Nuia Kuacha Alama - II

10:18:00 AM Unknown 1 Comments

 
NUIA KUACHA ALAMA - II
(“Nani atalia utakapokufa” Robin Sharma)

Kila mwanadamu anawajibu kwa Mungu na kwa jamii yake. Rafiki yangu hupenda kusema, “Wajibu mkubwa ulionao ni kutambua au kujua kuwa unawajibu” (The greatest responsibility is to know, that you are responsible). Tunapozungumza kuhusu kuacha alama (legacy) hatuzungumzi kuhusu kuacha majengo au vito vya thamani; bali tunazungumza aina na mfumo wa maisha utakaokuwezesha kuishi kwa ufanisi hapa duniani; kugusa maisha ya watu na kuacha alama katika mioyo yao.
Watu wote walioacha alama walijua kwanini wapo duniani katika nyakati zao, walikuwa tayari kutumia uwezo ulikuwa ndani yao ili kuwafaidia watu wengine na kugusa maisha yao; walijua wanawajibika kwa jamii zao na kwa vizazi vitakavyo kuja baada yao. Kazi zao na kujitoa kwao kumerahisisha maisha yetu ya sasa, na kufanya ulimwengu kuwa bora zaidi. Hata mimi na wewe tunaowajibu wetu kila mmoja, swali la kujiuliza je tutautimiza wajibu huo kikamilifu?
Mwandishi wa kitabu cha The leader who had no title, Robin Sharma amewahi kuandika chapisho, “Nani atalia utakapokufa” Hii ikiwa na maana kwamba, je! ni jambo gani litabaki hai kama alama utakapomaliza utumishi wako hapa duniani? [2Tim4:6-8]
Katika jamii ya Wayahudi endapo mtu angekufa na jina lake likasahaulika haraka katika jamii hiyo ilihesabiwa kuwa ni laana. Watu wengi walioacha alama wanaishi zaidi wanapokufu kuliko wanapokuwa hai, umaarufu wa Princes Diana uliongezeka zaidi baada ya kifo chake kuliko alipokuwa hai, vivyo hivyo Yesu Kristo. Tunapaswa kuishi kwa nidhamu ambayo itatupatia maisha hata tutakapokuwa kaburini.
Utakapoondoka duniani unataka watu [jamii yako, familia yako, rafiki zako] waseme wewe ulikuwa mtu wa namna gani? Au ungependa vizazi vijavyo baada ya wewe viseme wewe ulikuwa mtu wa namna gani? Ungependa utambulike kama mtu wa namna gani? Muadilifu? Mfano wa kuigwa kwa vijana? Mkarimu? Mtu aliyetumia uwezo wake kumtukuza Mungu na kuwafaidia wengine? Mtu aliyeishi kwa ufanisi [effective life]?
Utakapoanza kujiuliza maswali haya mara kwa mara; ghafla utapata kutambua na kujua namna ikupasavyo kuishi kulingana na kile unachotaka kisemwe baada ya kuondoka kwako. Kile unachotaka kisemwe kuhusu wewe, Anza kukiishi sasa; usisubiri kesho. Kumbuka, usiniambie unachoweza kufanya; nioneshe.
Kile tulichokifanya kwa ajili yetu tu, hufa na kuzikwa pamoja nasi kaburini; lakini kile tulichokifanya kwa ajili ya wengine na kwa ulimwengu, huendelea kuwepo hata wakati sisi hatupo”-Albert Pike, (Tafasiri ya mwandishi)


1 comment :