira tuliyopo ni muhimu ukachagua cha kusoma ukilenga
kuboresha eneo mahususi katika maisha yako. Na hapa utapata fursa ya kufanya
tathmini kuona kama unasogea, na kama kusoma kwako kuna kuletea faida inayoweza
kupimwa [measurable results].
Kumbuka, huwezi kusoma vitabu vyote
vilivyoandikwa, hivyo basi lazima ujue nini cha kusoma na nini cha kuacha hata
kama kina sura nzuri, ili mwisho wa mwaka useme kwa kusoma vitabu au kwa
kujifunza ujuzi fulani nimepiga hatua hii; kiuchumi, kiroho, mahusiano, ufanisi
kazi, huduma, ubora wa kazi zangu n.k
There’s a place for you at the Top
ROHO YA BATROMAYO KIPOFU
“ONA FURSA”
Batromayo aliona watu kama miti. Watu wengi
wanasumbuliwa na roho hii hawaoni picha halisi, picha yao haijatulia. Ni kama
vile ungo wao wa kudakia mawimbi haujatulia, hawapati picha halisi. Ni muhimu
sana mwaka huu 2018 sote tumuombe Mungu afungue macho yetu tuweze kuona fursa!
Kwa uzoefu mdogo nathubutu kusema, “fursa
haziwezekani bila imani”. Macho ya mwili hayotoshi, ile kwamba macho yetu
yanaona taa za barabarani na tunavuka salama haina maana kama tunaona fursa
pembezoni mwa barabara. Mtu anayeweza kufikiri kimkakati “strategic thinking”
anaweza kuona fursa na kuzitumia. Kufikiri kimkakati kutakuwezesha uone miaka
kumi ijayo na zaidi.
Kwa kukosa imani watu hauza mambo ambayo
baadaye yangekuwa fursa kubwa, kwa uhaba wa imani watu huogopa kuanza jambo
ambalo halijazoeleka. Anayewekeza miaka mia moja ijayo anaamini kwamba, Mungu
atamlinda na kumpa uhai, ndani yake mtu huyo hamna hofu ya kifo. Fursa inataka imani katika sura tatu,
kwanza mwamini Mungu muumba wako, jiamini na kisha amini wazo lako. Adui mkubwa wa fursa ni hofu, uwekezaji
unakwenda na ujasiri.
Zamani walituambia, “wasiwasi ndio akili”
si kweli. Nenda msituni utagundua mnyama mfalme wa msitu ni simba ambaye ni
mnyama jasiri. Njoo duniani utagundua mataifa makubwa yana ujasiri mkubwa pia. Alisema msemaji wa Marekani wa mambo
ya nje wakati huo John carry, “Dola ya Washington haitatikisika” alisema hayo
kwa ujasiri sana akionya taifa moja alilolitazama kama adui. Hatuna sababu ya
kuogopa amesisitiza Shiv Khera katika kitabu cha, Unaweza Kushinda: “Losers want security, winners seek
opportunity. Losers more afraid of life than death…”.
Tunawezaje kuona fursa? Maana kama
hatukuijua fursa kabla ya kukutana nayo, siku ikitokea tutaiona kama mkosi. Lazima
ujifunze kuhusu fursa na uzifahamu ili siku ukikutana nayo uitambue kirahisi.
Wewe si tajiri ila jitahidi usome kuhusu utajiri. Leo wewe si mfanya biashara
lakini jitahidi kusoma na kujifunza kuhusu biashara. Soma wasifu wa wafanya
biashara kama; Mohamed Dewji, Warren Buffet, Reginard Mengi, Ratan Naval Tata,
Alhaji Dangote, Said Bakhresa na wengine wenye ushawishi kwako.
Watu wengi wanapenda kushinda ila ni
wachache tu ambao wanapenda maandalizi kwa ajili ya kushinda. Fursa zinakutaka
ufanye maandalizi. Wewe ndiye unapaswa kuisubiri fursa kwani fursa haina nafasi
ya kumsubiri mtu! Fursa huja kwa waliojiandaa. Preparation is the Key!
Sala: Ee Mungu Baba Muumbaji wetu,
utufungue macho ili mwaka huu 2018 sote kwa umoja wetu tuweze kuona fursa.
