Weka imani yako .......
WEKA IMANI YAKO KATIKA KAZI TIMILIFU
YA YESU KRISTO
“Kwa maana yeye
aliyeingia katika raha yake amestarehe mwenyewe katika kazi yake, kama vile
Mungu alivyostarehe katika kazi zake…” Waebrania 4: 10
Kazi
yote aliyofanya Kristo hapa duniani haikuwa kwa ajili yake mwenyewe, ilikuwa ni
kwa ajili ya mimi na wewe. Alikufa ili sisi tupate kuwa hai, alichukua magonjwa
yetu ili sisi tupate kufurahia afya na uzima wake katika maisha yetu. Amechukua
huzuni, mahangaiko, masikitiko na mizigo yote katika maisha ili sisi tupate
amani na kustarehe kwa kazi yake. Kazi zote alizifanya kwa ajili yetu ili sisi
tupate kustarehe katika Yeye. Ikiwa Kristo amekufa msalabani kwa ajili ya
dhambi zetu, sisi hatuwezi kufa tena; bali tutastarehe katika kazi yake.
Njia
pekee ya sisi kuona na kufurahi matokeo ya utimilifu wa kazi ya Mungu katika
maisha yetu ni imani, Tunapoamini juu ya kazi yake katika eneo fulani la maisha
yetu ndipo hapo matokeo ya kazi hiyo hudhihirika. Ikiwa kuna jambo unahisi
limekuwa mzigo kwako[burden] na kukuelemea katika maisha yako au familia, kazi
zako au shughuli zako; mwaka huu unapoanza weka imani yako katika kazi timilifu
ya Yesu Kristo na katika Ahadi ya Neno lake. Kumbuka, Tunaitwa katika raha ya
Kristo kwa njia ya imani yetu katika kazi yake timilifu.
“Njoni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye
kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha” Mathayo 11:28
Unapoanza
mwaka mpya, wito wetu kwako ni kwamba, jifunze kuweka imani yako katika kazi
timilifu ya Yesu Kristo ili upate kuona Ukuu wa Mungu ukifunuliwa katika maisha
yako ndani mwaka huu. Ikiwa amesema atafanya jambo fulani katika maisha yako,
huna sababu ya kumsaidia kufanya kwa kuwa hofu au mahangaiko nafsini mwako;
kazi yako ni moja tu kuingia katika raha yake na kustarehe huku ukijua kuwa
Yeye anawajibika na maisha yako [Kutoka 14:14].
“Maana Yeye alisema, ikiwa; Na Yeye aliamuru,
ikasimama” Zaburi 33:9
Tunapoweka
imani katika kazi yake na ahadi yake, tunauhakika ya kwamba kila kitu kipo
katika mikono salama; hivyo hofu, mashaka, kuelemewa katika nafsi na mahangaiko
hutoweka. Unapoanza mwaka huu, amua kwa dhati kuweka imani yako katika kazi
timilifu na Ahadi yake, haijalishi mwaka jana hali ilikuwaje; kwa kuwa Bwana
anafanya jambo jipya. Mazingira ya mwaka jana, yasikukwamishe kumuamini Mungu katika mwaka huu mpya. Kumbuka jambo hili, Mungu anapotoa ahadi; kwake jambo hilo
limeshakamilika. Na tunapoamini ahadi hiyo, haiwi tu upendeleo bali inakuwa
haki yako kisheria [legal right].
“Lakini akiiona ahadi ya Mungu hakusita kwa
kutokuamini, bali alitiwa mguvu kwa imani, akimtukuza Mungu; huku akijua hakika
ya kuwa Mungu aweza kufanya [kudhihirisha] yale aliyoahidi. Kwa hiyo ilihesabiwa kwake
kuwa ni haki” Warumi4: 20-21 [Msisitizo umeongezwa]
Kazi
ya Yesu Kristo haikulenga tu katika kuleta utimilifu wa roho ya mtu
[anayeamini], lakini pia ililenga kuleta utimilifu wa nafsi, mwili na jamii
yake; ili kurejesha hadhi ya Kimungu katika maisha ya mtu huyo na mazingira
yake. Hivyo, unayohaki ya kumuamini Mungu ili Kazi zake, Ukuu wake na Uweza
wake uweze kuwa dhahiri [kufunuliwa] katika maisha yako, familia, watoto,
mipango, biashara, kazi, jamii au Taifa…nk. [Luka 4:18-19]
“Ni nani aliyesadiki habari tuliyoileta? Na
mkono wa Bwana amefunuliwa nani?” Isaya 53:1
Katika mwaka huu mpya 2016, Mwenyezi
Mungu akufadhili na kukuangazia Nuru ya uso wake.
Heri ya Mwaka Mpya 2016
0 comments :