KUELEKEA UHURU WA
KIFEDHA
(THE BIBLICAL LAWS OF MONEY)
Tafiti mbalimbali zinaeleza kwamba, moja ya
changamoto kubwa ulimwenguni hasa bara la Afrika ni umasikini mkubwa wa kipato.
Ni ukweli unaosikitisha, na eneo hili ni moja ya maeneo ambayo hayana msisitizo
mkubwa ndani ya mwili wa Kristo (kanisa). Eneo la maarifa kuhusu fedha au
uchumi ili kumkomboa mtu kiuchumi ni kama limeachwa; Na kwa sehemu kubwa ukiona
mahali fedha inatajwa kanisani au kikundi cha sala basi ujue ni sadaka
inayozungumziwa. Ni watu wachache sana wanaozungumzia au kuhubiri au kufundisha
maarifa kuhusu fedha na uchumi ili kumuwezesha mtu kupiga hatua katika eneo
hilo kwenye maisha yake na jamii yake.
Jambo moja ambalo ni halisi na halikwepeki
ni kwamba, ili kuishi katika ulimwengu huu wa sasa kila mtu anahitaji fedha za
kutosha kumuweza kukidhi mahitaji yake na mahitaji ya wale wanaomzunguka. Kumbuka
fedha haina dini, haijali kabila wala rangi yako; haiwezi kuja kwako kwa sababu
wewe ni wa dini au dhehebu au rangi au kabila fulani (it is neutral). Na kwa sehemu kubwa, kiwango cha fedha au mafanikio
ya kiuchumi ya mtu yanategemea kiwango cha maarifa na ufahamu sahihi alionao juu ya kanuni za fedha
(The laws of money).
Nakumbuka siku moja wakati nipo sekondari niliwahi
kuhudhuria kikundi cha sala mahali
fulani, na siku hiyo tukafundishwa kuwa ili kufanikiwa kifedha basi ni
lazima tutoe sadaka ya kupanda ili makusudi tuvune mara mia kwa kigezo kwamba
ukitoa utapokea mara mia ya ulichotoa (bila shaka unakumbuka hilo andiko). Na tena
nikakumbuka lile andiko la kila apandacho mtu ndicho atakachovuna, basi
nikapiga hesabu zangu pale, kwamba endapo nitatoa elfu moja basi nitarajie
kupokea laki moja (bila shaka sijakuacha hata kama ulikimbia hesabu, elfu moja
mara mia ni laki moja). Sijui kama unaelewa maana yake nini upo sekondari
unatarajia kupokea laki moja ya kwako binafsi (hahahaha). Nikawaza tu nikiipata
hiyo laki moja napanda elfu kumi, sasa piga hesabu hapo elfu kumi mara mia,
mavuno ni kiasi gani? (tajiri mtoto anayechipukia).
Japo unaweza kucheka, inawezekana umewahi
kuwaza hivyo pia. Kanuni moja muhimu sana kuhusu fedha ambayo huwa haifundishwi
na leo nataka niigusie ni kanuni ya
uzalishaji bidhaa au huduma (The law of production). Pamoja na kwamba
sadaka na maombi ni muhimu sana kwa ustawi wa mtu; ni ukweli uliowaza kwamba
hakuna aliyefanikiwa kiuchumi kwa mambo hayo TU (bila uzalishaji huduma na
bidhaa) isipokuwa aliyepo upande wa kupokea. Wazo kuu tunalotaka ulipate kwa siku ya
leo ni kwamba, ukitaka kufanikiwa kiuchumi hauwezi kukwepa uzalishaji bidhaa au
huduma kwa namna moja au nyingine.
Nioneshe anayeuza bidhaa au huduma, nikuoneshe mtu atakayefanikiwa
kiuchumi. Zalisha huduma au bidhaa ambayo tunauhitaji nayo, na sisi tutakuwa
tayari kukupa fedha kwa kuipata bidhaa/huduma hiyo kwa sababu tunaihitaji na
hapo mafanikio ya kiuchumi yatakuwa dhahiri kwako.
Mungu ameahidi mvua ya Baraka, sio mvua ya
fedha. Mungu ameahidi kushusha Baraka kwenye kazi ya mikono yako, kapu lako na
chombo chako cha kukandia unga, mifugo yako, mazao shambani kwako, hakuna
mahali ameahidi kushusha fedha toka juu. [Kumbukumbu la torati 28:4-5, 8]. Kusubiri
mavuno ya sadaka uliyopanda tangu mwaka juzi ili utoke kwenye mkwamo wa
kiuchumi uliona sasa, ni uvivu wa kufikiri, na ni kukosa uwajibikaji
(irresponsibility).
