Usiogope; Yesu Yu Hai

11:40:00 AM Unknown 0 Comments


USIOGOPE, YESU YU HAI
(Sasa ni Haleluyah) 

Rejea toleo la 12 katika blog yetu lililokuwa na kichwa, “Ogopa kuogopa” (http://lifeminusregret.blogspot.com/2015/08/ogopa-kougopa.html).  Ni kweli kama wakristo hatuna sababu ya kuogopa, na kwa wale ambao wanaona hawawezi kabisa kuisha bila hofu hao tunawasihi angalau waogope kuogopa. Si unajua hata daktari akiona hauna ugonjwa unaokusumbua, lakini unadai unaumwa huwa anaandika panadol, basi dozi yako “ogopa kuogopa”.
Mchungaji David Wilkerson Yule wa kitabu cha “ Wahuni waliobadilika” amekuwa mfano mzuri kwetu. Moja ya kauli zake anasema: “Worry is the tendency of those who have no heavenly Father” yaani, “Hofu ni tabia ya wale wasio na Baba wa mbinguni”. Yesu anasema msijisumbue mtakula nini wala mtavaa nini. Umewahi kujiuliza ni kwa nini Yesu anasema hivi? Jibu ni rahisi; tunaye Baba yetu wa mbinguni ajuaye kama tunahitaji hayo.
Hofu inaletwa na uyatima, hofu ni ukosefu wa Baba wa mbiguni. Kwa watu wa mataifa hofu kwao ni ibada. Mtoto asiye na wazazi ni lazima ajitafutie kila kitu, ni lazima ajilinde na ajisimamie. Majukumu haya huwa ni mazito na hivyo humfanya aishi katika hofu. Lakini sivyo ilivyo kwa wakristo, sisi tumeitwa kupumzika, Baba yuko kazini.  (Mathayo 11:28)
Kikomo cha hofu ni pale mtu anapofanyika Mwana. Njia ya kufanyika mwana ni kupitia Imani kwa Yesu Kristo. Imeandikwa, “Bali wote waliompokea [Yesu Kristo] aliwapa uwezo wa kufanyika wana wa Mungu ndio wale waliaminio Jina lake” Yohane 1:12
Mara mtu anapofanyika mwana anapaswa kuachana na tabia za watu wa mataifa ambao hawana Baba mbinguni ila duniani tu. Mhubiri mmoja anasimuli, alipokuwa akiomba bibi yake alimsikia na akamkosoa kwa kumwambia, “Unaomba vibaya”. Alipomuuliza bibi kwa nini unasema hivyo? Bibi yake akamjibu, “Unaomba mambo madogo Mungu ni Mungu Mkubwa”. Ni kweli, ingawa tunaye Baba wa mbinguni anayejishughulisha na mambo yetu lakini bado wengi wetu hawajui kuringa, hawajui kuomba mambo makubwa wanasumbukia mambo ambayo wasio na Baba wa mbinguni husumbukia pia. Mungu atusaidie tufanywe upya nia zetu!
Kifo cha Yesu kilikuwa sababu pekee iliyofanya mitume wake waogope. Walikuwa wanashinda ndani, milango ikiwa imefungwa kabisa. Leo hii Yesu Kristo yuko hai lakini bado wakristo wanaogopa. Kwa jinsi wakristo walivyo wengi, kama kila mmoja angetembea katika faida ya ufufuko wa Yesu basi badala ya kusikia, kokolikoo…. asubuhi mapema  tungesikia Haleluyah….Haleluyah…Haleluyah…. Haleluyah
Ninafanya hivyo karibia kila siku ninapo tafakari pendo lililo msukuma Mungu Baba kuandika mpango wa wokovu. Na mwisho wa tafakari yangu jadidi huwa ni Haleluyah, Haleluyah. Ni kweli, hakuna awezaye kumshinda mtu anayemsifu Mungu. Mitume walipata mashaka wakidhani Yesu ataoza kaburini, lakini siku ya kwanza ya juma Yesu alitoka kaburini akiwa hai na hivyo akafuta sababu zote za kuogopa.
Tunataka kujenga kizazi kisichoshangilia matangazo ya vifo, bali kinachosisimka kisikiapo habari za Yesu Yule aliyetoka kaburini. Yule ambaye kaburi lilishindwa kumshika, Yule ambaye mauti ilishindwa kummudu. Yule ambaye kifo kilimwachilia upesi kisimshike tena. Oh! ingekuwa mbaya sana kama Yesu angekaa kaburini milele kama walivyokaa babu zetu na bibi zetu. Huenda tungekuwa wanyonge na wenye hofu. Lakini kwa kuwa Yesu Kristo amefufuka, Simba wa kabila la Yuda, sasa ni Haleluyaaaaaaaaaa, Oh Glory……
Mpe Bwana utukufu maaana Yu hai milele.

0 comments :