Katika Jina la Yesu Nimeomba. Amina.
Usisite kutuandikia kwa anuani yetu kwa
maoni, ushauri na maombi. Barikiwa!
BIBLIA
INAMAJIBU YOTE
ISOME!
Ni
mwaka mpya sasa nuia idadi ya vitabu unavyopaswa kusoma mwaka 2018, zaidi ya
yote usisahau mpango wa kusoma Biblia, yearly bible reading plan! Tatizo la
kutokusoma linaendelea kuwatesa watu wa leo, kizazi hiki hakijajijengea tabia
ya kujisomea. Majibu mengi ya matatizo yetu yanayotukumba katika maisha ya kila
siku yako katika vitabu, bahati mbaya hatusomi.
Hivi
karibuni nikiwa naelekea Bagamoyo kwenye daladala nilifarijika baada ya mtoto
wa miaka kumi kuingia ndani ya gari na kisha kutoa kitabu na baada ya mwendo
kidogo akaanza kusoma. Nilitamani kupiga naye picha (selfie) kwa furaha, kuona
utamaduni ninao upenda umejengeka kwa mtoto yule. Miji na majiji yenye foleni
hutoa fursa kwa watu kujisomea wakiwa barabarani. Nyumbani utasema watoto
wasumbufu barabarani je? Furaha tunayoikosa vijiweni iko kitabuni, nguvu
tunayoikosa pahala pa kazi iko vitabuni, knowledge is power!! Mwenye maarifa
mengi ni mwenye nguvu nyingi hili halipingiki. Kile ambacho baba yangu hakusema
vitabu vimeniambia, kile ambacho dini ilinificha vitabu vimeniweka bayana. What a royal friend!
Nakushauri
usome vitabu, lakini soma zaidi Biblia. Katika neno la Mungu kuna umilele wote.
Yesu akasema, “ninyi mmekuwa safi kwa sababu ya lile neno mliliosikia”. Lile
neno la Mungu unalosikia linafanya unakuwa safi mwili na roho.
Neno
la Mungu limebeba majibu ya hali unazopitia wewe binafsi na Taifa lako pia. Unapotazama
uchumi wako na hali ya taifa lako usiende tu kwa kutumia elimu ya uchumi ya
darasani, ni muhimu utazame kiroho pia. Ukiona hali ngumu ya uchumi kwenye nchi
jiulize Mungu anataka nini kwa taifa lako, inawezekana kabisa anataka toba. Badala
ya kwenda kuchukua shahada ya uzamili ya uchumi mara nyingine ni muhimu kusoma
Biblia mfululuzo. Daniel kwa kusoma maandiko (neno la Mungu) aligundua nini
kinaendelea kwenye taifa lake.
Jifunze
kujua chanzo, anayejua chanzo halalamiki sana. Taifa linapopewa mtawala mkorofi
ni lazima ujue kuna mahali dhambi ilitendeka katika Taifa hilo na Mungu
amemweka mtawala huyo kwa makusudi yake ili watu wake watubu na kurejea. Katika
hali kama hiyo kufanya kazi kwa bidii hakutasaidia ila toba ya kweli kwa
wateule wote wa Mungu walioko kwenye taifa hilo inaweza kuleta suluhisho.
Moja
ya njia kuu ambayo Mungu amekuwa akiitumia kuzungumza na nchi na watu binafsi
ni hali ya uchumi. Ukiaona kuna mvua ya kutosha, tena kwa wakati wake ni lazima
ujue kuna kitu kizuri Mungu anazungumza, ukiona ukame na watu wanakufa kwa njaa
ujue kuna kitu Mungu anadai au ibada ya sanamu imekithiri, ukiona watu wengi
wanakimbia nchi ujue kuna laana ya ukiwa.
Katika
kila jambo lihusulo hali ya hewa, mahali pa kuishi, hali ya uchumi ni muhimu
utafute makusudi ya Mungu katika Biblia. Mambo haya yote ndani yake kuna
makusudi ya Mungu, ukiyatafute ndani ya neno la Mungu utayajua! Jipatie ufahamu
uyajue yanayokuhusu na yanayohusu nchi yako kwa kusoma maandiko. Barikiwa.
