Ishi Maisha Yako
ISHI MAISHA YAKO
(Shughuli hii inakuhusu wewe sisi tumekuja kukusaidia)
Ziko
namna mbalimbali za kuishi, lakini namna bora ya kuishi ni ile itokayo kwa
Mungu na inayoelezwa katika neno lake yaani, katika biblia. Ukiishi nje ya
maisha yanayopendekezwa na Biblia maana yake unaishi nje ya mpango wa Mungu.
Mtu
anaweza kufa kwa niaba yako lakini hawezi kuzaliwa kwa niaba yako. Mungu hawezi
kuruhusu ofisi yako ya maisha ikaimishwe ndio maana hawezi mtu kuzaliwa kwa
niaba ya mwingine. Ni lazima uishi maisha yako. Ngoma ya maisha inakuhusu wewe
ni lazima uicheze. “Inuka; maana
shughuli hii yakuhusu wewe; na sisi tu pamoja nawe; uwe na moyo mkuu,
ukaitende.”Ezra 10:4
Maneno,
“inuka” “wewe” “ukaitende” yanaonesha waziwazi kwamba,
hakuna kukwepa. Watu watalia kwa sababu mhusika unalia, watu watufurahi kwa
sababu mhusika unatabasamu bashasha. Ndivyo anavyonena Robert Frost mshairi
mwenye alama ya aina yake: “No tears in the Writer, No tears in the reader. No
surprise in the writer, No surprise in the reader”.
Kila
unayemwona kwenye maisha yako yupo ili kukusaidia na si kufanya kwa niaba yako.
Yupo kutoa msaada ili wewe ufanye. Marafiki hawataweza kufanya sehemu yako hata
ukiwaita watalala, watalala kwa sababa kazi inakuhusu wewe. Yesu alishuhudia
wanafunzi wake wakilala licha ya kuwataka waamke kuomba. Ni kwa sababu sherehe
ya wokovu ilimhusu Yesu Kristo.
Mambo
yanaweza kufanyika bila pesa lakini si bila ya wewe. Mhusika mkuu wa maisha
yako ni wewe. Wazazi, marafiki na jamaa hawana ruhusa ya kukubadili badala yake
wanatakiwa kukusaidia wewe kuwa wewe halisi. Mariamu mama yake Yesu hakuwa
kikwazo kwa huduma ya ukombozi badala yake aliacha Yesu Kristo awe Yesu Kristo
kweli kweli.
Familia
inaweza kuwa kitalu kizuri cha kukuzia maono na ndoto zako lakini pia inaweza
ikawa kamba nzuri ya kunyongea ndoto zako. Ninaposema familia sina maana ya
ndugu wa damu tu, bali ninawahusisha wote wanakuzunguka na unaoshirikiana nao.
Watu ambao unatumia muda mwingi pamoja nao. Uwe mwangalifu uwapo katikati yao!
Je,
ukiondoa shinikizo la wazazi, ungependa kuwa nani? UKiondoa mambo ya umasikini
ungesomea nini? Je, ukiondoa shinikizo la mgandamizo wa uchumi ungependa
kufanya kazi gani? Je, ukiondoa hofu zako ungependa kuanzisha nini? Hayo ambayo
ungeyafanya isipokuwa umezuiliwa kwa sababu ya ukosefu wa pesa, shinikizo la
wazazi na umasikini hakikisha unayafanya.
Mgombea
wa nafasi ya Urais katika uchaguzi wa sasa nchini Marekani Donald Trump
ameandika hivi katika moja ya vitabu vyake, “Its crucial to be true to yourself
true to your own choices” yaani, “Ni muhimu sana kuwa muwazi na mkweli kwako
binafsi na katika chaguzi zako.” Trump anataka tuwe wazi kwa nafsi zetu,
tusiidanganye mioyo yetu. Uwe muwazi, fanya upendacho ili uwe unachotaka. Mimi
ninapenda kuhubiri habari za Yesu, tazama! hata sasa ninamhubiri.
Zawadi ya kwanza ambayo tunaipata toka kwa
Mungu ni zawadi ya uhai. Ni zawadi ambayo ni ya pekee sana ambayo ni zawadi
binafsi. Mungu ametupa uhai ili tuishi kwa ajili yake, tufanye aliyotupangia
hata kama wengine hawatayakubali. Mimi pia nimekuja kukusaidia, kwa heri mpaka
wiki ijayo, Shallom….
0 comments :