Swali lililowapoteza wengi
SWALI LILILOWAPOTEZA WENGI
(Nitakula nini, Nitavaa nini)
Kujiuliza
kwamba, utakula nini na utavaa nini ni swali ambalo limewapoteza wengi, wengi
kwa kujiuliza swali hilo wameachana na wito wao. Wengine wamepoteza wito wao
kwa kujiuliza kuhusu wazazi wao na jamaa zao, watakula nini na watavaa nini.
Naamini
wazi ni kwa sababu hiyo Yesu alitutaka tusijiulize swali hilo. Aliwataka wanao
mwamini waachane na swali hilo. Alitumia mfano wa maua ya kondeni na ndege wa
angani ambao hawapandi wala hawavuni lakini wanaishi, alisema sisi ni bora
zaidi mbele zake kuliko ndege wa angani. “Akawaambia wanafunzi wake, Kwa sababu hiyo nawaambia, Msisumbukie
maisha yenu, mtakula nini; wala miili yenu, mtavaa nini.” Luka 12:22
Yesu
anasema hatuwezi kutumikia mabwana wawili, hatuwezi kutumikia Mungu na mali.
Unapoitwa ni lazima uchague kimoja. Wengi wanapoitwa katika uinjilishaji
wanakataa kwa sababu biashara zao zitakufa. Wengi wanaoitwa katika wito wa
ukombozi wa nchi zao au wa roho za watu wanakataa kwa kuwa jambo hilo litaumiza
wanaowategemea kwa chakula na mavazi.
Rai
yangu kwako leo ni kwamba, unaposikia kuitwa na Mungu kufanya kazi fulani
usijiulize swali ambalo Yesu ametukataza. Wengi wamejikuta wanaogopa kupigania
haki kwa sababu tu itaathiri kipato chao au chakula chao. Wito wako ndio
kitambulisho chako, kukataa wito ni kujikataa. Wengi wanajulikana kwa majina ya
wito wao: mwalimu, mwinjilisti, mchungaji, kiongozi, waimbaji, wasanii na
wabunifu.
Wito
unaleta faida kwa watu wengi zaidi kuliko sisi na familia zetu, mamilioni ya
wana wa Israeli walitegemea utii wa Musa, Mamilioni ya watu wa Afrika kusini
walitegemea utii wa hayati mzee Nelson Madiba Mandela.Tunapoishi kwa ajili ya
Mungu tunaishi kwa ajili ya watu wengi ambao kwa hakika hata si ndugu zetu wa
damu. Pastor Chris Oyakhilome anasema,
“It is the spiritual family that means so much to God, It is not for your
biological family” yaani, “Ni familia yako ya kiroho ndiyo yenye mashiko zaidi
mbele za Mungu, wala si kwa ajili ya ndugu zako wa damu”
Ingawaje
kwa asili Musa alikuwa Mwebrania lakini kimwili alikuwa ni mwana wa binti
Farao, alijulikana kama mtu anayetokea katika familia ya kitajiri. Angeliweza
kukubali kuishi kwa ajili ya familia ya Farao. Lakini familia ya kiroho ya Musa
ilihusisha watumwa, watu wasio na kitu, watu wanaoteswa utumwani. Musa aliitwa
kwa ajili ya watu wasio na kwao, uwe na hakika wito wako utakuletea familia na
utapaswa kuteseka kwa ajili ya familia hiyo.
Bwana
anapokuita na kukutuma kwa ajili ya jambo fulani uwe na hakika hatakupungukia
kwa chochote. Alipowaita na kuwatuma mitume wake hawakuwa na kitu lakini pamoja
na hayo hawakupungukiwa na kitu. Usijiulize kuhusu nguo na mavazi ya ndugu
zako, usijiulize kuhusu chakula chakula chako, mara zote walioitwa walilazimika
kuacha mifugo yao (kondoo), wengine biashara zao(uvuvi) na ndugu zao (wazazi).Katika
hawa wanafunzi wote pamoja na kuacha kila kitu bado hawakupungukiwa chochote,
na Yesu anawauliza mitume wake swali la kuwajenga: “Akawauliza, Je! Hapo nilipowatuma hamna mfuko, wala
mkoba, wala viatu, mlipungukiwa na kitu? Wakasema, La!” Luka 22:35
Wanafunzi walijibu, ”lah!” wakiwa na
maana kwamba hawakupungukiwa na kitu. Katika maisha yetu tumemwona Bwana na
sasa tunakika naye hata jangwani tunajua hatutakosa maji, hata usiku tunajua
hatutaogopa, hata hatarini tunahakika tutatoka salama. Kuna maneno mawili tu
ndiyo twaweza kumjibu BWANA pale tunaposikia kuitwa, nayo ni, “ndiyo BWANA.”
0 comments :