Napendekeza Usikope - II

1:53:00 PM Unknown 0 Comments

 
NAPENDEKEZA USIKOPE
(Makala ya Pili)

Katika toleo liliopita niliahidi kuendelea kujenga hoja yangu katika toleo hili. Hoja iliyomezani ni pendekezo langu kwamba, usikope. Mikopo inapaswa kutumika tu kama daraja la kuelekea kutokukopa (debt is a means to a debt free life)
Nimefanya utafiti kwa kusoma vitabu kadhaa vya kifedha kikiwepo, Money Master The Game cha Anthony Robins, The Richest man In Babylon cha George S Clason na vingine vingi. Katika vitabu hivyo mikopo haitajwi kama siri ya utajiri. Kwa mtazamo wangu, mkopo ni dharura sasa ni hatari kama kila siku itakuwa ni dharura. Yes! It’s dangerous if every day is an emergency day. Kanuni ya kumkimbiza mwizi inatudai tufunge mlango kwanza ndipo tumkimbize, vinginevyo unaweza ibiwa mara mbili. Hapa ni vema tufunge mlango ndipo tupambane na umasikini.
Mkopo unatoa ishara zifuatavyo:
1.      Ni dalili ya kupungukiwa. Tunawezaje kusema tumebarikiwa ikiwa tunamadeni? Hudson Taylor ni mmisionari aliyekataa kukopa anaeleza kwamba, tukikopa kwa lugha nyingine tunatamka kuwa Mungu ameshindwa kukutana na mahitaji yetu ndio maana tumeamua kukopa ili kujisaidia wenyewe. Maandiko yanasema, “Kwa kuwa yeye mwenyewe amesema, Sitakupungukia kabisa, wala sitakuacha kabisa.” Waebrania 13:5c
2.     Ni kinyume cha baraka, Neno la Mungu halichagizi kukopa. Moja ya Baraka kwa warithi wa Ibrahimu ni uhuru wa kifedha, si baraka kuu lakini ni moja ya baraka. Unaweza kukubali au kukataa kuwa sehemu ya ahadi hii, hilo ni juu yako ndugu: “nawe utakopesha mataifa mengi, wala hutakopa wewe” Kumbukumbu 28:12 Si kila tajiri anauhusiano mbaya na Mungu, na si kila masikini ni mcha Mungu. Uhusiano na Mungu unajengwa na namna tunavyovitumia vitu tulivyonavyo na kuwa navyo au kutokuwa navyo si kosa.
3.     Ni kizuizi cha kutoa fungu la kumi, Shetani anaweza kutumia mikopo kuwashawishi watu wasitoe fungu la kumi ambalo ni chanzo kikubwa cha Baraka. Nimewahoji watu kadhaa wenye mkopo mmoja na zaidi ya mmoja na kati yao hakuna hata mmoja anayetoa fungu la kumi la mshahara wake. Sababu mikopo imefanya mshahara wao umekuwa mdogo ukilinganisha na matumizi. Mmoja aliniambia alishasahau kutoa fungu la kumi, anaomba Mungu amsamehe.
4.     Inaua ubunifu, Mtu akishaifanya mikopo kuwa suluhisho la maisha yake hujisahau na hivyo si rahisi kwake kutumia njia sahihi za mafanikio kama vile: kuweka akiba, kuwekeza, na kupunguza matumizi yasiyo ya lazima.Kuna msemo usemao: “Pesa mikononi mwa Muhindi {Indians} hukaa sana kuliko mikononi mwa Mwafrika {Africans}” Usemi huu unaonesha jinsi Waafrika tulivyo na tabia kula pesa kwa haraka, na kuwa na matumizi mengi na hivyo hela haikai mkononi kwa kitambo kirefu, ilhali wengine huzalisha kidogo wapatacho na kukiongeza.
5.     Ni dalili ya utumwa. Biblia inasema wazi “Naye akopaye ni mtumwa wake akopeshaye” {Mithali 22:7b} Kuna furaha ambayo hurejea mara mtu anapomaliza kulipa deni au mkopo wake. Ni wazi furaha ile ambayo hurejea siku mtu anapolipa deni ndiyo furaha aliyoipoteza siku alipoingia katika deni. Utumwa wa kimwili na kifikra huanza kwa utumwa wa kifedha. Si rahisi kuyakataa mawazo ya mtu anayekudai, ndio maana nchi masikini hazina sauti, hazisikiki hata zikisema kwa nguvu. Waswahili husema, “dawa ya deni ni kulipa” maana yake, deni ni ugonjwa, deni ni usumbufu na kero na ili tuwe huru lazima tulipe na tusikope tena.
Suluhisho: Wiki ijayo nitataja njia kadhaa za kukusaidia kutoka katika mikopo na kuelekea utajiri. Usikose makala ya wiki ijayo itakayokueleza njia za kukutoa katika mikopo hadi utajiri. Shallomu! Peace and Prosperity upon you


0 comments :