There’s a place for you at the top!
USIWAPELEKE MAHALI
USIPOWEZA KUWATOA
Hili ni jambo la msingi kwa kiongozi wa
ngazi yoyote ile, haijalishi ni ngazi ya familia, kata, kampuni, taasisi
binafsi au kiongozi wa siasa. Kuna maeneo ukiwafikisha watu au ukiwapeleka
unaowaongoza hautaweza kuwatoa wote kwa usalama. Kiongozi lazima awe na kipimo
cha madhara na uathirika unaoweza kujitokeza kabla ya kuchukua uamuzi wake.
Kwenye biblia kuna kisa cha Lutu aliyemuita
Ibrahimu mjomba. Huyu baada ya kuipeleka familia yake katika miji ya Sodoma na
Gomora alishindwa kuwatoa wote. Huko alimpoteza mkewe. Alitamani waokoke familia nzima kama
walivyoingia lakini hakuweza. Ingawa haijaandikwa lakini nina hakika Lutu
alijisikia vibaya kumpleleka mkewe mahali asipoweza kumtoa. Sodoma ilikuwa ni
uchaguzi wa Lutu nyakati za kutengana na Ibrahamu, haukuwa uchaguzi wa mkewe
Lutu. “Lakini mkewe
Lutu akatazama nyuma yake, akawa nguzo ya chumvi.” Mwanzo 19:26
Rais Obama aliyekuwa kinara katika
kuangusha Serikali ya hayati Rais Gadafi wa Libya alinukuliwa akijutia
kushindwa kuijenga Libya mpya. Obama amewafikisha watu wa Libya mahali ambapo
hawezi kuwatoa. Mpaka ameondoka hajaweza kujenga Libya mpya aliyoahidi na
badala yake imekuwa pango la magaidi na wapiganaji.
Amesisitiza mwenye hekima mmoja kwamba, “In life you cannot undo every action”
akimaanisha, “Katika maisha si kila kitu unaweza kukirejesha tena katika
uhalisia wake.” Kuna akili zilizoharibika, kuna familia zilizoharibika, kuna
vikundi vilivyoharibika; kuna jamii zilizoharibika, pia kuna kampuni
zilizoharibika na si wote watakao weza kufanya urejesho. Kwa kuwa zoezi la
urejesho ni gumu na zito basi ni busara kuepuka uovu, tabia hatarishi na
mazingira yake. Huwezi kuepuka moshi ikiwa unapika kwa kuni, kwa hiyo katika
kubadilisha mwenendo huwezi kupuuza mchango wa mazingira yako. Mazingira
hatarishi ya Sodoma na Gomora ndio chanzo cha uharibifu wa mke wa Lutu.
Kama baba wa familia au kiongozi (Lutu) ni
lazima uogope maamuzi au maeneo ambayo huna uhakika kwamba, wale unaowaongoza
watatoka salama. Yuko rafiki anayeweza kukufundisha tabia mbaya ambayo huwezi
kuiacha, yako makundi mabaya ambayo yanaweza kukufundisha tabia hatarishi
ambazo huwezi kuzikomesha. Je, unamkumbuka uathirika uliingia lini maishani
mwako? Ulevi, ubwiaji wa unga na dawa za kulevya, utazamaji wa picha chafu na
uasherati? Ni baada ya kujisamehe sisi wenyewe ndipo tunapoweza kumsogelea Yesu
mwanamapinduzi ili atusamehe na kutupa upya.
Watu wengi wamekuwa wanamwogopa Yesu kwa
kuwa ni mwanamapinduzi na wanajua wakimsogelea atapindua tabia zao na atapanda
tabia njema. Mwanamke Msamaria aliyekutana na Yesu kwenye kisima cha Yakobo
alikuwa na uathirika. Alikuwa amekuwa na wanaume watano, that was an addiction! Na kwa muda ule mfupi Yesu alipindua
maisha yake.
Muda, afya njema, ufahamu, malezi ya
watoto, umoja na mshikamano ni moja ya mambo ya kulinda sana kwa kuwa
hayarejeshiki kirahisi na pengine hayarejesheki kabisa baada ya kuharibiwa.
Jilinde!
UTIMILIFU WA KUSUDI
LAKO UTAHITAJI MAFUNGO
Ni kwa zaidi ya miaka mitatu sasa Programu
yetu (Life Minus Regret) imekuwa kazini katika kuwasaidia watu kujua makusudi ya
kuumbwa kwao na kuyaishi. Tumekuwa tukiwahamasisha vijana wamjue Mungu ili naye
awaambie wao (vijana) ni akina nani.
