Moto wa milele upo
MOTO WA MILELE UPO
(Neno liko kama lilivyo wala si zito)
Ben
Carson ni mwanataaluma mstaafu, mwandishi na mwanasiasa ninayempa heshima
kubwa. Lakini kuna eneo moja tunatofautiana sana ki-msimamo na ndugu Ben
Carson. Ben haamini katika moto wa milele licha ya kwamba, neno la Mungu
linasema kuna moto wa milele, linasisitiza waziwazi jehanamu ya moto ipo.
Ben
anajenga hoja kwamba, “Mungu hawezi kumhukumu mtu aliyefanya makosa kwa miaka
sitini (60) adhabu ya milele labda adhabu ya miaka sitini (60)”. Ben anaona ni
afadhali mtu akikosa kwa mwaka mmoja akae Jehanamu kwa mwaka mmoja, ni mawazo
yake. Mawazo ya mwanadamu yeyote kama Ben si ya kusikilizwa ikiwa tu
yanakinzana na neno la Mungu. Neno litasimama imara hata kama wanasiasa wote
watalipinga hata kama ulimwengu wote utalikataa. Alichosema Yesu kitabaki pale
pale, neno lake halibadiliki kamwe. Yeye mwenyewe amesema, “Mimi ni Mungu, Sina
kigeugeu”
Jehanamu
ilikuja kama dharura, katika uumbaji hatusikii Mungu akiumba Jehanamu.
Mwandishi wa kitabu cha Mwanzo, Musa haoneshi kama hapo mwanzo jehanamu
iliumbwa. Mungu hakuumba watu au Malaika ili awaangamize, wote aliwaumba kwa
utukufu wake. Lusifa alipokosa ndipo Jehanamu ilipoundwa kwa ajili yake na si
kwa ajili ya wanadamu. Jehanamu ni kwa
ajili ya shetani ambaye ni muasi, wanadamu wakienda huko wanakwenda mahali
ambapo si pao.
Yesu
alisema, “Nakwenda kuwaandalia makao”. Makao ya wandamu ni mbinguni mahali
alipo Yesu. Ukiangalia mateso yaliyoko Jehanamu utagundua si eneo ambalo Mungu
anataka watu wake waende. Kumbuka alipoweka bustani nzuri ya Eden, ikiwa na
mito, miti mizuri, ndege, samaki na wanyama wazuri ndipo alipowaweka Adamu na
Eva. Je, alipoweka moto mkali, sehemu yenye kiu kali, sehemu ya mateso na dhiki
kuu alimkusudia nani? Bila shaka alimkusudia shetani na malaika zake. Ufunuo 20:10 “Na yule Ibilisi, mwenye kuwadanganya, akatupwa katika ziwa la moto na
kiberiti, alimo yule mnyama na yule nabii wa uongo. Nao watateswa mchana na
usiku hata milele na milele.”
Watu
wengi hawaamini katika uwepo wa moto wa milele na kama wangeliamini basi
wangelibadilika. Lakini ukweli ni kwamba, moto wa milele upo. Watu wataungua
usiku na mchana, watu watalia na kusaga meno. Wataona kiu bila ya kupewa maji,
wataishi motoni milele, yaani bila mwisho. Na iwapo mtu ye yote hakuonekana
ameandikwa katika kitabu cha uzima, alitupwa katika lile ziwa la moto. Ufunuo 20:15
Siku
moja nikiwa ofisini dada mmoja alinieleza kwamba, anampenda Mungu lakini hawezi
kuacha dhambi. Kwa kuwa napenda kuhubiri nikaamua kurefusha maongezi huku nikimweleza
jinsi jehanamu palivyokuwa pabaya. Ni kweli pasipo neema ya Kristo na msalaba
wake hatuwezi shinda dhambi, lakini ni lazima tujue sana kuhusu matokeo ya
kudumu ya dhambi (eternal repercussions).
Nilimweleza
kwa hekima, Ok! Unaona ugumu kuacha dhambi vipi umejiandaaje kuikabili jehanamu
ya moto. Kila tunapotenda dhambi kwa lugha nyingine tunasema, tuko tayari kwa
jehanamu, tuko tayari kwa jehanamu ya moto. Binafsi ninaogopa ni heri nitubu na
kugeuka.
KInachowafanya
watu wapende jehanamu na kumkataa Mungu ni uhuru. Wanataka wafanye kile miili
yao inapenda, wavae kili miili yao inajisikia, waishi wanavyotaka, na waseme
wawezavyo. Hawataki kujitia chini ya mamlaka ya Mungu na Kristo wake.
Waefeso 5:5 “Maana neno hili mnalijua hakika, ya kwamba hakuna mwasherati wala mchafu
wala mwenye tamaa, ndiye mwabudu sanamu, aliye na urithi katika ufalme wa
Kristo na Mungu.” Hawafanyi kwa bahati mbaya, Biblia
inasema wanajua. Uhuru wowote unaoturuhusu kulidharau neno la Mungu ni utumwa.
Sheria za nchi zinazopingana na neno la uzima ni pingu ya milele kwa raia wa nchi
husika. Chagua moja leo mbinguni au Jehanamu?
Tubu
ufalme umekufikia leo. Kama uko tayari kugeuka sema pamoja na mimi: “Bwana
Yesu wewe ni mwenye haki na mimi ni mdhambi. Unirehemu Bwana na uyafute makosa
yangu yote. Uniumbie na moyo safi kwa maana, sina moyo safi. Nipe na Roho wako
Bwana aniongoze tena. Amina”
0 comments :