Namna bora ya kutumia ....
NAMNA BORA YA KUTUMIA KIPAJI CHAKO.
(Appropriate your gift)
Kila kitu kizuri tunajua kinatoka kwa BWANA, Mungu anatenda kazi katika kuwaza na kufikiri kwetu. Ni Mungu atupaye mawazo. Wengi wamezoea kumshirikisha Mungu katika hatua ya utekelezaji, hawajazoea kumshirikisha Mungu katika msingi wa mawazo yao, ambayo ndio hatua ya awali kabisa. Daudi aliomba akisema, “Mawazo ya moyo wangu yapate kibali mbele zako” alitaka Mungu ahusike na mawazo yake.
Vipaji vyetu na taaluma zetu si tunda la akili zetu (it is not our brain child) ni zawadi kutoka juu. Kila kitu kizuri ni zawadi kutoka juu. “ ...kila kitolewacho kilicho kamili, hutoka juu, hushuka kwa Baba wa mianga.” Yakobo 1:17
Je! Una kipaji? Wewe ni mwanaridha, mtunga mashairi, fundi sanifu, mcheza mpira au mpigaji wa vyombo vya muziki. Vyote hivyo ni vipaji au karama kutoka kwa Mungu tunazopaswa kuzitumia kwa manufaa ya watu wote.
Je, wewe ni mtaalamu? Wewe ni mtawala (manager), wewe ni askari wa barabani, wewe ni mhasibu, wewe ni mgavi au mwalimu, zote ni fani ambazo zinapaswa kutumika kwa maslahi ya watu wote (For common good) wala si kwa maslahi yako binafsi. Ameonya msanii mmoja akisisema, “una mashavu makubwa paka pori, lakini umeshiba vya anasa”.
Hakuna mto unaokunywa maji yake wenyewe, hakuna jua linalojiangaza lenyewe vivyo hivyo hupaswi, kuiba au kujinuifaisha wewe tu. Ukiwa mhasibu kusanya na kuwasilisha ili baadaye kilichopatikana kiwafae watu wote. Ukiwa mchezaji wa timu usicheze ili tu kuonekana peke yako, cheza ili timu yote ifanikiwe na kushinda kama timu.
Mungu ametupa vipaji, karama kama nyezo za kuwatumikia wenzetu ili Mungu atukuzwe. Tunatakiwa kuwa waaminifu na watu wasio na ubinafsi (selfless) ili karama na uwezo tuliopewa na Mungu umnufaishe kila mtu. Uwezo wa Nelson Mandela umenufaisha wengi huko Afrika ya Kusini. Uwezo wa Yesu Kristo umeleta wokovu na kuhesabiwa haki kwa kila kiumbe.
Baba mbinafsi hula kitimoto na kuku choma mtaani na kuacha mihogo nyumbani, lakini baba mwaminifu yeye hupeleka kitoweo nyumbani akale pamoja na watoto na mke wake. Ni kwa namna hii karama zetu zinapaswa kutumika kumfaidia kila mmoja wetu katika familia ya Mungu. Ukiwa mwaminifu kwa kuyalinda mapato na maslahi ya ofisi yako basi kwa njia hiyo utakuwa umemsaidia kila atakayelipwa mshahara halali na ofisi hiyo.
Ukiwa na kipaji basi safari zinakuhusu, kila siku ni lazima uwaendee wale wanaotakiwa kunufaika kwa kupitia kipaji chako. Daktari aende kwa wagonjwa, mwalimu aende kwa wanafunzi, mfanyabiashara asipange bei yenye kumwonea mteja kwa lengo la kupata faida kubwa.
Kila siku Yesu alikuwa safarini akiwaendea wale alioitwa kwa ajili yao, alikwenda Samaria, Galilaya na katika miji na vitongoji vingi kuwaendea wanaomuhusu. Mwanadamu ni kiumbe wa safari na mizunguko, si rahisi kufika juu katika kilele cha mafanikio yako ikiwa utatulia sehemu moja. Mabadiliko ya kijiografia na maeneo yanabaraka zake. Ibrahimu, Yakobo, Musa na Yusufu wote walikuwa ni watu wa safari, walitii sauti ya Mungu, walihakikisha wanapatikana katika eneo wanalotakiwa kwa wakati. Walikuwa ni watu kwa ajili ya watu, kwa Ibrahimu sote tumepokea Baraka. Mimi na wewe tu baraka, kwa ajili ya mataifa kama ilivyokuwa kwa baba yetu Ibrahimu.
We are the blessings!!!
0 comments :