Ni Mungu aliyemwambia Yeremia, “nimekuweka uwe nabii wa mataifa” ni Yesu
aliyemwambia Petro, “lisha kondoo zangu”, na baadaye akamwambia tena, “chunga
kondoo zangu.” Hawa wote walipata kuambiwa kazi zao na wito wao kwa sababu
walitafuta kumjua Mungu na kuhusiana naye.
Mambo matatu ni muhimu katika kuhusiana na
Mungu; kusali, kufunga na kutoa sadaka. Yesu akasema “nanyi msalipo…,” maana
yake anategemea tutakuwa tunasali mara kwa mara, tena akasema, “nanyi
mfungapo….” Pia akihimiza “nanyi mtoapo sadaka…” Haya matatu aliyafundisha kwa
kuwa yote ni muhimu kufanyika mara kwa mara ili kumkamilisha mtu. Mathayo 5:2, 5,
6 na 16
Sala, sadaka na mafungo ni vitu muhimu
katika kuhusiana na Mungu. Katika eneo la sala na sadaka wengi wanajitahidi,
changamoto iko katika eneo la ushindi na mafanikio ambalo ni eneo la kufunga.
Wengi hupanga kufunga na kabla siku haijafika hughairi na kufakamia chakula.
Shetani hatoi ruhusa katika hili kwani anajua lina baraka, tena halijali idadi.
Mafungo ni muhimu kwa ajili ya huduma yako
na kusudi lako. Kama Yesu angeweza kutimiza kusudi lake bila mafungo
asingelifunga. Alifunga siku 40 kwa sababu ilikuwa muhimu. Huduma nyingi
huzaliwa kipindi cha mafungo. Huduma ya mitume waliotengwa yaani, Barnaba na
Sauli ilikuwa ni baada ya maombi na mafungo. Matendo ya Mitume 13:2
Jentezen Franklin katika kitabu chake cha:
“Fasting” anakiri huduma yake ilizaliwa kipindi cha mafungo, Mchungaji Oyadepo
na wengine wengi huelezea jinsi mafungo yalivyofungua njia katika wito wao na
makusudi ya Mungu maishani mwao.
Ukiweza unaweza kukataa kula chochote kile
kwa muda fulani. Pia katika kufunga unaweza kataa chakula cha nguvu yaani,
wanga na ukashinda siku yako yote ukinywa maji tu au chai tu. Siku hizi
nikifunga huwa nakunywa maji tu, hii huondoa maswali kwa wanaonizunguka kujua
kwamba nimefunga au sikufunga. Usifunge na kujinyima vimiminika kiasi cha
kukosa nguvu ya kuomba. Unaweza kunywa chai au juice pekee kwa saa 12 au 24 na
hayo ni mafungo mazuri kwani nina hakika utakuwa na nguvu katika kuomba na
kusali wala hutaomba kwa ulegevu.
Usichokijua nyuma ya mafanikio ya watu
wengi wakuu ni yako mafungo na sadaka. Mafungo hufanya mwili na nafsi
visielekee kwenye chakula na badala yake vimwelekee Mungu. Kuna jambo bado
halijatimia katika huduma na wito wako nalo litahitaji mafungo. Ni muhimu kwa
kukupa upenyo na kukufungulia yaliyofungwa.
Barikiwa
FURAHIA MAISHA YAKO!!
Mungu
ametuumba si tu kwa ajili ya ibada na kazi, bali hata kwa ajili ya kufurahia
maisha haya. Kutembelea fukwe, kula vizuri, kusafiri, kushiriki matukio ya
furaha na pengine hata kuwa na mitoko ya hapa na pale kwa wale wapendanao. Alisema
Ratan Tata yule mmiliki wa kiwanda cha kutengeneza magari ya TATA, “Hakuna
faida yoyote ikiwa utapanda cheo siku ambayo mnatengana na mpenzi wako…maisha
hayahitaji uwe shupavu na makini kiasi hicho” alimaanisha mafanikio ya
kazini yaende sambamba na furaha ya nyumbani, tukichukulia maisha kuwa magumu
sana kila siku itakuwa ni mapambano bila ya pumziko.
Biblia
inaweka wazi katika kitabu cha Mhubiri 3:13, “tena ni karama ya
Mungu kila mtu apate kula na kunywa, na kujiburudisha kwa mema katika kazi yake
yote.” Napenda mstari ulivyotafisiriwa kwa lugha nyingine, “It is a gift of
God to enjoy the good of all his labor”.
Mungu
anapenda kila mtu apate muda wa kufurahia matokeo ya kazi zake. Baada ya kazi
nzito ni furaha, partying and enjoying!!! Hatuna maana kwamba mioyo yetu izame
katika anasa la hasha! Bali kuwe na muda wa kupumzika na kufurahia maisha
ambayo ni zawadi kutoka kwa Mungu.
