Kwa kila ambaye....... II
KWA KILA AMBAYE HAJAOA AU KUOLEWA - II
(Amua kuwa na familia ya aina hii)
Tunapoandika kwa kila ambaye hajaoa na kuolewa sisi pia
ni wahusika. Tunapokufundisha tunajifunza pia, na nyakati nyingine tunayasema
yale ambayo BWANA ametupa sirini ili kutusaidia. Mengine ni uzoefu wetu
unaotokana na miongo kadhaa ambayo Bwana ametukirimia hapa Duniani, yamkini pia
ni mafunzo kutoka katika kukosea kwetu
au kutoka kwa wale ambao tumepata nafasi
ya kuwafuatilia. Msanii mmoja anasema, “wasio na watoto ndiyo wanajua kulea
vizuri” anamaanisha ndio wanazungumza sana wakidhani ni rahisi wasijue
kinachowapata wazazi katika kulea na kukuza watoto. Katika makala hii
ninaandika nikiwa na tahadhari hiyo kichwani.
Ili kuepuka majuto na sintofahamu kila ambaye hajaoa na
kuolewa azingatie mambo yafuatayo:
Mungu ndiye
atoe jawabu: Hili ni gumu ila ni la kweli na hivyo
hatuna budi kulisema. Maandiko yanaonesha wazi wazi, “BWANA ndiye akataye nena”
pengine imenenwa, ‘’jawabu la ulimi latoka kwake” yote yakimaanisha kwamba,
BWANA MUNGU ndiye mwenye maamuzi ya mwisho na ndiye mwenye sauti ya mwisho.
Yesu alipotaka kuepuka kikombe cha mateso aliomba, alitaka iwe ni mapenzi ya
Mungu kukiepuka na hata alipokipokea bado ilikuwa ni mapenzi ya Mungu. Mwenye
hekima mmoja anasema, “You cannot say, ‘Your will’ without saying ‘not my
will’” Ni kweli hatuwezi kusema tumemwachia Mungu aamue ilhali sisi wenyewe
bado tumeshikilia msimamo wetu. Kinachonifanya nimwombe Mungu si tu ni kwa
sababu nampenda bali ni kwa sababu sijimiliki, Yeye ni muumba wangu na mimi ni
mali yake. Yeye ni mfinyanzi na mimi ni chombo chake. Si urembo, urefu na
utanishati ndio uwe kivutio chetu, la hasha! Chaguo la Mungu ndiyo chaguo letu.
Epuka kumnyima Mungu kuwa mwamuzi wako katika jambo la msingi namna hii. Derek
Prince anakiri kila ilipokuja suala la kuoa mara zote (mbili kufuatia kifo cha
mke wa kwanza) alimtegemea Mungu pasipo kuweka ujuzi wake. Nimefuatilia hekima
ya wengi waliotutangulia, akiwamo Sunday Adelaja, Billy Graham na Derek Prince
kwa ujumla wanashauri watu waoe chaguo la Mungu. Waachane na watu waliowachora
kichwani (chaguo la fikra) badala yake wapokee zawadi toka kwa Bwana.
Jizatiti katika
Viwango vya kimungu (Committed to God’s standard): Ndoa ni ya kimungu, ni wazo lililotoka moyoni mwa Mungu wala si akilini
mwa Adamu. Ziko ndoa za kihindi, za kiafrika, za mkeka, za serikali na nyingine
nyingi. Lakini ndoa hizi kama hazikuwekwa katika viwango vya kimungu ambavyo ni
vya kibiblia si tu kwamba huwa hazina mashiko bali huwa hazikamilishi kazi.
Kusudi la ndoa ni kazi, anayetoa kazi hiyo ni Mungu. Ndiye anajuaye wanaofaa
kwa ufanisi bora wa jukumu hilo. Viwango vya kimungu ni pamoja na kuwa na mke
mmoja tu (msaidizi na si wasaidizi), kuwa na watoto waadilifu, kukamilishana,
kuwa na usafi na utakatifu. Mungu hakutaka kuleta Dunia ya watu bilioni saba
kwa siku moja bali alitaka kwa kupitia familia moja (ya Adamu na Eva)
wapatikane watu wote zaidi ya bilioni saba. Nadhani nia kubwa ni kupata ubora
ule ule wa utakatifu, uchaji na uadilifu. Rafiki yangu aliandika: “Quality is
never an accident, it is planned”
Achana na
ndoto: Kuna rafiki zangu wa kike ambao
walikuwa na ndoto na maono kwamba, tutaoana na sasa hivi wameshaolewa na watu
wengine kabisa; tena kwa ndoa takatifu, na mimi naziheshimu. Kuna wengine
nilipata maono na wao wakapata njozi lakini sasa wako na watu wengine na mimi
nawaita shemeji. Ndoto ni hatari! Ndoto ni njia isiyoaminika. Zamani nabii
akiota ndoto na kuisema au akitabiri na isitimie basi aliuawa. Kama ndoto za
ndoa zingekuwa hivyo basi wengi wangepigwa na kuchinjwa kama manabii wa uongo
mfano wa manabii wa baali walivyochinjwa na Eliya. Naamini ukikaa katika neno
la Mungu utakuwa salama, achana na ndoto. Ndoto zinapoteza wengi kuliko
wanaonufaika. Ndoto za injili na kazi hazina shida lakini za harusi na ndoa
zinamatatizo, si kigezo halali cha kumkubali mtu.
Omba bila
kukoma: Wanaosema hili si la kuombea hawana
tofauti na wanaosema hakuna Mungu. Binafsi najua Mungu atanijibu na kunipa haja
ya ninachostahili katika Kristo. Si tu kwamba najua atanijibu, bali ninajua
tena kwa hakika. Omba kwa bidii kiasi kwamba hata Mungu akijibu usiweze kujua
amekujibu maombi uliyaomba lini bali uwe unajua tu, amekujibu. Nampenda Hudson
Taylor mmisionari mwenye alama anasema, “kila alichonacho ni matokeo ya
maombi”. Hata mshahara wake ulipochelewa hakuthubutu kumwambia kiongozi wake,
bali aliingia kwenye maombi alitaka mshahara wake uwe ni jibu liliotokana na
maombi. Ni furaha namna gani kuwa na familia ambayo baba, mama na watoto wote
ni matokea ya maombi? Nimeshuhudia watoto katika nyumba ya dada yangu
ambao ni matokeo ya maombi, na ni furaha
kuona matunda ya maombi katika ulimwengu wa nyama. Pray, pray, pray
Tukutane wiki ijayo, usikose makala yako. Shallom…
0 comments :