Yesu ni mwalimu mwema
Tuyatii Maagizo Yake
Kijana
mmoja tajiri alimwendea Yesu na kumwita, “mwalimu mwema” naye Yesu akitaka sana
kumtukuza Baba wa Mbinguni akasema, “aliye mwema ni mmoja”. Kwa kawaida mtu
anapokusifu au anapokupa heshima yako huonesha utii kwa nafasi yako. Katika
dunia ya leo tunawasomi wanaoitwa daktari bigwa, Profesa, wako wahandisi hata
marubani.
Kuwasifia wataalamu hawa pasipo
kutekeleza wanachosema ni sawa na kufukuza upepo, ni kuwavisha kilemba cha
ukoka. Kumwita mtu Daktari bingwa hakuleti maana ikiwa akikikushauri jambo
lihusulo afya utakataa . Ni heri asiyemwita kwa cheo lakini akafuata maelekezo
yake. Vivyo hivyo haileti maana tumwitapo Yesu mwalimu ilhali hatufuati asemalo.
Ukimjua Yesu kama mwalimu mwema lazima ukubali kufanya asemalo hata kama kwa
akili za kawaida linaonekana ni la ki-puuzi au ni la kuaibisha.
“Ukimjua Yesu kama mwalimu mwema lazima ukubali kufanya asemalo hata kama kwa akili za kawaida linaonekana ni la ki-puuzi au ni la kuaibisha”
“Na
tazama, mtu mmoja akamwendea akamwambia, Mwalimu, nitende jambo gani jema, ili
nipate uzima wa milele? Akamwambia Kwani kuniuliza habari ya
wema? Aliye mwema ni mmoja. Lakini ukitaka kuingia katika uzima, zishike amri. Akamwambia, Zipi? Yesu akasema, Ni hizi, Usiue, Usizini, Usiibe,
Usishuhudie uongo, Waheshimu baba yako na mama yako, na, Mpende
jirani yako kama nafsi yako. Yule kijana akamwambia, Haya yote
nimeyashika; nimepungukiwa na nini tena? Yesu akamwambia, Ukitaka kuwa mkamilifu, enenda ukauze ulivyo navyo,
uwape maskini, nawe utakuwa na hazina mbinguni; kisha njoo unifuate. Yule kijana alipolisikia neno lile, akaenda zake kwa huzuni; kwa sababu
alikuwa na mali nyingi.” Mathayo 19:17-22
Licha
ya kumwita Yesu mwalimu mwema yaani, “Good Master” lakini kijana hakukubali
ushauri wa Yesu. Alipoambiwa auze kila kitu na kuwapa masikini hakukubali.
Anajua Yesu ni mwalimu mwema, anajua Yesu ni mtaalamu wa roho, mwili na nafisi
za wanadamu lakini hataki kumtii
anachosema. Alijua Yesu ni kila kitu lakini hakutaka kumsikia. Wako wengi
wanamwita Yesu Bwana, wengine wanasema, “nakupenda Yesu” lakini hawataki kutii
neno lake. Yeye mwenyewe anasema, “mkinipenda mtalishika neno langu”
Naamani
Yule Jemedari anafanana na huyu kijana tajiri. Yeye alipokwenda kwa Elisha
nabii hakutaka kujichovya mtoni mara saba. Alitaka Elisha amwekee mkono. Mara
nyingi tunapokwenda mbele za Mungu tunakosea, tunakwenda kumwagiza badala ya
kwenda kumsikiliza. Mungu anaweza asiseme na wewe kwa njozi, wala kwa nabii
wala kwa dalili. Lakini kupitia neno lake (Biblia) anasema nasi kila siku. Kila
tunaposoma maandiko tunasikia sauti ya Mungu. Biblia ni redio yake, isome na
usikilize. Naamani hakutaka kusikia maagizo ya nabii bali alitaka nabii ndiye
afuate mawazo na maagizo yake. “Lakini Naamani akakasirika, akaondoka, akasema, Tazama,
nalidhania, Bila shaka atatoka kwangu, na kusimama, na kuomba kwa jina la
Bwana, Mungu wake, na kupitisha mkono wake mahali penye ugonjwa, na kuniponya
mimi mwenye ukoma.”2 Wafalme 5:11
Jambo
zuri ni kwamba, kijana tajiri alimuuliza Yesu swali ambalo kila mwenye akili
timamu anapaswa kujiuliza. Mtu mzima hapaswi kujiuliza maswali ya kisiasi tu,
bali anapaswa kujiuliza maswali yahusuyo umilele wake na watoto wake. Kijana
akamuuliza Yesu, “nifanye nini ili nirithi uzima wa milele?”. Hakuuliza kwa
habari ya Simba na Yanga, wala hakuuliza kwa habari ya CHADEMA na CCM, hakugusa
habari za kuoa na kuolewa wala hakuhoji kwa habari ya Manchester United na
Arsenal bali alihoji kuhusu uzima wa milele. Kwa hili ninampongeza. Kila mwenye
hekima ni lazima ajue atakuwa wapi baada ya kifo. Swali hili linapaswa kutawala
akili ya kila mwanadamu. Uzima wa milele! Uzima wa milele! Uzima wa milele!
“Si vibaya kumiliki pesa, lakini ni hatari kama pesa zitatumiliki sisi hata tushindwe kumpa Mungu nafasi ya kwanza””
Yesu
akimjibu Yule kijana alimwambia akitaka uzima wa milele azishike amri, wewe na
mimi pia tukitaka uzima wa milele ni muhimu tuzishike amri zake Mungu. Si
vibaya kumiliki pesa, lakini ni hatari kama pesa zitatumiliki sisi hata
tushindwe kumpa Mungu nafasi ya kwanza. Yule kijana aliiona ni heri akose
ukamilifu lakini abakie na pesa. Aliona bora akose furaha lakini abakie na
pesa. Aliondoka kwa huzuni, watu wengi wana pesa lakini hawana furaha ya kweli,
mali zao zimewatenga na ukamilifu.
Uzima
wa milele unapatika kwa kumwamini BWANA YESU. Tena kila aliaminiye jina lake
anao uzima wa milele. Ukimwamini leo na kuisikia sauti yake utaokoka. Usimwite
BWANA kama hutaki kufanya aliyokuamuru yaani, kushika amri zake.
Siku
ya mwisho Yesu atawaita mashahidi wawili, ataliita neno lake na kupima utii
wetu kwa neno lake. Agano jipya ni shahidi wa pili na Agano la kale ni shahidi
kwanza. Mashahidi hawa wawili watapima utendaji wetu wa neno. “Nami nitawaruhusu mashahidi wangu
wawili,”Ufunuo 11:3a
0 comments :