BWANA ALIPOAMURU BARAKA
MUDA MWAFAKA ENEO
MWAFAKA.
Katika mambo ambayo Mungu hata subiri
ufanye maandalizi ni hukumu na fursa. Kila siku unapaswa kuwa tayari, katika
eneo husika, mwenye maandalizi kamili, ndio maana ya lile neno kesheni. Si kila
eneo, si kila Mkoa, si kila medani wala si kila nchi itakuwa na Baraka zako;
liko eneo moja, iko aina ya biashara fulani, uko mkoa na pahala ambapo Mungu
ameamuru baraka zako zipatikane. Wakati mwingine tunachagua miji kwa macho ya
nyama na hivyo tunavyokwenda ndani yake hatufanikiwi sana. Si kila aliyeko
Ulaya anamafanikio, kuna wengine wako huko na wanaomba chakula, hawana uhakika
wa kupata milo mitatu.
Kuna watu ambao walikuwa jijini Dar es
salaam ilhali baraka yao ilikuwa Dodoma. Kwa vyovyote vile haikuwa rahisi
kuwapeleka watu hao Dodoma inawezekana walifikiri hakuna maisha bora nje ya
jiji la Dar es salaam. Lakini Mungu kwa
kutumia Tangazo la Serikali la kuhamia Dodoma amewawezesha pia maelfu ya
watanzania kwenda kwenye baraka yao iliyoamriwa mjini Dodoma. Tangu nyakati
za Yesu Kristo mpaka sasa matangazo mengi ya Serikali yamekuwa yakibeba
makusudi ya Mungu ya amani. Amani maana yake uchumi mzuri, Baraka na mafanikio.
Yanaweza matangazo hayo yakaonekana magumu na mabaya yenye kubeba usumbufu
lakini baadaye Mungu hujitwalia utukufu na watu wake hustawi.
Ukihamishwa
kwa Tangazo la Serikali usigome, Matangazo hayo hubeba baraka. Katika saa yako ya kusimama kiuchumi na
kiutumishi tangazo hilo halitaweza kukudhuru hata kama lilitolewa ili
kukuangamiza wewe. Tangazo la Herode la kuua watoto wote chini ya miaka miwili
halikuweza kumua Yesu maana ilikuwa ni wakati wa Yesu kung’aa na kuokoa, halikuweza
kumzuia.
Si miji peke yake, hata changamoto nyingine
za maisha zenye ukakasi ndani yake kuna
baraka pia. Wako watu ambao bila talaka wasingelipata wokovu, bila kuachwa
wasingelijua kusimama wenyewe, wako wale ambao bila kufeli masomo wasingeli
jaribu biashara ambazo leo zimewapandisha na kuwafanya wakuu.
Baraka hizo zisingepatikana ikiwa kila kitu
kingekuwa shwari, mara nyingi inapokuwa ni shwari watu hujisahau sana na
kufanya yasiyo ya msingi. Biblia inasema, “Katika shida yangu nalimwona BWANA”. Kuna nyakati ambapo ni kupitia shida
na usumbufu tunaweza kumwona Mungu. Ni methali ya zamani ya wazungu, “Bahari
shwari haitoi wanamaji hodari” ni kweli baharia hodari ni lazima atakuwa na
uzoefu wa kutatua shida za majini.
Usiogope sura ya mji, usiogope ukubwa wa
changamoto inayokukabiri; cha msingi hakikisha uko mahali sahihi ukisubiri
wakati sahihi wa kuinuliwa kwako. Mahali ambapo Mungu ameamuru baraka pana
changamoto lakini pia pana baraka nyingi. Kuwa mahali pa baraka haina maana
hapatakuwa na changamoto kabisa! Mara nyingi ustawi wako katika eneo hilo
utategemea pia namna unavyomkumbuka Mungu, kumkumbuka maana yake kushika amri
zake na kumshuhudia kwamba ni yeye ni Mungu aliyekufikisha hapo Sayuni yako.
