Napendekeza usikope III
NAPENDEKEZA USIKOPE
(Makala ya Tatu)
Leo
nitaanza kutaja njia za kuondokana na madeni. Wengine husema mbona kwenye
biblia kuna mfano wa kabaila aliyetoa talanta. Ni kweli upo, lakini waliochukua
talanta walikuwa na lengo la kuzalisha na walifanya hivyo. Vipi wewe tangu
uanze kuchukua mikopo umezalisha kiasi gani? Tunakopa ili kutengeneza njia ya
kutokukopa tena, lengo lingine kinyume na hili ni batili. Walichukua
wakazalisha zaidi na nina amini baadaye walirudisha pesa za kabaila na wakapata
mitaji yao na kuendelea na maisha yao bila kudaiwa na mtu yeyote.
Matendo
yetu hayana nguvu ukilinganisha na kanuni zilizotusukuma katika kutenda matendo
hayo. Kama kanuni iliyomsukuma mtu { kukopa} haina msaada basi hata atende kwa
umakini wa kiwango cha juu sana bado matokeo yatakuwa mabaya. Kanuni lazima
ifafanue sababu. Kwa nini unakopa? Utakopa mpaka lini?
Ile
kwamba benki wana hela haina maana lazima twende tukakope, kabla ya kukopa ni
lazima nijiulize na kupima ufanisi na uzoefu wangu katika kujitawala na kutumia
mkopo. Kinachotokea katika maisha ya sasa ni mkopo unazaa mkopo badala ya mkopo
kuzaa uhuru wa kifedha. Wako ambao wamekopa hadi hawakopesheki tena, Hii ni
hatari!
Usitegemee
mfanyakazi katika taasisi inayotoa mikopo akwambie kwamba, mikopo ni mibaya.
Udhaifu wa wateja ndio utajiri na ujazo
tele wa mshahara wake. Inahitaji mtu huru kama mwandishi wa makala haya kuweza
kulisema jambo hili. Ili utoke kwenye madeni fanya yafuatayo:
- Andika Malengo yako ya kifedha: Ni rahisi kufanya kazi au biashara kuliko kuandika malengo, ndio maana watu wengi wanafanya biashara na kazi bila kuandika malengo yao. Kama ni rahisi wangeandika. Malengo yako lazima yawe na ukomo kama asemavyo Napoleon Hill: “Goal is a dream with deadline”
Unahitaji shilingi ngapi katika muda
gani? Unahitaji pesa hizo kwa ajili ya nini? Malengo yako lazima yafafanua
mambo haya.Kuna kitu cha ajabu kinatokea unapopanga na kukabidhi malengo yako
kwa Mungu. Nimeona Mungu akinisaidia katika malengo yangu na mipango yangu ya
mwaka huu. Kupanga ni kutumia masaa machache kuishi mwaka mzima, ni kutumia
siku moja kuishi mwaka mmoja.
Malengo yako ya kiuchumi yanapaswa
kuwa ni zaidi ya kujikimu yaani, zaidi ya kumudu gharama za maisha (maji,
nauli, umeme, chakula, ada, pango na maradhi). Ni vyema uandike malengo na
mipango ya kukuza uchumi wako. Wanaondika malengo yao hupata kipato maradufu
ukilinganisha na wale wasio andika. Asilimia 5% ya watu ambao huandika malengo
yao tafiti zilizofanyika huko Marekani zinaonesha ni wenye kipato kizuri kuliko
asilimia 95% isiyo weka malengo kwa maandishi. Meneja wa Tigo wa Kanda ya
nyanda za juu kusini alisema, “nikishapanga malengo yangu na kuyaandika
huyawasilisha kwa mke wangu na mke wangu husaini kama ameridhia au lah!”. Dr
Myles Munroe anasema, “Mungu ni Alpha na Omega kwa sababu, Yeye hupanga mwanzo
na mwisho wa kila jambo”. Tujifunze kwa Mungu kwa kuanza kupanga na kuandika
malengo yetu ya, kiuchumi, kijamii na kitaaluma.