Maneno
ya Reba Mc Entire huwa ni ya kuchekesha lakini yana maana alisema, “to
succeed in life you just need a wishbone, backbone and a funny bone”.
Ni kweli kabisa kila siku ni lazima tuwe na msingi wa kutumaini na kutamani
yajayo lakini ni lazima ucheshi na furaha viwe kama uti wa mgongo wa mafanikio
yetu.
Namna
rahisi ya kufurahia haya maisha ni kuwa sababu ya wengine kufurahi. Katika
mchakato wa kufanya watoto, majirani, mke, mume, binti wa kazi, au mfanyakazi
mwenzio afurahi utajikuta wewe mwenyewe unafurahi. Furaha inatabia ya kurudi
kwenye chanzo chake, hakikisha unakuwa chanzo cha furaha.
Maisha
haya si marefu kiasi kwamba tukumbatie huzuni, ukiishi miaka 50 unamapumziko ya
Jumamosi na Jumapili 2500 tu na inawezekana zimeshapungua, kama una mika 25
umeshatumia nusu ya majuma hayo. Jipange.
Enjoy…………
UVIVU NA
UUAJI.
Maneno
haya mawili si rahisi kuyatenganisha, ni kama chanda na pete. Uvivu una hasara
kubwa sana na matokea yake ni uuaji. Utaua karama yako au kipaji chako, utaua
mtaji na pengine utapoteza yale ambayo wengine waliyasumbukia kwa muda mrefu na
walikupatia wewe uyaendeleze.
Uvivu
haufanyi tu ukose yale unayoyatamani kuyapata bali unakupokonya hata lile dogo
ulilonalo tayari. Muuzaji hodari atachukua wateja wa yule dhaifu na mvivu katika
biashara. Kile usichokitunza huondoka na hii ni kanuni wazi. Kile usichokilinda
kitaibwa hii haipingiki, ndio maana ikananenwa shika sana ulichonacho.
Nyakati
za mfalme Sulemani katika maandiko, yuko mama aliyemlalia mtoto wake na kumuua
kisha kugombea mtoto wa mwenzake. Alilala wakati wanawake wenzake hupumzika tu
maana wanajua mtoto ni muhimu kwao kwa saa 24. Ni uzembe wa hali ya juu
kusinzia hadi kuua mtoto uliyemsumbukia kwa muda mrefu (1Wafalme3:19).
Inawezekana wewe na mimi tukiendelea kulala kuna vitu vitakufa. Rafiki yangu
mmoja aliwahi kuniambia, “Alphonce, vijana hatulali tunapumzika tu” Ukipenda
usingizi utaua ndoto zako na hatma yako.
Siku
nyingine nikajifunza kuachana na neno sana. Nakushauri pia uondoe neno “sana”
katika misamiati yako. Nimechoka sana, nimesoma sana, nimetembea sana ni
sentensi zenye kuhalalishi na kutoa udhuru wa kutofanya kitu kinachotakiwa au
cha ziada. Hii ni dalili ya uvivu, neno sana lazima liondoke. Aliyechoka sana
atatamani kulala sana lakini aliyechoka atatamani kupumzika na kurejea tena
ulingoni. “So avoid using the word ‘very’
because it’s lazy”
Mwingine
anaweza kuwaza, Uvivu ni nini? Ni ile hali ya kughairisha mambo. Nitafanya
jioni, nitafanya kesho na hatimaye nitafanya mwakani. Uvivu pia ni hali ya
kushindwa kuzingatia jambo moja, ni kuitawanya akili katika mambo mengi ambayo
pengine si ya msingi. Uvivu pia ni ule uoga unakuja wakati wa kupanga mipango
mikubwa na migumu na hivyo mtu kwa kujihurumia anajipangia mipango midogo na ya
kawaida sana. Mvivu anakubali huondoka mapema hata kama kazi haijaisha, kamwe
hapambani mpaka mwisho. Kwa hiyo uvivu
ni ile hali ya kuishia njiani.
Inawezekana
umepoteza fursa nyingi na sasa huna cha kushika. Lile neno shika sana
ulichonacho halina tena nguvu kwako maana huna cha kushika. Usiogope, Yesu
Kristo aliye ufufuo na uzima na kweli anaouwezo wa kufufua yaliyokufa. Yeye
alimwita Lazaro aliyekufa na akatoka mzima. Kwake huyu Mungu mwenye nguvu, na
Mfalme wa ajabu twaweza kuomba, Ee Bwana fufua kazi zako ndani yetu.
Amka
sasa uangaze….