Barikiwa na Endelea mbele…
MWAKA 2018
UWE MWAKA WA KUJIHATARISHA ZAIDI ILI KUPATA MAFANIKIO
Wengi
wanashindwa kwa sababu hawafanyi kitu mpaka waone ni salama kabisa, hawaanzi
mradi mpaka waone ni faida tupu, tabia hii imezuia mafanikio ya wengi. Mwaka
jana niliingia kwenye biashara ya mtandaoni (online business) na kupata hasara
ya milioni nne, mwaka huo huo bila ya kukata tamaa nikaingia katika biashara
nyingine na kupata faida ya milioni nne! Ukipata hasara katika biashara moja
haina maana kwamba na biashara nyingine utapata hasara pia.
Kitabu
cha Mhubiri kinasema, “Mwenye
kuuangalia upepo hatapanda; Naye ayatazamaye mawingu hatavuna” Mhubiri
11:4. Ukichunguza chunguza sana huji kufanikiwa katika uwekezaji na maendeleo.
Kuna wakulima ambao wakijua ni msimu wa kilimo wanalima na hawa ndio
hufanikiwa. Na kuna wale ambao hata kama ni msimu wa kilimo wao huchunguza
chunguza mawingu na mwishowe wanashindwa kupanda mbegu zao.
Tabia
ya kujihatarisha ni njema na imewasaidia wengi. Fanya kitu kwa wakati uchunguzi
utakuja baadaye! Amesema Ratan Naval Tata mwanzilishi wa kampuni ya kutengeneza
mitambo na magari aina ya TATA, “I don’t believe in taking right decision, I
take decisions and then make them right” kwa tafsiri yangu amesema, “Siamini
katika kuchukua maamuzi sahihi, bali nafanya maamuzi na baadaye nayafanya kuwa
maamuzi sahihi”
Kujihatarisha
inaweza ikawa ni kuachana na uhusiano mbaya, inaweza ikawa ni kuhama mji mmoja
kwenda mwingine, inaweza ikawa ni kufunga na kuomba licha ya dalili za vidonda
vya tumbo. Inawezekana ikawa ni kurejea nyumbani usiku kila siku kwa sababu za
msingi, au ikawa ni kuamka mapema. Pia kujihatarisha inaweza ikawa ni kufanya
kinyume na walio wengi, kwenda katika upekee wako au katika njia ya ubunifu
ambayo wengi hawapiti. Vyovyote vile kama hatukujihatarisha kabisa hatutapata
badiliko lolote.
Matajiri
wengi akiwemo Bill Gates na Oprah Winfrey wamekuwa na sifa ya kukatiza masomo
au kuacha kabisa ili kwenda kutumikia ndoto zao. Hii nayo ni kujihatarisha,
kuacha kile ambacho dunia inaamini ni ufunguo wa maisha ilikuwa ni sawa na
kuyafunga maisha yao. Lakini pamoja na hatari ya kuacha shule bado wamefanikiwa
na wamewaajiri waliohudhuria vizuri shuleni. Kama kunamafanikio nje ya elimu
basi ni muhimu tukajua elimu si ufunguo pekee. Maisha ni zaidi ya vidato!
Maskini
wote wanachukia vurugu na hatari, hawapendi biashara nje ya kiyoyozi hata mara
moja hawajitumi kutembeza bidhaa. Wanapenda usalama, kulala mapema na kuchelewa
kuamka. Hawapendi kusafiri juu ya magari aina ya Fuso yanayokwenda minadani,
wanapenda usafiri tulivu na salama, hawataki usumbufu wa wachuuzi wadogo wadogo
wenye kutembeza biashara. Hawawazi kuajiri, wao wanataka kuajiriwa tu!
Nakumbuka
mwaka 2015 baada ya sala na maombi niliamua kuondoka nyumbani umbali wa mikoa mitano na kuhamia jijini Dar-es-salaam
na ndani ya miezi miwili nilipata nilichokuwa nahitaji kwa muda ule. Si kila
mtu atafanikiwa mjini wengine wanahitaji kurudi vijijini na wengine kwenda
mjini ili kukutana na mafanikio yao. Ili kukutana na ndoto zao wengine
itawalazimu kutoka Ulaya na kurejea katika nchi zao.
Unapopanga
mipango yako mipya weka na mipango yenye kukuhatarisha (bila kuvunja sheria) na ndiyo mipango ya mafanikio.
Take risks,
if possible take calculated risk……