Napendekeza usikope
NAPENDEKEZA USIKOPE
(Makala ya Kwanza)
Kukopa
katika benki (taasisi za fedha) ili kujikomboa kiuchumi ni sawa na kujificha
chini ya transifoma ya umeme wakati mvua kali yenye kuambatana na radi ikinyesha.
Benki nyingi hazikopi hovyo na zikilazimika kukopa hufanya hivyo ili
kuwakopesha wengine. Wanakopa ili kukopesha na kuwekeza. Je, ni watu wangapi
ambao wana mikopo benki; walichukua mikopo hiyo ili kukopesha wengine au ili
kuwekeza kwa lengo la kupata riba? Mpaka tumejitazama na kuhamia katika nafasi
ya benki hatuwezi kupata matokeo mazuri kama benki zipatavyo faida katika
mikopo yake. Kwa kweli nalazimika kukumbuka na kujaribu kutafsiri maneno ya
mshairi huyu: “Benki ni mahali wanapokupatia mwavuli wakati hali ya hewa ni tulivu na
kukutaka urejeshe mara tu mvua itakapo anza kunyesha” Robert Frost
Inawezekana
ujumbe wangu ukaleta ukakasi masikioni mwako na ganzi katika meno yako, ndiyo!
Sote tumelelewa na kukua huku; nchi, wazazi, walezi pamoja na jamaa zetu
wakikopa na hivyo makala hii inakabiliwa na upinzani mzito kutoka katika
Historia. Sijui kama unajua, mtoto akizaliwa jela hupaita nyumbani badala ya
gerezani. Tuliozaliwa katika mazingira yenye changamoto lazima tufikiri kwa
upya namna ya kutoka katika ombwe la mikopo. Namna ya kuvunja kawaida isiyofaa. Kawaida nzuri au utamaduni mzuri waweza kuwa
sheria lakini si busara kuacha kawaida mbaya kuwa kama sheria.
Kuna
watu wanakopa kwa sababu hawataki kupunguza matumizi yasiyo ya lazima. Kuna
matumizi mengi tunayafanya na hayana tija ndani ya dakika tano zijazo. Ni
matumizi ambayo hutupatia furaha wakati tunapoyafanya na baada ya hapo kilio. Mwenye
hekima mmoja anasema, “Ikitokea bahati mbaya mchimba shimo akajikuta ndani ya
shimo jambo la kwanza analopaswa kufanya ni kuacha kuchimba shimo hilo ili asijichimbie
kwenda kina kirefu zaidi”. IKiwa uko katika madeni na mikopo isiyokwisha jambo
la kwanza la msingi ni kuamua kuacha kukopa. Ninapendekeza usikope katika benki
na taasisi nyingine zenye kutoza riba kubwa.
Mikopo
inadumaza akili, inakutaka uwe mteja wa benki kila siku tena haikupi nafasi ya
kufikiri kama benki. Badala ya kuwaza
kukopesha watu wengine, milele utakuwa ukiwaza kukopa. Wakati wewe unawaza
ukope shilingi ngapi, benki wanawaza wakutoze riba kiasi gani. Umewahi kuwaza
kwamba kusingekuwa na mikopo ungeishi vipi? Ni kweli kwamba, hakuna namna
nyingine ya kuishi isipokuwa kwa kukopa
tu? Naamini jawabu ni hapana.
Jambo
la kwanza kabla ya kufanya uamuzi wa kukopa si kuitazama shida yako bali ni
kuangalia masharti ya mkopo husika. Je, unauwezo kiasi gani wa kuyasoma na
kuyadadavua masharti ya mkopo? Kesi ya meno hupelekwa kwa daktari wa meno,
mambo ya nyota kwa mamajusi iweje mambo yahusuyo pesa yaende bila idhini wala
ushauri wa mtaalamu yeyote? Ni vizuri
wataalamu wakupe ushauri kuhusu mkopo wako, na wataalamu hao wawe ni nje ya
benki. Kesi ya nyani usimpelekee tumbili.
Kila
tunapokopa kwa lugha nyingine tunatangaza kwamba sisi si wabarikiwa. Je,
unalijua na hili? Tunapokopa tunamaanisha tumepungukiwa ilhali ahadi inasema
hatuta pungukiwa: “Msiwe na tabia
ya kupenda fedha; mwe radhi na vitu mlivyo navyo; kwa kuwa yeye mwenyewe
amesema, Sitakupungukia kabisa, wala sitakuacha kabisa.” Waebrania 13:5
Tafakari
halafu Chukua hatua, usikope hovyo. Wiki ijayo nitaendelea kujenga hoja ili
tujue ubaya wa mikopo hii ni kulingana na utafiti nilioufanya kwa kuwahoji na
kutazama mwenendo wa jamii ya sasa. Hadi wiki ijayo, Shalomu!!!
Kwa
maswali au maoni kuhusu hili tuandikie
katika email na blog yetu.
0 comments :