Siachi

11:13:00 PM Unknown 0 Comments

 
SIACHI
(Dhambi ni kutelekeza kipaji chako)
“If you can’t walk then crawl. But whatever you do you have to keep moving Forward'” Martin Luther King Jr.
Katika siku za karibuni tumeshuhudia migomo ya watu wenye taaluma na vipaji mbalimbali. Kumekuwa na migomo ya walimu, madereva, madaktari na watu wa kada na tasnia nyingine tofauti tofauti. Migomo hii hulenga kuifanya jamii na serikali itambue mahitaji ya makundi haya kipekee, hususani tafsiri ya uwiano wa mchango wao kwa jamii na mishahara wanayolipwa.
Katika migomo yote, mgomo wa madaktari hutikisa zaidi, madhara yake ni dhahiri machoni pa wote. Watu hupoteza maisha, wagonjwa huteseka na ndugu zao hupoteza matumaini. Kama ilivyo kwa madaktari, yako madhara kwa kila mwenye kipaji ambaye ataacha kukitumia. Waathirika ni wale ambao Mungu alitaka wanufaike kwa kipaji chako. Ni wazi hakuna mto unaokunywa maji yake wenyewe. Yako madhara kama viongozi watajiuzulu bila msingi, yako madhara kama wahubiri watasimama na kuacha kuhubiri. Yesu alisema, atazamaye nyuma hafai kwa ufalme wake.
Dereva mwenye hekima akikimbia nafasi yake atafanya madereva walevi wapate ajira na kisha kuua watu kwa ajali isiyo na sababu. Kwa sababu ya wenye hekima kuogopa siasa, nchi zimeongozwa na mabaradhuli. Mchungaji akiacha kuombea kondoo shetani anawatafuna. Kuacha wajibu wetu ni dhambi, Samweli akasema, siachi…… 1Sam 12:23
Wizi, uzinzi, ulevi na uasherati si dhambi kubwa ukilinganisha na mhandisi kuacha kazi aliyoitiwa na Mungu. Dhambi kubwa ni mwimbaji wa kusifu na kuabudi kuacha huduma yake, mhubiri kuacha kuhubiri, kiongozi kuacha kuongoza.
Wewe kama ni ndege jielekeze katika kuruka na si kuogelea. Ni kwa faida yako, ukitaka kujua madhara ya kutokutumia kipaji chako jifunze katika vipaji ambavyo madhara yake yako nje kama vile udaktari au udereva, ambapo kosa moja hugharimu pumzi za watu.
Paulo alisema, “Ole wangu nisipo ihubiri injili”. Usipofanyia kazi kipaji ulichopewa na Mungu unafanya dunia iwe kama kibogoyo, maana pengo lako halitazibika. Uzuri wa dunia ni pamoja na mchango wa kipaji chako.
Jaribu kufikiri familia yenu bila ya wewe, kanisa lenu bila ya wewe, kazini kwako bila ya wewe kuwepo  kama hakuna pengo lolote katika kutokuwepo kwako ujue wazi hautumii kipaji chako. Imagine the World without Jesus Christ!
Mimi siachi kuhubiri, siachi kuimba, siachi siasa safi, siachi ufundi, siachi sanaa, siachi nasema siacha ubunifu wangu. Usiache karama yako ya maombi (1Sam 12:23); usiache biashara yako wala usidharau mwanzo wako mdogo, wala usipuuze wazo lako la ushindi. Kuendelea mbele inapaswa kuwa kama wimbo wako. Mungu Baba na akuimarishe katika kipaji na wito wako ulioitiwa, ukawe hodari; kama jua lisivyo acha kuangaza na wewe kwa kupitia kipaji chako ukaangaze milele kwa jina la Yesu Kristo. Amen
Kileleni ndipo tunapopatikana.

0 comments :