Toa huduma bora, Uza bidhaa bora

11:44:00 AM Unknown 0 Comments


 
TOA HUDUMA BORA, UZA BIDHAA BORA
(Ubora si ajali, “Quality is not accident”)
Tangu zamani tumesikia kwamba, ukimpa mtu samaki utakuwa umemlisha kwa siku moja lakini ukimfundisha mtu kuvua samaki utakuwa umemlisha kwa maisha yake yote. Kumpa mtu mtaji bila maarifa ya kufanya biashara ni sawa na bure. Anayekusaidia kuijua teknolojia ya uzalishaji anamsaada zaidi kwako kuliko anayekupatia pesa.

Baada ya vita kuu ya pili ya dunia bara la Ulaya lilijikuta likiwa hoi kiuchumi. Viwanda vyake vingi vilidorora, watu wengi waliuawa na uchumi wake ulikuwa umeanguka kabisa. Marekani iliamua kuisaidia Ulaya katika mpango uliojulikana kama Marshall plan ukiasisiwa na Mwana Amerika George Marshall. Katika pragramu hiyo ya ujenzi wa Ulaya (Uerope Recovery Program) Marekeni ilitoa dollar zake billion 13. Na mara baada ya pragramu hiyo kuisha, uchumi wa nchi nufaika  ulikuwa bora kwa zaidi ya 35% ukilinganisha na uchumi wao kabla ya msaada.

Msaada huo alioutoa Marekani haukuwa katika mfano wa samaki bali ulikuwa katika mfano wa uvuvi. Wahandisi walitoka ulaya na kwenda kujifunza Marekani namna ya kuendesha na kuhuisha tena viwanda vyao, wahandisi wengine walitoka Marekani na kwenda kushirikiana na nchi nufaika. Kupitia kubadilishana wataalamu nchi hiazi zilibadilishana teknolojia pia (transfer technology). Nchi nufaika pia ziliondoa vizuizi vya kibishara na kuamua kushirikiana kitu ambacho kilipelekea kuzaliwa kwa Jumuiya ya Ulaya. UJerumani iliyokuwa ikikabiliwa na shida ya chakula iliimarika sana na  viwanda vyake vya uzalishaji vilihuishwa na kuweza kuzalisha vema.

Ni wazi kama msaada huo ungekuwa ni pesa tu, Ulaya isingelisimama kiuchumi. Pesa mikononi mwa mpumbavu ni kifo. Kabla hujapata pesa lazima uwe na uzoefu na maarifa ya namna ya kuitumia. Mtu mwenye pesa akikutana na mtu mwenye uzoefu na maarifa, pesa zake huenda kwa mtu mwenye maarifa na yeye hubakia na maarifa. Kwa hiyo ili mtu akae na pesa ni muhimu pia awe na maarifa.

Naungana na Donald Trump, Robert Kiyosaki , Anthony Robbins na wengine wengi tunaoamini kwamba mifuko ya hifadhi ya jamii imefeli. Mifuko ya hifadhi ya jamii inawapa watu pesa wakiwa wamechoka na pengine ni wazee yaani, unaweka magurudumu mapya (new tyres)katika injini ya gari  iliyochoka kabisa.

 Inawapa wastaafu pesa bila maarifa wala namna nzuri ya kuzitumia, wengi hawana elimu juu ya usimamizi wa fedha. Hata Marekani ingetoa pesa kwa mtindo wa mifuko ya pensheni kusingelikuwa na mafanikio yoyote katika kuisaidia Ulaya. Mwenye hekima mmoja anasema, “Umewahi kuwaza kitu gani kitatokea ikiwa Mhasibu atafanya ‘wiring’ ya umeme? Umewahi kuwaza kitu gani kitatokea ikiwa Mhandisi atamng’oa mtu meno? Je, nini kitatokea ikiwa mtu ataenda kwa daktari ili kupata ushauri wa nyota?” Majibu unayoyapata ndiyo kinachotokea pesa inapotua mikononi mwa mtu asiyejua namna ya kufanya.

Ili watu wapate uhuru wao kiuchumi na kifedha ni lazima wajipenyeze katika utoaji wa huduma au uuzaji wa bidhaa. Bidhaa zinapaswa kuwa bora, ubora hauji kama ajali ni matokeo ya bidii, maarifa, sadaka na jitihada. (Quality is not an accident) Ile huduma unayoweza kuitoa vizuri na wateja wakaridhika (shule, televisheni, muziki, mgahawa, hoteli, uambaji, uandishi, usisimuaji na usanii) ndio mlango wa utajiri wako. Mpaka watu waingie katika uuzaji wa bidhaa (duka la nguo, duka la vifaa vya magari, mazao ya chakula, duka ya huduma, maduka ya vitabu, viwanda, mazao ya misitu, uandaaji na uuzaji wa samaki, usindikaji n.k) ndipo uhuru wao huja. Ni vema kujifunza teknolojia inayotumika katika kusindika na kuandaa bidhaa mbali mbali.

Sunday Adelaja anasema: “Maombi peke yake hayatoshi, kutoa fungu la kumi peke yake haitoshi”. Utoaji wa huduma nzuri na uuzaji wa bidhaa bora ni jambo muhimu. Ubunifu nao si wa kubezwa, wabunifu wengi ni viongozi. Unaweza kubuni Saluni ya watoto yenye picha za watoto, silabi na picha za Yesu badala ya saluni ambazo ukutani kuna picha chafu za uharibifu.

Wakristo si wana maombi tu, bali ni wauzaji waaminifu, watoa huduma bora, wenye lugha nzuri. Mteja anayekuja katika duka au hoteli ya Mkristo anapaswa kukutana na matunda ya Roho Mtakatifu. Furaha, amani, uvumilivu na mengine mengi ambayo yote si tu kwamba, yatamtukuza Mungu bali pia yatakupatia fedha.

Kila mtu anapaswa awajibike na kujitokeza katika utoaji wa huduma bora na uuzaji wa bidhaa bora. Kutokujiamini kwa watu wengi kunatokana na watu hao kushindwa kumwamini Mungu hivyo kumtanguliza Mungu ni jambo jema lakini si la mwisho. Baada ya kumtanguliza Mungu biashara na utoaji wa huduma ufuate.

Rais Obama akiwataka wananchi wa Marekani kuwajibika alisema, “Hata kama Serikali itatoa elimu bora, hata kama serikali itaweka miundombinu bora ya elimu bado mzazi atawajibika, usitegemee serikali itakuja nyumbani kwako kuzima televisheni ili mtoto wako afanye kazi ya nyumbani (home work) kama mzazi unawajibu wa kuzima televisheni”.

0 comments :