- Punguza matumizi: Mikopo si suluhisho la kudumu la matatizo ya kifedha bali ni suluhisho la haraka. Nadhani tunapaswa kwenda katika uhuru wa kifedha wa kudumu badala ya jawabu la msisimko (lasting financial freedom rather than momentary and romantic answer). Kanuni zinaeleza wazi tukitaka uhuru wa kifedha ni muhimu kuzalisha kuliko matumizi yetu ili tupate ziada. Kanuni nyingine ni ile ya kupunguza matumizi yetu ili tunachopata kitoshe na pengine kitupatie ziada. Hatupunguzi matumizi haya milele bali kwa muda tu wakati tunatoka kwenye madeni na tunapandisha juu kipato chetu na mwishowe baada ya kufanikiwa tutarejea katika mitindo ya kisasa na mahitaji tutakayo.
Huwezi kuchangia kila harusi na kila
sherehe. Anasa na tafrija zinachukua sehemu kubwa ya kipato usipokuwa makini
inawezekana ndiyo kikawa kikwazo cha uchumi wako. Muda huu ninapoandika makala
hii nina kadi tatu za harusi, Fikiri!
Ili kupunguza matumizi lazima uweze kusema ‘hapana’ au kusema ‘sina
pesa’ hata matajiri wakubwa kunavitu hawana uwezo navyo, ndiyo! There are some
stuff even millionaires cannot afford. Nyuma
ya matumizi ziko tabia, mihemko na hisia. Kupenda sana mavazi, ulevi, uvutaji
wa sigara, kuhonga wanawake, na ulafi. Haya ni mambo ambayo yanaongeza
matumizi na nyuma yake kuna kasumba mbaya ambazo zinahitaji tiba. Matumizi haya
yanaweza kupungua kama tabia hizo sitapatiwa tiba kwa kuamua kupunguza hatimaye
kuacha au kutubu na kugeuka.
Njia
rahisi za kupunguza matumizi ni kama:
Kununua vitu kwa jumla kwani rejareja ni ghali zaidi (buy in bulk), Kuwa na
mtindo rahisi wa kusuka au kujipamba ili kuondoa gharama za saluni, kubeba
chakula kutoka nyumbani badala ya kununua katika migahawa iliyoko ofisini,
epuka kupita katika maduka ili usijitamanishe (avoid window shopping),
kutengeneza vitu vya nyumbani kama juisi za matunda badala ya kununua zilizoandaliwa
tayari.
- Fanya kazi: Kazi si laana bali ni Baraka. Wito wa kuilima na kuitunza bustani ya Edeni [wito wa kazi] ulikuja kabla hata Adam na Eva hawajakosa kwa hiyo kazi si sehemu ya laana bali ni baraka. Unapoamka asubuhi kwenda kazini basi ujue unakwenda sehemu ya baraka [Mwanzo 2:15].
Mafanikio ya kiuchumi yanapaswa kuwa
ni matokeo ya kazi. Ndio maana huwezi kutajirika kwa hela ya kuokota au kwa
kucheza michezo ya kubeti. Ndoto au mipango ya kifedha bila kufanya kazi kwa
umakini na kwa bidii ni bure. Kupanga mipango tu haitoshi ni muhimu upange na
ushambulie [Dream and Fire]. Kuwa na malengo tu haitoshi ni lazima ulenge na
kufyatua.
Ni vizuri kutumia muda wa ziada
kutafuta kipato cha ziada kwa kuwa ni ziada ndiyo iletayo uhuru wa kifedha.
Omba (apply) kazi yenye maslahi bora au fanya kazi katika taasisi mbili kwa
wakati mmoja japo hii inachosha sana. Mungu alibariki ardhi na mifugo, ukilima
usisahau kufuga na mifugo. Jitahidi kufanya kazi na ziada kidogo. Work and a
little bit more
Wiki
Ijayo nitahitimisha makala yangu kwa kutaja njia nyingine nne Barikiwa…..
0 comments :