Linda sifa yako nzuri
(Mwenendo wangu ni mzuri kuliko
uzuri wa huyu dada)
Manukato
au marashi husifika kwa kutoa harufu nzuri sana, hata hivyo harufu hiyo haiwezi
kwenda mbali ukilinganisha na sifa njema. Sifa njema huenea kijiji kizima,
manukato hayana uwezo huo. Sifa njema huenda mbali sana mahali ambapo manukato
hayafiki. Nelson Mandela, nani asiye mjua? Yesu Kristo Mfalme, nani aisiyemjua?
Askofu Desmond Tutu, nani asiyemjua? Vipi kuhusu sifa za mama Teresa? Sifa za
hawa wote zimeenea mno.
Imenenwa
katika Mhubiri 7:1a “Heri sifa njema
kuliko manukato mazuri” ikiwa na maana, heri mwenendo bora na halisi kuliko
mwenendo mbaya na feki. Ikimaanisha heri kuwa na mwenendo mmoja wa kweli kuliko
kuwa mnafiki. Heri kuonesha tabia yako ya ndani kuliko kuificha. Manukato au
marashi hutoa harufu ambayo kwa asili si ya mtu. Hata kama mtu hujaoga manukato
yanauwezo wa kufanya anukie vizuri. Manukato yanaficha uchafu wala hayauondoi.
Manaukato yanakusanya uovu na kuupa harufu ya wema.
Jina
jema ni jumla ya matendo yako, jina jema ni kitambulisho chako. Marhama au
manukato [perfume] hufanya tunukie vizuri hata kama moyoni mwetu tumeoza kwa
sababu ya dhambi. Maandiko yanatutaka tuchague jina jema. Ninafananisha jina
jema na utakatifu wa ndani na manukato ni harufu inayoficha ile dhambi ikaayo
ndani ya mtu.
Siku
moja tulikuwa mahali fulani na kulikuwa na dada mrembo kweli kweli. Na wengi
walimtolea macho, na rafiki zangu walitamani na mimi nitoe macho. Kwa kweli
alikuwa dada mlimbwende lakini haina maana yoyote kama kila tunapokutana na
mrembo tunashindwa kujitawala. Kushindwa kujizuia ni dalili ya watu wa siku za
mwisho. “…Wasiojizuia…” 2Timotheo 3:3
Rafiki
zangu walitaka nichangamkie fursa ya yule dada wakiniambia, “pastor vipi” yaani,
“mchungaji vipi” na mimi nikawajibu kizungu, “my character is beautiful than
the beauty of this lady” yaani, “mwenendo wangu ni mzuri kuliko uzuri wa huyu
dada”. Mara nyingine tumepotea kwa sababu tumekwenda haraka bila ya kujali muda
mwingi ambao tumetumia katika kujenga haiba, tabia na wasifu wetu.
Dada
mmoja aliniambia kwa masikitiko jinsi sifa yake ilivyoharibiwa haraka na kaka
waliyeingia naye kwenye uhusiano. Aliandika kwa huzuni, “ameharibu sifa yangu
yote”. Huenda ni sifa ambayo aliijenga kwa muda mrefu ya mwenendo bora.
Imeharibiwa katika mwendo wa sekunde tu!
Katika
karne hii waaminifu na wenye mwenendo bora wamekuwa bidhaa adimu. Watu
hawaamini kama utakatifu unawezekana tena. Hawawezi kukubali kama utawaambia
wewe si mlevi wala si mwasherati. Rafiki yangu hupenda kusema, “simba akisema
hali nyasi hajidai ndivyo alivyo”. Leo
hii tabia nzuri zimekuwa adimu, dunia haimini kama Simba hali nyasi, inachojua
ni kwamba kila mtu ni mwovu tu.
Kuna
jambo linashangaza kidogo, wakati mji mzima wa Ninawi ukiokoka, mji mzima wa
Sodoma na Gomara uliangamia. Yaani wakati mkoa fulani wote unaokoka mkoa
mwingine wote unaangamia. Kanuni ni hii, ni vigumu kumpata mtakatifu katikati
ya waovu, na ni vigumu kumpata mtu mwovu katikati ya watakatifu. Miji hupambana
kuhakikisha ama ni uovu tu unaoshamiri au utakatifu tu ndio unashamiri. Kwa
asilimia hamsini mtu ni mazingira yake. Pastor Sunday Adeleja anasema, “Mazingira
yanatutengeneza kwa takribani asilimia 50” sisi pia ni matokeo ya mazingira yetu.
Kazi
ya wahubiri ni kufanya mazingira ya mbinguni yaje duniani, ambayo ni amani,
utakatifu na uaminifu. Dunia ni kama msitu mkubwa ambao wanyama wote hula
nyasi. Sasa wanyama walao nyasi hawataki kuamini kwamba wapo wasiokula nyasi,
simba hali nyasi. Ndivyo walivyo watakatifu katikati ya ulimwengu ambao BWANA
mwenyewe amesema ni wa mbwa mwitu. Chukua muda huu kutafakari tabia, mwenendo
na haiba yako na kisha amua kubadilika na kuulinda mwenendo wako mzuri. Mpaka
wiki ijayo Shallomu…
0 comments :